Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mastaa hawa wapo hoi sokoni, thamani zimeshuka

Andy Robertson Real Beki wa Liverpool, Andy Robertson

Thu, 6 Jul 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Tovuti ya soka ya TransferMarkt imetoa orodha ya wachezaji ambao thamani zao zimeshuka kwa kiwango kikubwa sana katika kipindi cha msimu mmoja uliopita.

Ishu ya umri, majeruhi na kushuka kiwango kumesababisha mastaa hawa 10 ambao thamani zao sokoni zimeshuka kwa kiwango kikubwa sana, akiwamo staa wa zamani wa Manchester United, ambaye thamani yake imeshuka kwa asilimia 69 ndani ya mwaka mmoja tu.

Sadio Mane

Mane, 31, alikuwa mmoja wa majembe matata kabisa kwenye kikosi cha Liverpool chini ya Kocha Jurgen Klopp kabla ya kutimkia zake Bayern Munich kwenye dirisha la majira ya kiangazi la mwaka jana kwa ada ya Pauni 27.5 milioni.

Msenegali huyo alitazamwa kama mtu mwafaka wa kwenda kuchukua buti za Robert Lewandowski, lakini kilichotokea huko Bavaria ni majanga. Majeruhi yamemtibulia sana. Thamani yake ya sasa sokoni ni Pauni 21.5 milioni ikiwa ni anguko la asilimia 39 kutoka thamani yake ya mwaka jana ya Pauni 60.5 milioni.

Wilfred Ndidi

Ndidi, 26, alikuwa kwenye kiwango bora sana katika msimu wa 2021-22 uliomshuhudia akiwa mmoja wa viungo mahiri kabisa wa kukaba kwenye Ligi Kuu England. Thamani yake ya mwaka jana ya Pauni 41.5 milioni ilikuja kipindi ambacho klabu kubwa kubwa huko Ulaya zilikuwa zikipambana kunasa saini yake.

Lakini, baada ya kucheza ovyo na kufanya Leicester City kushuka daraja, jambo hilo limeshusha thamani ya Ndidi kwa zaidi ya asilimia 58 na hivyo sasa kuthaminishwa kuwa na thamani ya Pauni 21.5 milioni. Pauni 30 milioni zimeondoka.

Paul Pogba

Pogba aliwahi kuwa mwanasoka ghali zaidi duniani wakati alipohama Juventus kwenda Manchester United kwa ada ya Pauni 89 milioni mwaka 2016. Lakini, kiungo huyo hakuwahi kucheza kwa kiwango cha kuthibitisha thamani ya pesa yake alipotua Old Trafford kabla ya kuondoka bure akirudi Juventus baada ya mkataba wake kumalizika mwaka jana.

Alicheza mechi 10 tu kikosini Juventus kwa msimu uliopita kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya goti na kufanya thamani yake kushuka hadi Pauni 13 milioni kutoka Pauni 41 milioni ikiwa ni anguko la asilimia 69.

Jadon Sancho

Sancho alitua Manchester United kama moja ya usajili mkubwa kabisa miaka miwili iliyopita kwenye dirisha la majira ya kiangazi mwaka 2021. Winga huyo ameshindwa kuthibitisha thamani yake halisi ya pesa ya Pauni 73 milioni iliyolipwa kupata huduma yake.

Sasa anatajwa kama mmoja wa wachezaji wanaoweza kufunguliwa mlango wa kutokea huko Man United kwenye dirisha hili. Thamani yake sokoni sasa imeshuka hadi Pauni 39 milioni, kutoka Pauni 65 milioni za msimu uliopita ikiwa ni anguko la asilimia 40. Pauni 26 milioni zimeondoka.

Romelu Lukaku

Lukaku maisha ya soka lake yalitibuka kwenye majira ya kiangazi ya mwaka jana baada ya kurudi Chelsea na kushindwa kufanya kweli ndani ya uwanja. Muda wake wa mkopo huko Inter Milan alikocheza kwa msimu uliopita, ulikuwa wa kurekebisha mambo yake ya ndani ya uwanja na hakika mambo hayakwenda kama alivyohitaji.

Na sasa thamani ya straika huyo wa kimataifa wa Ubelgiji imeshuka hadi Pauni 34 milioni kutoka Pauni 60 milioni ikiwa ni anguko la asilimia 43. Hiyo ina maana Pauni 26 milioni zimeondoka kwenye thamani ya Lukaku.

Youri Tielemans

Tielemans alikamilisha uhamisho wake wa bure akitua Aston Villa kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi huko Ulaya. Staa huyo ametokea kwenye timu iliyoshuka daraja ya Leicester City na jambo hilo lilifanya thamani yake huko sokoni kushuka.

Kinachoelezwa ni kwamba thamani ya mchezaji huyo sokoni ilishuka kwa asilimia 35, kutoka Pauni 47.5 milioni hadi Pauni 21.5 milioni. Hiyo ina maana, Tielemans kwenye thamani yake imeondoka Pauni 26 milioni.

Mohamed Salah

Hakuwa kwenye kiwango bora sana cha soka lake kwa msimu wa 2022-23. Hata hivyo, supastaa Mohamed Salah alifanikiwa kufunga mabao 19 na kuasisti mara 12 katika mechi 38 alicheza kwenye Ligi Kuu England. Si takwimu mbaya sana, lakini kwa mchezaji wa aina yake, matarajio yalikuwa makubwa zaidi.

Lakini, kutokana na umri wake kuwa na miaka 31, hilo linashusha thamani yake sokoni. Kwa mujibu wa Transfermarkt, thamani ya sasa ya Mo Salah ni Pauni 36 milioni ikiwa imeshuka kutoka Pauni 64.5 milioni aliyokuwa nayo majira ya kiangazi mwaka jana.

Son Heung-min

Son alikuwa na msimu wa hovyo kwa mara ya kwanza tangu alipoanza kuitumikia Tottenham Hotspur - licha ya kwamba alitokea kushinda Kiatu cha Dhahabu kwenye msimu wa 2021-22. Kwa msimu uliopita alifunga mabao 10 na kuasisti sita, huku umri wake ukifikia miaka 30 hilo kwa namna moja au nyingine linashusha thamani yake hukjo sokoni.

Thamani ya sasa ya supastaa huyo wa Korea Kusini ni Pauni 43 milioni ikishuka kutoka Pauni 64.5 milioni ikiwa ni anguko la asilimia 33. Hiyo ina maana Pauni 21.5 zimeondoka kwenye thamani yake.

Andrew Robertson

Robertson amejipambanua na kuwa mmoja wa mabeki wa kushoto mahiri kabisa duniani kutokana na kile anachokifanya chini ya kocha Jurgen Klopp huko kwenye kikosi cha Liverpool. Hata hivyo, safu ya ulinzi ya Liverpool ilikuwa kwenye majanga makubwa msimu uliopita na jambo hilo limemfanya Robertson thamani yake kushuka kwa asilimia 39 kutoka Pauni 49 milioni hadi Pauni 34 milioni, ikiwa ni anguko la Pauni 15 milioni kwa mujibu wa TransferMarkt. Robertson ni moja ya washambuliaji matata kabisa kwenye Ligi Kuu England.

Federico Chiesa

Chiesa amekuwa akisumbuliwa sana na majeruhi mfululizo tangu alipong'ara akiwa na Italia kwenye Euro 2020.

Juventus ilithibitisha alilazimika kwenda kukutana na maalamu wa maumivu ya goti Machi mwaka huu na tangu wakati huo amekuwa akipambana kuweka sawa hali yake ya kiafya.

Thamani ya sasa ya supastaa huyo Mtaliano ni Pauni 34 milioni kutoka Pauni 55.5 milioni, hilo likiwa ni anguko la asilimia 39. Hiyo ina maana, Chiesa kwenye thamani yake imepotea Pauni 21.5 milioni.

Chanzo: Mwanaspoti