Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mastaa matajiri AFCON 2023

Mo Salah Pfa Mastaa matajiri AFCON 2023

Sat, 6 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Siku zinazidi kukatika na fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) zinazotarajiwa kuanza Januari 13, kule  Ivory Coast zinazidi kukaribia. Timu nyingi tayari zimeshaingia kwenye kambi za maandalizi kwa ajili ya michuano hiyo mikubwa zaidi ya kimataifa kwa Bara la Afrika.

Wachezaji kutoka sehemu mbalimbali duniani wameshawasili kwenye mataifa yao kwa ajili ya kuyatumikia. Mastaa hawa wengi wanatajwa kuwa na utajiri mkubwa. Leo tumekuletea wachezaji 10 waliopiga pesa ndefu mwaka jana ambao watakuwepo kwenye AFCON, pesa hizi ni kupitia mishahara na mikataba yao ya nje ya uwanja.

10. Edouard Mendy, Senegal — Dola 13 milioni

Staa huyu mwenye umri wa miaka 31 ambaye anaichezea Timu ya Taifa ya Senegal, kwa mwaka anapata Dola 13 milioni ambazo Dola 12 milioni huzivuna kutoka kwenye mshahara wake na Dola 1 milioni ni kwenye madili mengine ya nje uwanja.

Ni mmoja kati ya mastaa walioitwa kwenye kikosi cha Senegal kitakachoshiriki AFCON ambao wanaingiza pesa nyingi zaidi.

Ameingia kwenye orodha hii baada ya kukamilisha uhamisho wa kibosi wa kujiunga na Al Hilal ya Saudi Arabia katika dirisha lililopita la majira ya kiangazi.

9. Sebastien Haller, Ivory Coast — Dola 14 milioni

Wenyeji wa mashindano haya wanajivunia mdunguaji huyu ambaye anaichezea Borussia Dortmund. Amepita kwenye vikosi mbalimbali barani Ulaya ikiwa pamoja na Ajax, West Ham na Eintracht Frankfurt.

Mwaka 2022 alipimwa na kukutwa na saratani lakini alipatiwa matibabu na akarejea kwenye majukumu yake mwaka jana.

Kwa sasa yeye ndiye mchezaji wa pili anayelipwa pesa nyingi zaidi kwenye kikosi cha Dortmund akizidiwa na Nikolas Sule ambaye anapata Pauni 9.4 milioni kwa mwaka.

Mbali ya mshahara wa Dola 12 milioni ambao Sebastian anaupata, pia anakunja pesa nje ya uwanja kupitia mikataba yake ya ubalozi na kampuni mbalimbali ikiwamo ya vifaa vya michezo ya Puma.

8. Seko Fofana, Ivory Coast — Dola 16 milioni

Huyu ndiye mchezaji kutoka Ivory Coast anayepokea mshahara mkubwa zaidi mbali ya madili ya nje ya uwanja.

Anatokea kwenye ardhi inapofanyika Mashindano ya AFCON mwaka huu, Ivory Coast. Seko Fofana amekuwa mmoja kati ya wachezaji wanaolipwa sana baada ya kuondoka RC Lens na kutua Al Nassr katika dirisha lililopita la majira ya kiangazi.

Ndani ya Al Nassr amepewa mkataba huu unaomuwezesha kupata mshahara mara 10 zaidi ya ule ambao alikuwa akiupata Lens.

7. Thomas Partey, Ghana — Dola 16 milioni

Licha ya majeraha ya mara kwa mara ambayo amekuwa akikumbana nayo, jamaa pochi lake bado limenona. Partey ambaye anatarajiwa kuwapo kwenye mashindano ya mwaka huu, anapokea mshahara wa Dola 13 milioni kwa mwaka ndani ya Arsenal, pia anatapata Dola 3 milioni kutoka katika kampuni ya vifaa vya michezo ya Adidas.

Hiyo inamfanya kupata Dola 16 milioni kwa mwaka.

Kwenye michuano ya AFCON mwaka huu atakuwa na kikosi cha Ghana ingawa bado kuna wasi wasi kuhusiana na afya yake.

6. Franck Kessie, Ivory Coast — Dola 17 milioni

Baada ya kuisaidia Barcelona kushinda taji la Ligi Kuu Hispania mwaka jana, kiungo huyu raia wa Ivory Coast alitimkia zake Saudi Arabia kujiunga na Al Alhi ambako anavuta mkwanja sio wa kitoto.

Naye ni mmoja kati ya mastaa watakaoitumikia timu ya taifa ya Ivory Coast kwenye mashindano ya AFCON mwaka huu.

Anapokea mshahara wa Dola 15 milioni na anakunja Dola 2 milioni kupitia mikataba yake ya ubalozi ikiwemo ule wa Adidas.

5. Achraf Hakimi, Morocco — Dola 20 milioni

Mwaka jana alitawala vichwa vya habari duniani kutokana na mgogoro wake na mkewe. Staa huyu wa kimataifa wa Morocco ambaye kwa sasa anaichezea PSG kwa mwaka anapata mshahara wa Dola 15 milioni.

Amewahi kuichezea Real Madrid, Borussia Dortmund na Inter Milan na kwa sasa huyu ndio mchezaji anayelipwa zaidi kutoka Morocco.

Staa huyu mwenye umri wa miaka 24, mbali ya mshahara wake pia anapata Dola 5 milioni kupitia mikataba mbalimbali ya udhamini aliyoingia na kampuni za Adidas UK, Pepsi, Huawei, Puma na Beats by Dre.

4. Kalidou Koulibaly, Senegal — Dola 26 milioni

Ni mmoja kati ya mabeki wa kati bora kutoka Senegal. Alionyesha kiwango bora alipokuwa akiichezea Napoli kwa zaidi ya miaka saba kabla ya kujiunga na Chelsea ambapo mambo yalimuendea kombo.

Baada ya mambo kuwa mabaya alijiunga na Al Hilal ya Saudi Arabia katika dirisha lililopita la majira ya kiangazi ambako amesaini mkataba wa Dola 26 milioni.

3. Riyad Mahrez, Algeria — Dola 32 milioni

Riyad Mahrez alipata mafanikio sana alipokuwa akiichezea Manchester City kabla hajajiunga na A Ahli ya Saudi Arabia kwenye dirisha lililopita la majira ya kiangazi.

Huko anapata mshahara wa Dola 30 milioni kwa mwaka na pia anapata Dola 2 milioni kwa mwaka kupitia mikataba yake na Pepsi na Nike.

Huyu ndio kapteni wa timu ya taifa ya Algeria.

2. Sadio Mane, Senegal — Dola 52 milioni

Alichomzidi Mohamed Salah ni mshahara tu ambapo anapokea Dola 48 milioni kwa mwaka na kwenye upande wa vyanzo vingine vya mapato hususani madili ya ubalozi Mane anapata Dola 4 milioni.

Mane aliisaidia Senegal kuchukua ubingwa wa mashindano yaliyopita ya AFCON 2021 baada ya kuwafunga mabingwa mara saba wa michuano hiyo Misri kwa penalti 4-2 na sasa mwaka huu atakuwa na kazi ya kuhakikisha wanaendelea kulilinda taji hilo.

Kwa sasa anaichezea Al Nassr ambapo yupo na Cristiano Ronaldo.

1. Mohamed Salah, Misri — Dola 53 milioni

Mohamed Salah ndiye anayeongoza kwenye orodha hii, staa huyu kutoka Liverpool anapokea mshahara unaofikia Pauni 400,000 kwa wiki. Katika dirisha lililopita alipata ofa nono ya kwenda Saudi Arabia ambako Al Ittihad ilitaka kumsajili lakini alikataa.

Anapokea Dola 35 milioni kwa mwaka kupitia mshahara wake na Dola 18 milioni kutoka kwenye mikataba yake mbalimbali ya ubalozi wa Kampuni za Vidafone, Pepsi na Adidas.

Salah sasa ndiye mfungaji kinara wa muda wote wa Misri katika mechi za kufuzu ushiriki wa Kombe la Dunia, akiwa na mabao 15. Kwa ujumla, Salah  ameifungia Misri mabao 55 katika mechi 94 za kimataifa. Straika mstaafu Hossam Hassan ndiye aliyemzidi Mo Salah katika orodha ya muda wote ya walioifungia Misri mabao mengi, akiifungia mabao 68 katika mechi 176 kuanzia mwaka 1985 hadi 2006.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live