Staa wa zamani wa Simba, Yusuph Mgwao amesema enzi zao kwenye pambano la watani wa jadi wachezaji walikuwa katika presha kubwa na wengi wao walitamani kukaa jukwaani kwa sababu aliyefanya vizuri mambo yalikuwa poa kwake, ilhali aliyeharibu kazi alikuwa nayo.
Simba na Yanga watakipiga katika mchezo wa Ligi Kuu keshokutwa katika Uwanja wa Benjamini Mkapa ambapo wababe hao wa soka nchini watachuana kusaka pointi tatu ili kukoleza mbio za ubingwa.
Akizungumza Mgwao alisema enzi zao mechi hiyo iliweza kujenga mchezaji na kumpa umaarufu mkubwa iwapo atamaliza akiwa katika kiwango bora, lakini kwa aliyeharibu maisha ya soka yaligeuka kuwa magumu.
Alisema wachezaji wengi walikuwa na hofu jambo ambalo wengi wao walitamani zaidi liwapite kwa kukaa benchi au jukwaani kuhofia kutofanya vizuri ili kutoandamwa na mashabiki na viongozi hasa ikitokea wamefungwa.
“Ukiharibu utashutumiwa, hakuna atakayeona kama ulifanya kosa la kimchezo. Utaandamwa sana na wengine watakuambia umeuza mechi na mchezaji ukiwa na roho nyepesi basi maisha yako ya soka yanaweza kuishia hapo, hivyo wengi walikuwa wanaogopa inapofika hizi mechi za watani wa jadi," alisema Mgwao.
Hata hiyo, aliwasifia viongozi na mashabiki wa soka wa sasa wa timu hizo kuwa waelewa, hivyo mchezaji akifanya kosa la kibinadamu katika pambano hilo huchukuliwa kosa la kawaida jambo ambalo nyota wengi wanatamani kucheza mechi hiyo.
“Ndiyo maana unaona kwa sasa wachezaji wanatamani kupangwa kwenye mchezo huu kwa sababu watacheza bila hofu. Hata ikitokea mkafungwa inakuwa sehemu ya mchezo, lakini zamani mkipoteza basi ataanza kutafutwa mchawi," alisema straika huyo.