Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mastaa hawa walikimbia kwao kisa vita

Alphonso Davies Bn Alphonso Davies

Thu, 26 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Asikuambie mtu, vita ni mbaya. Israel na Palestina kwa sasa hapakaliki. Maelfu wanakimbia kujiokoa na vita. Urusi na Ukraine nako hapajapoa. Sio salama.

Hapa Afrika stori ni kama unavyosikia huko Sudan. Hali ni mbaya. Watu ni kukimbia tu kutoroka nchi zao. Wakimbizi. Wanaenda kusaka amani kwengine.

Vita vinakatisha tamaa ya maisha, lakini wapo waliokumbwa na misukosuko kama hiyo na wakatoboa kwenye maisha yao.

Wanasoka pia wapo waliokumbwa na kadhia hiyo na kusababisha wakimbie nchi zao na kukulia nchi nyingine kabla ya kuingia kwenye soka.

Hawa hapa wanasoka watano ambao walikuwa wakimbizi baada ya nchi zao kukumbwa na machafuko ya vita kabla ya kuwa mastaa wakubwa.

ALPHONSO DAVIES

Wazazi wa Alphonso Davies walikimbia kutoka Liberia hadi Ghana walikokuwa wakiishia kwenye kambi ya wakimbizi, chanzo kikubwa kikiwa ni vita nchini humo.

Davies akazaliwa kwenye kambi ya wakimbizi huko Ghana na alipofikisha umri wa miaka mitano familia yake ikazamia Canada.

Akiwa nchini humo staa huyu ndio alianza kucheza mpira na ilipofika Juni, 2017 wiki moja baada ya kupewa uraia wa Canada akaweka rekodi ya kuwa mchezaji kijana zaidi kuwahi kuichezea timu ya taifa ya Canada akiwa na umri wa miaka 16.

Kwa sasa ndiye mchezaji pekee raia wa Canada ambaye ni balozi wa umoja wa mataifa kitengo cha wakimbizi na pesa zote za posho anazopata kwenye timu ya taifa huchangia kwa ajili ya wakimbizi.

LUKA MODRIC

Alizaliwa Croatia mwaka 1985, wakati ambao nchi hiyo ilikuwa ikipambana kupata uhuru wake. Alikuwa akiishi kwenye kijiji cha Modrici na familia yake pamoja na babu yake. Wakati vita ilipochanganya waasi wa Serbia walimuua babu yake na kusababisha Modric na watu wengine waliobakia kukimbia nyumba waliyokuwa wakiishi na ilichomwa moto.

Modric alitumia miaka mingi kuishi kwenye hotel zilizokuwa zinafadhili wakimbizi katika mji wa Zadar. Akiwa kwenye mji huo ndio kipaji chake kikaonekana wakati alipokuwa akicheza soka mitaani.

Tangu hapo kiungo huyu wa Madrid amekuwa mmoja kati ya wachezaji bora duniani na ameshawahi kushinda tuzo mbalimbali kama mchezaji bora wa FIFA wa mwaka na Ballon d’Or.

AWER MABIL

Mabil alizaliwa kwenye kambi ya wakimbizi Kenya mwaka 1995 na wazazi wake waliokuwa wakimbizi kutoka Sudan Kusini kutokana na vita.

Mabil alilelewa kwenye kambi ya wakimbizi na alianza kucheza soka pia hadi mwaka 2006 na familia yake ilihamia Australia.

Baada ya kufika huko kipaji chake kilionekana na akasajiliwa na Adelaide United, kisha akaanza kucheza timu ya taifa mwaka 2018.

Mabil ndio alikuwa mfungaji wa bao la ushindi lililoipeleka Australia kwenye mashindano ya Kombe la Dunia mwaka jana, Qatar.

Alipoulizwa kuhusu bao, alisema hiyo ndio njia pekee ya kuishukuru Australia kwa niaba ya familia yake kwa jinsi walivyowapokea na kukubali kuwapa hifadhi.

EDUARDO CAMAVINGA

Alizaliwa kwenye kambi ya wakimbizi huko Cabinda, Angola, mwaka 2002. Wazazi wake ambao kiasili wametokea Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, walizamia Ufaransa akiwa na umri wa miaka miwili.

Akiwa huko wakati anacheza kwenye michuano ya majira ya kiangazi ‘summer football camps’ ambayo ni maalumu kwa ajili ya kutafuta vipaji. Maskauti wakamwona na wakampa shavu.

Baada ya hapo akiwa na umri wa miaka 17, akaweka rekodi ya kuwa mchezaji mdogo zaidi kuwahi kuifungia bao timu ya taifa ya Ufaransa.

VICTOR MOSES

Mzaliwa wa maeneo ya Kaduna, Nigeria, Moses akiwa na umri wa miaka 11 wazazi wake waliuliwa kutokana na machafuko ya kidini yaliyotokea mwaka 2002.

Wakati wazazi wake wanafariki dunia Moses alikuwa na marafiki zake anacheza mpira hivyo alipopata taarifa hiyo alijificha hakurudi tena nyumbani kwao hadi alipopata nafasi ya kukimbilia Uingereza ambako alipewa hifadhi na moja ya familia huko Kusini mwa London.

Alionyesha kipaji cha soka hivyo akaanza kucheza soka la kulipwa akiwa na Crystal Palace F.C, Chelsea ambayo aliisaidia kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu England mwaka 2017 chini ya Antonio Conte. Alichagua kucheza timu ya taifa ya Nigeria.

Chanzo: Mwanaspoti