Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mastaa kambini Yanga wamzungumzia Joseph Guede

Joseph Guede Yanga Joseph Guédé Gnadou

Sat, 17 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakati Yanga ikishuka leo kukichapa na KMC katika Uwanja wa Jamuhuri, Morogoro, mastaa wa kikosi hicho akiwemo Pacome Zouzoua wameonyesha imani juu ya straika Joseph Guede.

Nyota huyo aliyesajiliwa dirisha dogo msimu huu, amecheza mechi nne bila kufunga bao akifikisha dakika 225, huku matarajio ya mashabiki wengi yakiwa hayajatimia.

Nahodha msaidizi na beki wa kikosi hicho, Dickson Job alisema katika kipindi kifupi alichomuona mazoezini mpaka kwenye mechi amebaini kuwa ni mshambuliaji mzuri ila bado kitu kidogo tu.

“Anajua kutoa pasi vizuri na sio mchoyo kabisa anapokuwa uwanjani, lakini matokeo sio ishu japo kwa nafasi yake inahitaji hilo. Kikubwa ni kwamba ana uwezo wa kubadilisha mchezo,” alisema Job.

“Muda sio mrefu mashabiki watasahau kuhusu hizo lawama wanazotoa sasa kwani akichanganya tu na kuzoea mazingira basi wataongea hadithi nyingine.”

Kiungo Pacome Zouzua alisema kuwa hata yeye wakati anafika haikuwa rahisi kuingia kwenye mfumo na kuonyesha uwezo kwani katika kitu kigumu ni kuzoeana na wachezaji wengine na wanatofautiana kiuchezaji.

“Mabao yatakuja tu anahitaji muda zaidi ukizingatia bado anapewa nafasi, basi hakuna kinachoshindikana, lakini pia ni mchezaji mkubwa sana.

“Amecheza timu nyingi ana uzoefu. Anachohitaji ni muda wa kuzoea mazingira. Mchezaji anaweza kuwa kimya hata  msimu mzima ila akija kuwaka hazimi kizembe mifano ipo mingi tu,” alisema.

Nickson Kibabage aliyewahi kucheza naye Ligi Kuu Morocco akiwa katika kikosi cha Difaa Al Jadida ya Morocco, alisema hakumuona katika mechi moja kwani amekutana naye sana tu na alimshuhudia akiwa FAR Rabat katika ubora wa juu.

“Bado hajacheza kama ninavyomfahamu, ila haraka huwa hazina baraka hivyo nina imani juu ya kile alichonacho na kwa mtu anayejua mpira akimuona tu anajua kuwa Guede ana kitu,” alisema.

“Muda wowote mchezaji anaweza kubadilisha upepo na wakamshangaa ila miguu yake ina kitu na anajua kucheza mipira ya juu hata chini. Pia kinachohitajika ni utulivu tu.”

Ikumbukwe kuwa kabla ya kutua Yanga, Guede alikuwa nje kwa miezi minne baada ya kumalizana na timu ya Tuzlaspor ya Uturuki na huenda akawa anahitaji muda zaidi kutokana na sababu hiyo. Wapo wachezaji ambao walishawahi kupitia changamoto kama ya mshambuliaji huyo, lakini baadaye walikuja kuonyesha kiwango bora na mfano niLomalisi Mutambala na Jesus Moloko

Katika hatua nyingine, Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi alisema sio sahihi kuwalinganisha Pacome Zouzoua, Attohoula Yao na Maxi Nzengeli na kina Joseph Guede Augustine Okrah.

“Kwa upande wa Guede na Okrah ni wachezaji ambao ni bora na wamenionyesha wana kitu, lakini wanahitaji muda zaidi ili kuweza kuingia kwenye mfumo na kuwa bora zaidi ya walivyo sasa.

“Sitaki kumtaja mchezaji mmojammoja sio nzuri kwangu kwa sababu nafanya kazi na wachezaji wote, lakini nafurahia kuona kuna wachezaji ndio kwanza wamesajiliwa ila wameingia moja kwa moja kwenye mfumo na wananipa matokeo.” alisema.

Gamondi alisema hana shida na Guede na Okrah, lakini wanahitaji muda zaidi ili kuingia kwenye mfumo na ataendelea kuwapa nafasi hadi mwisho wa msimu akiamini watampa kitu.

Akizungumzia wachezaji wake kuendelea kuwa imara licha ya kucheza mechi mfululizo, alisema mbinu za mazoezi mara baada ya mchezo na wachezaji wenyewe ndio siri kubwa ya ubora.

“Mashabiki na wanachama wa Yanga wanatakiwa kuwa na furaha juu ya timu yao kwa sababu wachezaji wao wamekuwa wakipambana kuhakikisha hawawaangushi. Licha ya changamoto wanazopitia wana kikosi bora na imara.” Matokeo mabaya yanawapa mbinu za kupambana zaidi, hivyo pia matokeo mazuri yanawapa nafasi ya kuendeleza walipoishia huku akikiri kuwa timu yake ina wachezaji bora na wapambanaji ndio siri ya mafanikio.

Gamondi alisema benchi la ufundi likiwa na mbinu bora bila ya wachezaji bora hakuna wanachoweza kufanya, na anafurahi kuwa na kikosi imara licha ya kufanya makosa modogomadogo, lakini anaamini wote wanaangalia mafanikio zaidi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live