Henock Inonga na Clatous Chama ndio majina ambayo yatajwa huko Morocco ambako Wekundu wa Msimbazi, Simba watatua muda wowote kwa ajili ya kumaliza kibarua cha hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Raja Casablanca.
Kwa mujibu wa mchezaji kinda wa Kitanzania, Adrian Kitare, ambaye yupo Casablanca akiwa na timu za vijana za kikosi hicho, alisema kufanya vizuri kwa wachezaji hao kwenye hatua zilizopita kiasi cha kuingia kwenye vikosi bora vya wiki kumefanya majina yao kutajwa zaidi nchini humo na mashabiki hadi wachezaji wa timu hiyo kubwa barani Afrika.
Katika kipindi hiki cha mapumziko ya wiki ya kimataifa, Adrian ambaye alipata nafasi kufanya mazoezi na wachezaji wa kikosi cha kwanza, alisema pamoja na ukubwa wa Raja, lakini kuna hofu kubwa pia kwenye kikosi chao kuhusu baadhi ya mastaa wa Simba: “Kwenye kile kikosi bora cha wiki ya tatu ya Ligi ya Mabingwa, Raja tulitoa mchezaji mmoja ambaye ni Jamal ni beki wa kati, alipangwa na Inonga na kuhusu Chama waliona alifunga bao bora la wiki, wao nao wanafuatilia kile kinachoendelea kwenye mashindano na wamekuwa wakiwazungumzia sana hapa.”
“Ilikuwa rahisi kwao kujua habari za Chama na Inonga kwa sababu wanafanya vizuri pamoja na hawakuonyesha makali yao dhidi yao kwenye mchezo wa kwanza Dar es Salaam, ila akilini mwao wanajua ubora wa hao wachezaji, kwa hapa Jamal ni mchezaji mkubwa na amekuwa akitegemewa kwenye timu ni mfano wa kuigwa.”
Kinda huyo alipata nafasi pia ya kuzungumza na Jamal na anasema staa huyo alikuwa akimuuliza mambo mengi kuhusu Simba, huku akionyesha hali ya kuwafahamu kwa undani zaidi: “Huyu ni mchezaji mkubwa hapa, aliniuliza kama kuna baadhi ya vitu navifahamu kuhusu Simba, huyu jamaa ni staa lakini anapenda sana kufahamu wapinzani wake,” alisema.
Bao la mpira wa adhabu la kiungo wa Simba, Chama katika ushindi wa mabao 7-0 dhidi ya Horoya ya Guinea kwenye mchezo wa Kundi C, ndilo lililoteuliwa ëBao Bora la Wikií. Takwimu zinaonyesha nyota huyo wa kimataifa wa Zambia ndiye mchezaji hatari zaidi kwenye kikosi hicho akiwa na mabao manne.
Upande wake Inonga aliingia kwenye kikosi bora cha wiki baada ya kuifungia Simba bao pakee kwenye mchezo wa kwanza dhidi ya Vipers lililoweka hai matumaini ya kikosi hicho kutinga hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kabla ya kurudiana nao.
Kipindi kama hiki cha mapumziko ya kupisha mechi za timu za taifa kocha wa kikosi cha kwanza hutoa nafasi kwa wachezaji wachache wa timu za vijana kwa ajili ya kufanya mazoezi na wakubwa kwa lengo la kupata uzoefu zaidi.
Adrian alisema asilimia kubwa ya mastaa wa Raja Casablanca wapo kwenye maandalizi ya mchezo huo wa kukamilisha ratiba dhidi ya Simba maana wachezaji wao wa ndani hakuna hata mmoja aliyeitwa kwenye kikosi cha Morocco ambacho kilicheza mchezo wa kirafiki na kuifunga Brazil mabao 2-1.
“Ni ngumu sana kwa mchezaji wa ndani Morocco kuitwa timu yao ya taifa kwa sababu wachezaji wao wengi wanafanya vizuri Ulaya,” alisema.
Kwa upande wake Kocha wa Simba, Roberto Oliveira Robertinhoí alisema kwa wachezaji ambao amekuwa nao kwenye kipindi hiki cha wiki ya kimataifa anaendelea nao kwenye programu zake za mazoezi huku akisubiri kikosi chake kukamilika ili kuingia msituni kwa ajili ya kulinda heshima yao dhidi ya Raja, Aprili Mosi.
“Tunaendelea na maandalizi kwa ajili ya mchezo wetu ujao dhidi ya Raja, tunahitaji kulinda heshima yetu, ninafuraha kuona kwa sasa wachezaji wanaelewa mfumo wangu, tutaenda kucheza mpira wetu kwa kushambulia kupitia pembeni na mategemeo ni kufanya vizuri pamoja na kwamba tulipoteza tukiwa nyumbani,” alisema.