Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mastaa hawa panga linawahusu Bara

Skudu Makudubela Vvvv.jpeg Mastaa hawa panga linawahusu Bara

Wed, 13 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Desemba 16 mwaka huu, Dirisha Dogo la Usajili kwa wachezaji wa Ligi Kuu Bara, Championship na First League linafunguliwa rasmi.

Ni wakati ambao vikosi vinapata nafasi ya kusajili na kuuza wachezaji sambamba na kuachana na wale ambao hawana tija kwenye vikosi vyao kutokana na mipango ya kocha husika.

Mwanaspoti limefanya uchunguzi kutoka katika timu tatu za juu kwenye msimamo, kwa maana ya Yanga, Azam na Simba na kugundua kuna mastaa wa kigeni ambao wapo kwenye wino mwekundu wa viongozi wa timu hizo na kama watashindwa kufanya maajabu katika siku chache hizi zilizobaki, basi huenda wakatemwa au kutolewa kwa mkopo.

Kupitia Makala haya, hawa ni wachezaji tisa kutoka timu tatu za juu kwenye msimamo ambao huenda wakavua jezi wanazovaa sasa na kutafuta maisha mengine.

IDRIS MBOMBO-AZAM

Huyu ni mshambuliaji wa Azam raia wa Congo DR aliyetua Azam misimu miwili iliyopita na msimu huu kuongezewa mkataba wa mwaka mmoja utakaotamatika mwaka 2024.

Kwa sasa Mbombo ni majeruhi akiuguza goti na atakaa nje kwa muda usiopungua wiki tatu.

Jambo hilo limeendelea kumpa wakati mgumu straika huyo na tayari benchi la ufundi la Azam na uongozi uko mbioni kuachana naye ili kusajili mastaa wapya wa kigeni akiwemo Djuma Shaban aliyekuwa Yanga msimu uliopita.

Kwa sasa pale Azam katika eneo la Mbombo wanacheza Prince Dube, Allasane Diao na Abdul Seleman ‘Sopu’.

HAFIDH KONKONI- YANGA

Huyu ni straika Mghana aliyesajiliwa na Yanga mwanzoni mwa msimu huu akitokea Bechem United  alikokuwa amefunga jumla ya mabao 15 msimu uliopita na kutabiriwa ndiye Mbadala wa Fiston Mayele aliyeuzwa Pyramids.

Lakini mambo yamekuwa magumu tangu atue Yanga kwani hana nafasi ya uhakika kucheza kikosini na hata pale anapopata nafasi ameshindwa kuonyesha makeke.

Konkoni hadi sasa ana bao moja tu kwenye ligi lakini Mwanaspoti linajua Yanga iko sokoni kutafuta straika mwingine ambaye  ataenda kumwondoa Mghana huyo pale Jangwani.

Nafasi anayocheza Konkoni (mshambuliaji wa kati), kwa Sasa Yanga wanacheza kwa kupokezana Kennedy Musonda na Clement Mzize.

AUBIN KRAMO- SIMBA Kabla ya msimu huu kuanza, Simba ilitua Ivory Coast na kumsainisha mkataba wa miaka miwili winga machachari Aubin Kramo aliyekuwa akikipiga Asec Mimosas ya nchini humo.

Kramo alitua Simba lakini mambo yakawa magumu kwani hajacheza mechi hata moja ya kimashindano kutokana na kuandamwa na majeraha.

Kwa sasa yupo kwao akipatiwa matibabu ya goti lakini huenda barua ya kuachwa na Simba ikamkuta huko huko kwani wakali hao wa Kariakoo wapo mbioni kushusha mapro wapya unyamani dirisha dogo.

Kramo anayecheza eneo la winga zote mbili kwa sasa nafasi hizo ndani ya Simba zinachezwa na Kibu Denis, Clatous Chama na Saidi Ntibanzokiza kwa uhakika zaidi.

ABDULAI IDDRISU- AZAM Azam FC ipo sokoni ikitafuta kipa mpya lakini si hivyo tu imewaweka sokoni makipa wake wawili, Mghana Abdulai Iddrisu na Mcomoro Ali Ahmada.

Licha ya wawili hao kuwa sokoni lakini Iddrisu ndiye huenda akaondoka kikosini hapo dirisha dogo lijalo huku Ahmada akitarajiwa kuondoka mwishoni mwa msimu mkataba wake utakapomalizika.

Nidhamu mbovu na ubora wao wa kawaida ndizo sababu kuu zinazotajwa kuwaondoa makipa hao viunga vya Chamazi na kusaka makipa wengine wapya watakaoendana na matakwa ya timu.

GIFT FRED - YANGA Huyu ni beki wa kati wa Yanga aliyesajiliwa mwanzoni mwa msimu huu akitokea Sports Club Villa ya Uganda kwa mkataba wa miaka miwili.

Villa alikuwa muhimili katika eneo la beki na tegemeo kwenye kikosi cha kwanza, lakini tangu ametua Yanga mambo yamekuwa shaghala bhagala.

Yanga inapanga kumtoa Gift kwa mkopo dirisha dogo litakalofunguliwa Desemba 16, huku nafasi yake ikitarajiwa kuzibwa kwa kusajili kiungo wa kati.

Mabeki wazawa, Dickson Job, Bakari Mwamnyeto na Ibarahim Abdallah ‘Bacca’, ndio wanaocheza eneo la Gift Yanga.

WILLY ONANA- SIMBA Winga huyu Mcameroon yupo Msimbazi na alisajiliwa mwanzoni mwa msimu huu akitokea Rayon Sports ya Rwanda alikokuwa mfungaji bora baada ya kupachika mabao 16 msimu uliopita.

Onana alitua Simba kwa mbwembwe akianza kutupia bao la kideoni kwenye mechi ya tamasha la ‘Simba Day’, dhidi ya Power Dynamos na Wanamsimbazi kumtabiria makubwa kabla mambo hayajamuendea kombo.

Baada ya hapo ameonekana ni mchezaji wa kawaida sana kutokana na kiwango anachokionyesha pale anapopata nafasi.

Hadi sasa ameifungia Simba bao moja tu kwenye ligi na sio mchezaji muhimu kwenye kikosi hicho na huenda akaachwa dirisha dogo lijalo ili kupisha usajili  wa mashine mpya na Simba imepanga kushusha wachezaji wasiopungua wanne.

JAMES AKAMINKO - AZAM Huenda utashtuka kuona jina hili la James Akaminko kwenye hii orodha, lakini usiwaze, ndivyo maisha ya soka yalivyo. Hayatabiriki.

Huyu ni kiungo fundi wa boli kutoka Ghana aliyetua Azam msimu uliopita na kucheza kwa kiwango kikubwa jambo lililozifanya Simba na Yanga kufikiria kumsajili.

Msimu huu mambo hayamwendei vyema ndani ya Azam, inaelezwa hana mahusiano mazuri na wachezaji wenzake sambamba na bechi la ufundi.

Mwanaspoti linajua ni miongoni mwa majina ambayo yapo mezani kwa vigogo wa timu hiyo yakisubiri panga kwenye usajili wa dirisha dogo.

MAHLATSE MAKUDUBELA ‘Skudu’- YANGA Baada ya Yanga kutamba sana kipindi cha usajili ikijinadi kusajili mchezaji hatari atakayevaa jezi namba sita iliyoachwa na Feisal Salum ‘Fei Toto’, aliyeondoka kwa shari na kutua na Azam, Yanga ilimtambulisha Mahlatse Makudubela ‘Skudu’ raia wa Afrika Kusini na kumpa jezi hiyo.

Makudubela akaanza kwa mbwembwe maisha mapya ndani ya Yanga huku akionekana zaidi kufurahisha kwa aina yake ya uchezaji ‘Shibobo’ lakini kwa sasa anatia amebaki kuwa machachari bila hatari.

Skudu sasa hana nafasi ndani ya kikosi cha kwanza cha Yanga chini ya Kocha Miguel Gamondi na kama timu hiyo itapata winga hatari wa kigeni basi mkali huyo wa kucheza muziki aina ya Amapiano atakuwa hatarini kuachwa.

LUIS MIQUISSONE - SIMBA Mashabiki wa Simba wanamuita ‘Konde Boy’, Kijana mwenye kimo kifupi na machachari kutoka Msumbiji ambaye alikonga mioyo yao msimu wa 2020/2021 kwa kiwango  bora kabla ya kusajiliwa na vigogo wa soka la Afrika, Al Ahly ya Misri.

Akiwa Ahly, Luis alishindwa kuonyesha makali yake na kuishia kukaa benchi kabla ya kutolewa kwa Mkopo kwenye klabu ya Abha ya Saudia ambako pia alishindwa kuwika kutokana na majeraha.

Simba ikaona sio kesi, ikamrejesha kundini msimu huu na kuwa usajili uliowafurahisha mashabiki wengi wa timu hiyo lakini kwa sasa unawashangaza.

Luis licha ya kuwa na asisti tatu kwenye ligi, si mchezaji tegemeo ndani ya Simba na amekuwa na kasi ya kawaida jambo linalowafanya vigogo wa chama hilo kufikiria kumnyofoa katika dirisha dogo na kusajili mbadala wake.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live