Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mastaa waanika tatizo la Simba lilipo

Simba Kiko Chamazi.jpeg Kikosi cha Simba

Sun, 16 Jun 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Hakuna ubishi hali ndani ya klabu ya Simba sio shwari. Misimu mitatu mfululizo ya kutoka kapa katika michuano ya Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho ni mambo yaliyochafua hali ya hewa Msimbazi.

Kumaliza nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu iliyomalizika hivi karibuni na kukosa tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika ni jambo jingine lililowatibua Wanasimba.

Ilianza kama utani baada ya kuelezwa, Rais wa Heshima na bilionea anayetambuliwa kama mwekezaji wa Simba, hata kama mchakato wa mabadiliko ya klabu hiyo kuendeshwa kwa mfumo wa hisa ukiwa bado, Mohammed ‘Mo’ Dewji amewalazimisha Mwenyekiti na wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi kujiuzulu.

Licha ya jitihada za kukanushwa kwa taarifa hizo, ukweli ulibainika baada ya wajumbe wanne akiwamo Rashid Shangazi, Raphael Chageni, Hamza Johari na Zulfikar Chandoo walitajwa kujiuzulu mapema na Shangazi aliweka bayana sababu ya kufanya hivyo akiwa mjini Dodoma.

Siku chache zilizopita Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Salim Abdallah ‘Try Again’ akajitokeza na kuweka bayana amejiuzulu nafasi hiyo na kupendekeza Rais wa Heshima, Mo Dewji aishikilie nafasi hiyo na kumwomba amteua ikimpenda.

Kweli buana, Mo Dewji naye akaibuka na kuweka baya kuridhia uamuzi wa Try Again wa kujiuzulu na kubeba jukumu la kuiongoza Simba kama Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi nafasi aliyokuwa akiishikilia kabla ya kumteua Try Again aishikilie na kutangaz a pia kumrejesha Try Again kuwa mjumbe.

Hali ikiwa hivyo kwa upande wa mwekezaji, kule kwa uongozi Mwenyekiti na baadhi ya wajumbe waliochaguliwa kwenye Uchaguzi Mkuu uliopita nao wakayasema yao na kutoa misimamo ambayo ni kama inazidi kuivuruga klabu kiasi Mjumbe wa Baraza la Ushauri la klabu hiyo, Swedi Mkwabi kutoa ushauri.

Mkwabi aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Simba, aliwataka viongozi wenzake kwenda kuyamaliza mambo yao kwenye vikao vya ndani badala ya kutumia vyombo vya habari na mitandao kuumbuana, kwani inaleta aibu kwa klabu nzima.

TATIZO LIPO HAPA

Ukiachana na ukweli hadi sasa Simba bado haijakamilisha mchakato wa mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji inayoendelea kutumiwa kwa sasa, lakini ukweli ni wanasimba na hata viongozi wa klabu hiyo wanalumbana na kuiweka katika mtego klabu yao, bila kijua kinachoitafuna.

Ukweli ni, ukiachana na Mo Dewji kutambulika kama mwekezaji wa klabu kwa kilichoelezwa ameshaweka Sh 20 Bilioni ambazo hata hivyo hakuna mwanachama anayejua zimeingizwa kwenye akaunti ipi, lakini hata nguvu ya mwenyekiti wa klabu kwa upande wa wanachama wanaotajwa kuwa na hisa 51 hana nguvu, kwani akiingia kwenye vikao vya Bodi ya Wakurugenzi anakuwa Mjumbe asiye na nguvu.

Nguvu kubwa ipo kwa upande wa mwekezaji unaotajwa kuwa na asilimia 49 za hisa ambazo hata hivyo bado hazijagawanywa kwa vile mchakato umekwamia njiani, unaoongozwa na Mo Dewji aliyetangaza kurejea tena kuwa Mwenyekiti wa Bodi, huku Mangungu akinukuliwa atatambuliwa akipigiwa kura na si vinginevyo.

Hata hivyo, yote kwa yote imebainika udhaifu uliopo katika katiba ya klabu hiyo ya mwaka 2018 iliyofanyiwa marekebisho Januari mwaka huu ndio kiini cha sarakasi zote, ikiwamo suala la Mo Dewji kuingia na kutoka katika nafasi ya Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi iliyoelezwa ni lazima apigiwe kura ili kuidhinishwa.

Ukiisoma katiba nzima ya Simba, haionyeshi suala hilo la Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi kupigiwa kura na wajumbe wanaounda bodi hiyo wakiwamo wale wa upande wa wanachama unaoongoza na Mangungu wala wale wa upande wa mwekezaji (Mo Dewji) ambaye hata hivyo hatambuliki kisheria kwa vile mchakato mzima wa mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji bado haujakamilika.

Sehemu ya III ya katiba hiyo ikielezea Muundo wa vyombo vya Utendaji vya klabu hiyo ya Simba Sports Club Company Limited ikiainishwa katika Ibara ya 17 ikitaja Mkutano Mkuu, Bodi ya Wakurugenzi, Sekretarietu, Vyombo vya Haki, Kamati ya Uchaguzi Mkuu, Baraza la Wadhamini, Matawi, Uongozi wa Vialaya na Mikoa wa Simba SC nchi nzima na Baraza la Ushauri.

Katika eneo la Bodi ya Wakurugenzi iliyoanishwa muundo wake katika Ibara ya 29 kipengele cha cha 1-4 chenye kifungo cha (a-e) hakuna sehemu inaonyesha kama Mwenyekiti wa Bodi atapigiwa kura ili kushika nafasi hiyo, japo Ibara ya 50 ya katiba hiyo inatoa mwanya kwa kueleza inadili na mambo yasiyoainishiwa katika katiba moja kwa moja.

Ibara hiyo ya 50 ya masuala yasiyoelezwa katika katiba inasomeka hivi; Suala lolote lisiloelezwa katika katiba hii au kwa mambo yasiyozuilika, lazima yashughulikiwe na Bodi ya Wakurugenzi. Hakuna Rufaa itakayokatwa dhidi ya maamuzi yatakayotolewa na Bodi ya Wakurugenzi inayoainishwa katika kifungo za (3) cha Ibara wa 30 muda wa madaraka ya wajumbe wake kwa kusema; endapo itatokea nafasi yoyote ya Bodi ya Wakurugenzi kuwa wazi, katika Mkutano Mkuu wa kawaida unaofuata nafasi hiyo zitajazwa kwa kuchaguliwa wajumbe wengine kwa kipindi kilichobaki cha mamlaka.

Mwanaspoti iliyo na nakala ya katiba hiyo iliyorekebishwa na kuidhinishwa na Msajili wa Vyama na Klabu za Michezo wa Taifa, Mei 13 mwaka huu imebaini kuna mapengo mengi ya katiba hiyo ambayo kwa namna moja au nyingine inaleta mgongano ambao Wanasimba wanashindwa kuushughulikia.

Suala la utata wa katiba ya Simba na mchakato wa mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji ulishalalamikiwa na mmoja wa waasisi wa klabu hiyo, Hamis Kilomoni na hata baadhi ya viongozi na wanachama wa klabu hiyo, lakini hata ulipofanyika Mkutano wa Dharura Januari mwaka huu na kurekebishwa kwa vipengele vitano kati ya sita zilivyopendekezwa, bado tatizo limebaki kama lilivyo na kutofahamika Simba iwe na nguvu upande upi, wa mwekezaji mwenye hisa 49 au wanachama wenye 51 ambao hawana meno kwa sasa.

WASIKIE WADAU

Kwa ishu ya Mo kurudi tena kama Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi baada ya awali kujiuzulu na kumteua Try Again, mwenyekiti wa zamani wa klabu hiyo ya Simba, Swedi Mkwabi amesema hakuna shida kama alivyoombwa na Salim Abdallah ‘Try Again’ aliyachia ngazi hivi karibuni.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mkwabi alisema haoni shida kwa sababu Mo, ndiye aliyemteua Try Again kukaa katika nafasi hiyo wakati anajiweka pembeni mwaka 2021.

“Nawashauri wajumbe wa Bodi kukaa chini pamoja ili waweze kutoa tofauti zao, kama watashindwa kuna Baraza la Ushauri ambalo mimi ni mjumbe tukae tujenge timu yetu, Simba haijafanya vizuri msimu ulioisha hivyo wanachama na mashabiki wanatuangalia sisi viongozi kujua nini tunafanya,” alisema Mkwabi na kuongeza;

“Walioamua kujiuzuru kwa kutowajibika vizuri wamefanya uamuzi wa busara, waliobaki watumie muda huu kujipanga kutengeneza Simba imara kwani wanachama, mashabiki na wapenzi wa Simba wamewapa dhamana wao.”

Mkwabi alisema kama kuna jambo la dharula ambalo limekuwa kubwa sana waite mkutano wa dharula waongee na wanachama waachane na mambo ya kuzungumza kwenye vyombo vya habari wanaongeza hali ya sintofahamu kwa wanachama.

Huku, Kipa wa zamani wa kimataif aliyewahi kucheza CDA, Simba, Yanga, Majimaji, Mtibwa Sugar na Taifa Stars, Steven Nemes, alisema;

“Mpira wa Tanzania unaendeshwa kwa matakwa ya watu binafsi na sio kufuata katiba, naamini baadae watakaa pamoja na kumaliza tofauti zao tayari kwa ajili ya kuiendeleza timu hiyo,” alisema Nemes na kuongeza;

“Shida iliyopo ni kutofuatwa kwa katiba ya klabu, wanatakiwa kukutana na kukaa pamoja ili waweze kulimaliza na kutengeneza timu ya ushindani.”

“Kuna utofauti mkubwa kati ya Yanga, Azam FC na Simba, ukiangalia timu mbili za mwanzo zilijijenga vizuri hivyo Wanasimba wanatakiwa kujenga umoja na mshikamano ili waweze kuirudisha timu kwenye ushindani,” alisema.

Nyota mwingine wa klabu hiyo, Zamoyoni Mogella ‘Golden Boy’, aliffanua;  “Ukiangalia haya yote yanayoendelea unayaona yanatokana na tatizo la Katiba lililopo, ndiyo maana unaona anatokea mmoja wao kwa utashi wake anajichukulia maamuzi ya kumchagua mtu bila ya kufuata misingi ya chombo kinachowaongoza,” alisema Mogella aliyewahi kuwika na Tumbaku, Yanga na Volcano ya Kenya.

Mogella aliongeza, hata sakata la mchakato wa mabadiliko ya klabu hiyo kuchukua muda mrefu kukamilika linatokana na ishu nzima ya Katiba, hivyo ni jukumu la Wanachama kukaa chini na kuangalia namna nzuri ya kutatua changamoto wanayopitia kwa sasa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live