Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mastaa waipa Yanga mbinu mpya

IMG 4176 Yanga 1 2 Usm.jpeg Mastaa waipa Yanga mbinu mpya

Wed, 31 May 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kuna ishu ya kiufundi waliyoiona wataalamu wa soka, inayoweza ikawasaidia Yanga kupindua meza ugenini dhidi ya USM Alger, mchezo utakaoamua nani bingwa wa Kombe la Shirikisho la Afrika, utakaopigwa Juni 3.

kitendo cha Yanga kupoteza kwa mabao 2-1 Uwanja wa Benjamin Mkapa, hakukusababishwa na wachezaji kucheza chini ya kiwango, isipokuwa ni namna walivyotumia nguvu zao dakika 90, wakati Alger ilitumia nguvu hizo kwa malengo ya kusaka bao tu.

Beki wa zamani wa timu hiyo, William Mtendamema alisema wachezaji walijituma na kucheza kwa kiwango kizuri, kilichowaangusha ni aina ya uchezaji wa Alger ambao dakika 90 wanaangalia zaidi fursa na matumizi ya nguvu ya kuwapa matokeo tu, baada ya hapo ikawa ni mwendo wa kujiangusha.

"Baada ya kupata bao la kuongoza walikuwa wanatumia muda mwingi kujiangusha lengo lao lilikuwa ni kuhifadhi nguvu zao, wakati huohuo wachezaji wa Yanga walitumia nguvu muda wote kuhakikisha wanasazawazisha na kupata ushindi.

"Baada ya Yanga kusawazisha bao, Alger ilirejea na nguvu ya kusaka bao walipofunga la pili waliendelea kupunguza matumizi ya nguvu zao wakaanza kuziba mianya ya kushambuliwa na wakawa wanajiangusha muda mwingi ile siyo bahati mbaya kwao ni mbinu za mchezo, chakufanya Yanga wanatakiwa kwenda kupata mabao ya mapema ambayo yatawavuruga.

Kwa upande wa beki wa zamani wa Simba, Boniface Pawasa alisema Yanga wanapaswa kuwafunga mabao mengi dakika za mapema na wanatakiwa kuchunga dakika za mwanzo na za mwisho, hilo linatokana na aina ya uchezaji wao.

"Waarabu wana mipango mingi, ndio maana wakiongoza utawaona wazembe, sasa wakianza kusaka bao watakupa picha nyingine kukuonyesha wanajua soka, ndio maana matumizi yao ya nguvu wanatumia sana akili kujua nini wafanye na kwa muda gani, Yanga ilicheza vizuri, wajipange vizuri kwa hilo tu," alisema.

Kwa upande wa kocha wa zamani wa Simba, Abdallah Kibadeni alisema :"Wachezaji wanatakiwa wajitambue kuwa ni wakati gani wanahitaji bao ili wasitoke kwenye mwelekeo ijapokuwa wapinzani wanaonekana kuwa na mbinu ya kupoteza muda kwa kujiangusha hii itawasaidia kuwasoma na kujua nini wakifanye."

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: