Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mastaa hawa kazini kwao kuna kazi

Metacha Diarra Mshery Mastaa hawa kazini kwao kuna kazi

Wed, 1 Nov 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kuna wachezaji kutoka Simba, Yanga na Azam FC ambao bado hawajaonja mechi za Ligi Kuu Bara na washindani wao wa namba wanafanya vizuri, hivyo ni ishara kwao kujiweka sawa ili uwepo wao uwe muhimu kwenye timu. Kibwana Shomary wa Yanga baada ya kusajiliwa beki Yao Kouassi alisema: “Kazini kwangu kuna kazi” akiwa na maana kuwa ni ngumu kupata nafasi kwa urahisi kama ilivyokuwa mwanzo kwenye kikosi hicho.

Yanga imecheza mechi saba ikiwa na pointi 18 sawa na Simba ambayo imecheza mechi sita, lakini ipo nyuma kwa mabao ya kufunga na kufungwa, ilhali Azam FC ina mechi saba na pointi 13, hivyo mastaa ambao hawajapata nafasi ya kucheza wakipambana wanaweza kufanya jambo.

Mwanaspoti linakuletea mastaa ambao walikuwa wanapewa nafasi kubwa ya kuwika msimu huu, lakini hawajacheza na endapo wakikaza buti wanaweza kupindua meza ili kupata namba vikosini.

David Kameta ‘Duchu’ (Simba)

Tangu arejee Simba akitokea Mtibwa Sugar, bado hajaanza kupata nafasi ya kucheza, ambapo panga pangua katika nafasi yake kuna Shomari Kapombe ambaye ukomavu na uzoefu wake ni msaada kwa timu hiyo. Duchu wakati anasajiliwa kila mmoja aliamini anakwenda kuchukua nafasi kwa Kapombe lakini mambo yamekuwa magumu, ila kulingana na umri wa Duchu akiendelea kupambana anaweza akawa tegemeo kwa timu baadaye.

Alicheza kwa mkopo Mtibwa na baada ya kupandisha kiwango alirejeshwa tena Simba, hivyo anatakiwa kujituma zaidi kama anataka kupata nafasi kwenye timu hiyo.

Nassor Kapama (Simba)

Tangu msimu uliopita aliotua akitokea Kagera Sugar, hakuwa na nafasi kikosi cha kwanza na katika mechi sita ambazo zimechezwa hadi sasa hajacheza.

Awali mashabiki waliamini alitakiwa kuachwa dirisha kubwa, lakini zali lilimwangukia akabaki, ikiaminika atacheza, lakini mambo yamekuwa magumu pamoja na kwamba anatajwa anaweza kucheza nafasi mbalimbali uwanjani isipokuwa golini.

Abdallah Hamis (Simba)

Simba ilimsajili dirisha lililopita Abdallah Hamis aliyekuwa anachezea Orapa United ya Botswana, lakini bado hajaanza kupata nafasi ya kucheza ingawa kuna kipindi alikuwa anaitwa timu ya Taifa ‘Taifa Stars’. Kuna wakati anacheza kama kiungo mkabaji nafasi ambayo kuna Mzamiru Yassin na Sadio Kanoute, ilhali Fabrice Ngoma akicheza kama kiungo mshambuliaji na pia kuna Clatous Chama na Said Ntibazonkiza ‘Saido’ walio kumfunika. Jambo pekee analotakiwa kulifanya ni kuhakikisha kuwa anaendelea kupiga kazi kubwa mazoezini ili awe na uhakika wa kupata namba.

Hussein Abel (Simba)

Simba ilimsajili kipa Hussein Abel kutoka KMC, lakini katika mechi sita hakuna aliyokaa golini, na katika nafasi hiyo anashindana na Ayoub Lakred na Ally Salum ambao wamekuwa wakipishana mara kwa mara. Wengine ni Ally Ferouz ambaye hajacheza pamoja na Aishi Manula ambaye pia hajaanza kudaka kutokana na kutoka kuuguza upasuaji aliofanyiwa miezi kadhaa iliyopita.

M’hd Mussa (Simba)

Simba ilimsajili mshambuliaji Mohamed Mussa kupitia michuano ya Kombe la Mapinduzi mwaka huu. Aling’ara kwenye mechi moja ya msimu uliopita dhidi ya Coastal Union ya Tanga ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC), lakini tangu hapo hana nafasi kikosini. Siyo suala tu la kutocheza, pia kuna michezo mingine hata benchi hakai.

Ahamada Ali (Azam FC)

Kipa huyu wa Azam FC msimu uliomalizika alipata nafasi ya kudaka mechi nyingi, lakini katika Ligi Kuu Bara inayoendelea timu yake ikiwa imecheza mechi saba hajadaka hata moja. Awali ilielezwa kuwa anaweza kusepa zake dakika za mwisho za msimu uliopita, lakini alijikuta akibaki na mara kwa mara anasugua kwenye benchi.

Aubin Kramo (Simba)

Simba ilimsajili mshambuliaji Aubin Kramo kutoka Asec Mimosas ya Ivory Coast alikofanya vizuri kwenye Kombe la Shirikisho la Afrika msimu uliopita akimaliza na mabao sita nyuma ya Fiston Mayele aliyekuwa Yanga akiwa kinara na mabao saba. Lakini tangu ametua nchini wimbo ni majeraha ya mara kwa mara na bado hajaonekana kwenye uzi wa timu hiyo katika Ligi Kuu Bara.

Crispin Ngushi (Yanga)

Kati ya wachezaji walioponea chupuchupu kuondoka Yanga nwanzoni mwa msimu ni mshambuliaji Crispin Ngushi, kwani msimu uliopita hakuwa na nafasi kikosini, lakini mechi ya Siku ya Mwananchi dhidi ya Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini, timu yake ikishinda bao 1-0, alicheza kwa kiwango cha juu kilichowapa mashabiki imani ya kumuona akifanya makubwa, ila hadi sasa hajaonja mechi ya Ligi Kuu. Yanga licha ya kutokuwa na straika tegemeo kama alivyokuwa Mayele msimu uliopita, bado imekuwa changamoto kwake kuingia kikosini, kutokana na ubora wa mawinga ambao kocha anawapa nafasi na wanafunga Aziz Ki (mabao sita) na Maxi (mabao matano).

Abuutwalib Mshery (Yanga)

Katika nafasi ya makipa, aliyecheza dakika nyingi Yanga (540) ni Djigui Diarra na Metacha Mnata akicheza 90 dhidi ya KMC pale Yanga iliposhinda mabao 5-0 Uwanja wa Azam Complex, hivyo Mshery hajacheza dakika hata moja msimu huu na hii ni kutokana na kuoka katika majeraha. Kabla ya kutu Metacha Mshery alikuwa anatajwa kuwa kipa namba mbili, lakini sasa mambo yameonekana kuwa magumu kwake tangu alipopata majeraha, labda kwa sasa akiaminiwa maana Metacha na benchi la ufundi kuna namna wanavutana kwa sasa.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: