Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mastaa hawa kila mtu na njia yake

Mastaa Hawaaaaa Mastaa hawa kila mtu na njia yake

Wed, 11 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kuna usemi usemao ukiona cha nini wenzako wanawaza watakipata lini. Hiyo ndiyo hali halisi kwa baadhi ya mastaa ambao Simba na Yanga ziliwatema msimu uliopita huku Singida Big Stars ikiwasajili.

Vigogo hao wa soka kumtema mchezaji haijalishi kama ni kiwango chake kushuka au la, lakini wanaweza kumuacha kwa kumchoka kutokana na kuwa naye kwa muda mrefu.

Mwanaspoti linakuletea mastaa ambao timu hizo ziliwaacha wakatimkia Singida Big Stars na huko ugenini kila mmoja amejitengenezea mwelekeo wake, kwani wapo amba wana nafasi ya kuanza kikosi cha kwanza na wengine wanasugua benchini.

GADIEL MICHAEL

Beki huyu alitua Simba kwa mbwembwe kubwa akitokea Yanga 2019 wakati huo akiwa na uhakika wa kucheza beki wa kushoto kutoka na mahitaji ya kikosi hicho tofauti na sasa.

Kutokana na upepo mzuri ambao Simba walikuwa nao wakati huo hakuna mchezaji ambaye hakutamani kukipiga Msimbazi kwa kuwa mafanikio yalionekana ndani na hata nje.

Gadiel hakuangalia ushindani wa namba uliokuwepo Simba kwa Mohamed Hussen ‘Tshabalala’, akaona ni vyema akatimiza lengo la kwenda kukipiga Msimbazi.

Msimu uliopita baada ya kumalizika kwa mkataba wake uongozi wa Simba ulitangaza kumuacha na sasa ndiye nahodha wa Singida Big Stars ambako ni panga pangua anaanza kikosini.

Licha unahodha tu, jicho la Mwanaspoti limeangaza katika michezo tofauti ambayo amecheza na kiwango chake kilivyokuwa bora kwani jamaa anaupiga mwingi na kuwashangaza wengi kutokana na namna ambavyo anasakata kabumbu akiaminiwa na kocha wake.

BENO KAKOLANYA

Miaka minne ndani ya Simba japokuwa hakuwa anapata nafasi mara kwa mara chini ya kipa namba moja Aishi Manula ambaye ameliteka lango Msimbazi, lakini baadhi ya wadau wa soka walimtaka kuondoka kwenda kuendeleza kipaji chake na yeye aliziba pamba masikioni kwa kuwa alifahamu kwenda kwake Simba sio kuwa kipa namba moja, bali ni kumsaidia aliyepo.

Baada ya Simba kumuona wa nini na kushindwa kumuongezea mkataba alipotaka kumlipa kiasi cha pesa flani (hakutaka kukiweka wazi) na uongozi kukataa akaona isiwe tabu akatimka zake na huko aliko ameaminiwa vizuri kusimama langoni.

Beno anasema kitendo cha kuaminiwa na Singida kumempa furaha na kujiona mpya hivyo atapambana kuhakikisha anafanya vizuri na kuiweka timu yake salama.

JOASH ONYANGO

Ubora wake hauwezi kuamini kama ndiye huyo Simba walimuacha bila kugeuza kisogo, ingawa huko aliko namba yake kikosini imekuwa ya kubadilishana na wakali wengine.

Katika mafanikio aliyoyapata Simba misimu minne mfululizo yalichagiwa na ubora wake katika safu ya ulinzi.

Akaona isiwe tabu kuondoka nchini msimu huu kauanza akiwa na walima alizeti hao.

Onyango ubora wake wengi haikutarajiwa kama Simba ingemruhusu kuondoka kwa mkopo. Lakini wakati mashabiki wa Simba wanawaza kwanini alitemwa, aliko pia mambo yake sio mazuri sana. Lililo wazi ni kwamba aliondoka Simba na kuacha alama kiasi cha kupewa jina la utani ‘Nusu Chuma, Nusu Mtu’, lakini upepo bado haujaenda vizuri kwake baada ya kukosekana katika michezo dhidi ya Simba, Mtibwa, Azam tangu alipoumia katika mchezo na Tabora United.

DICKSON AMBUNDO

Winga huyu alitua Yanga 2021 akibahatika kupata nafasi mara chache ndani ya kikosi hicho akitokea Dodoma Jiji

Kwa ubora alionao unaweza kushangaa mchezaji kama huyu kutemwa Yanga, lakini Ambundo anasema maisha lazima yaendelee kwa kuwa mpira ndio kazi aliyoichagua na kutoka sehemu moja sio kushindwa kucheza, ila ni suala la mifumo ambayo kuna muda inaweza kumtoa mchezaji katika timu husika.

Anasema alitua Singida kufanya kazi awezavyo ili timu iliyomuamini iweze kupata mafanikio ambayo imejipangia msimu huu.

HABIBU KYOMBO

Straika huyu aliyesajiliwa na Simba msimu uliopita kutua kwake hakukuwakosha sana mashabiki Msimbazi miongoni mwao waliujia juu uongozi siku tu alipotangazwa kabla ya ligi kuanza.

Manung’uniko yao yalikuwa na kitu kwani hakupata nafasi mara kwa mara katika kikosi cha kwanza cha Simba.

Baada ya msimu kumalizika Simba ilitumia ‘fagio la chuma’ kuwafagia mastaa wengi ilioona haitawatumia msimu huu na yeye akiwemo. Mbali na wenzake waliopewa mkono wa kwaheri yeye peke ndiye hajaanza katika michezo mitatu Singida Big Stars akipata nafasi ya kukaa benchi mchezo dhidi ya Azam wa kusaka mshindi wa tatu katika Ngao ya Jamii mjini Tanga.

Akiwazungumzia mastaa hao, kocha ambaye pia ni mchezaji wa zamani Kenny Mwaisabula anasema wote ambao waliachwa na timu hizo sio wabovu, bali namba vikosini zimewakosesha kuonyesha uwezo wao.

Anasema Kakolanya alivyokaa benchi kiwango chake kilipotelea hapo wakati angekuwa timu nyingine tegemeo kama alivyokuwa Yanga kabla ya kutimkia Simba angekuwa tegemeo.

“Hata Gadiel ni mchezaji mzuri sana lakini pale (Simba) ilikuwa ngumu kuingia mgeni na kupata nafasi ya kuanza, hivyo mchezaji akiamua kukubaliana na hali timu nyingine anapata nafasi.”

Chanzo: Mwanaspoti