Kuna muda wachezaji huwa wanapitia nyakati ngumu na hiyo husababisha timu zao kuwatoa kwa mkopo ama kuwauza mazima.
Wakati mwingine pale wanapokuwa wanatolewa kwa mkopo hukutana na timu zao na kuziadhibu vya kutosha na muda mwingine hupotea kabisa.
Joao Cancelo ni miongoni mwa mastaa ambao walitolewa kwa mkopo na Man City katika dirisha lililopita la majira ya baridi na mapema wiki hii alikutana na waajiri wake hao ingawa hakuonyesha kiwango bora kutokana na muda mfupi aliopewa kucheza.
Leo tutawatazama wachezaji watano ambao wamekutana na timu zao kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa baada ya kutolewa kwa mkopo.
5. Thibaut Courtois
Kipa huyu wa kimataifa wa Ubelgiji, alicheza Atletico Madrid kwa mkopo kwa misimu mitatu kabla hajaarudi Chelsea nakuwa mmoja ya makipa tegemeo.
Katika kipindi hicho cha misimu mitatu Atletico na Chelsea zilikutana kwenye Ligi ya Mabingwa lakini hapo awali ilikuwa ngumu kucheza kwa sababu kwenye mkataba wake kulikuwa na kipengele kilichowataka Atletico kulipa Pauni 2.5 milioni kwa kila mechi atakayocheza dhidi yao.
Lakini Atletico ililalamika na kudai kwamba isingeweza kulipa kiasi hicho na ikashtaki, kisha mamlaka zikawaruhusu kumtumia na staa huyo akaichezea Atletico kwenye mechi zote mbili kisha Chelsea ikatolewa huku yeye akionyesha kiwango bora sana.
4. Philippe Coutinho
Baada ya kusajiliwa na Barcelona mambo yalionekana kuwa magumu kwake, hivyo akatolewa kwa mkopo kwenda Bayern Munich kwa ajili ya kupunguza gharama za matumizi.
Hata hivyo, balaa liliwarudia Barcelona wenyewe baada ya kukutana na Munich kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa.
Coutinho alifunga mabao mawili na kutoa asisti moja kwenye ushindi wa jumla wa mabao 8-2 walioupata Munich dhidi ya Barca msimu wa 2019-20.
3. Fernando Morientes
Morientes alikuwa na wakati mzuri sana akiwa na Real Madrid ambapo alifanikiwa kushinda mataji matatu ya Ligi ya Mabingwa kwenye misimu sita aliyodumu na matajiri hao.
Hata hivyo msimu wa 2003-04 alitolewa kwa mkopo kwenda Monaco na akakutana na miamba hiyo kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa.
Morientes alifunga katika mechi zote mbili za hatua ya robo fainali na kuchangia Madrid kutolewa kwa faida ya bao la ugenini.
2. Kingsley Coman
Jamaa ana historia nzuri dhidi ya waajiri wake wa zamani ama waliomtoa kwa mkopo pale anapokutana nao.
Mwaka 2016, Coman alikuwa akiichezea Bayern Munich kwa mkopo na wakakutana na Juventus kwenye hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa.
Licha ya kwamba alikuwa na wakati mgumu kwenye kikosi cha Juve alipokuwa Serie A, alifanikiwa kufunga bao moja na kutoa asisti kwa Thomas Muller.
Miaka minne baadae wakati ameshasaini mkataba wa kudumu wa kuitumikia Munich akakutana na waajiri wake wa zamani wa PSG kwenye mchezo wa fainali ya Ligi ya Mabingwa na akafunga bao pekee na la ushindi kwenye mechi hiyo.
1. Joao Cancelo
Fundi huyu alifanikiwa kucheza dakika kwenye mchezo wa Jumanne iliyopita kati ya waajiri wake Manchester City akiwa na Bayern Munich ambayo anaichezea kwa mkopo akijiunga nayo january mwaka huu.
Tofauti na wachezaji wengine kwenye orodha hii, Cancelo hakufanya makubwa sana mbele ya Man City na mwisho Munich ikaambulia kichapo cha mabao 3-0.