Huenda Manchester United ikawakosa mastaa wake kadhaa kuelekea mechi ya Ligi Kuu England dhidi ya Liverpool itakayopigwa Jumapili katika Uwanja wa Anfield, sehemu ambayo ilipokea kichapo cha mabao 7-0 msimu uliopita.
Mbali na orodha iliyokuwa ikijulikana awali, Harry Maguire na Luke Shaw wameongezeka katika orodha ya wachezaji majeruhi baada ya kuumia kwenye mechi ya Ligi Mabingwa Ulaya dhidi ya Bayern Munich, Jumanne usiku.
Erik ten Hag anaumiza kichwa kuelekea mechi hiyo kwani kuna uwezekano kati ya mastaa 13 wakakosa mchezo huo mkali unaosubiriwa kwa hamu na mashabiki.
Victor Lindelof
Beki huyu alikosa mechi ya Ligi Kuu Englan dhidi ya Bournemouth, ambayo Mashetani Wekundu walichezea kichapo cha kushtukiza cha mabao 3-0. Lindelof alicheza mechi 10 kati ya 16 kwenye ligi na huenda akakosekana dhidi ya Liverpool.
Harry Maguire
Beki huyu amekuwa na mchango mkubwa tangu kiwango chake kilipoimarika. Maguire amecheza mechi zote nane za mwisho za Ligi Kuu England, pia aliibuka mchezaji bora wa mwezi wa Ligi Kuu wa Novemba. Kukosekana kwake Anfield NI pigo kwa Man United kwenye safu ya ulinzi. Beki huyo wa kimataifa England aliumia kwenye mechi ya Ligi Mabingwa Ulaya dhidi ya Bayern Munich ambapo alicheza kwa dakika 40 tu.
Luke Shaw
Beki huyo alikuwa nje kwa takribani miezi mitatu msimu huu. Shaw alicheza mechi nne za Ligi Kuu baada ya kurejea dimbani, na wiki iliyopita alilazimika kutolewa nje katika kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Bayern kutokana na majeraha. Imeelezwa beki huyo atafanyiwa vipimo zaidi.
Lisandro Martinez
Baada ya kuonyesha kiwango bora tangu alipotua akitokea Ajax, beki huyo amecheza mechi sita tu msimu huu kabla ya kuumia miezi kadhaa iliyopita. Licha ya kurejea na kuanza mazoezi beki huyo hatajumuishwa katika kikosi kitachocheza dhidi ya Liverpool utakaochezwa Jumapili.
Tyrell Malacia
Beki huyo hayupo kikosini kwa muda mrefu, aliumia kabla ya msimu mpya kuanza na taarifa ziliripoti huenda akachelewa zaidi kurudi dimbani. Ingawaje madaktari wa Man United wana matumaini anaweza kurejea dimbani baada ya Sikukuu ya mwaka mpya.
Casemiro
Kiungo huyo wa kimataifa wa Brazil yupo nje ya dimba kwa muda wa miezi miwili kutokana na maumivu ya paja. Casemiro aliumia kwenye mechi ya Kombe la Carabao ambapo United ilipokea kichapo cha mabao 3-0 dhidi ya Newcastle.
Kama ilivyo kwa Martinez, kiungo huyo amerejea dimbani lakini itakuwa mapema kumjumuisha kikosini dhidi ya Liverpool, Jumapili.
Christian Eriksen
Kiungo huyo wa kimataifa wa Denmark alikosa mechi nne za mwisho za Ligi Kuu England pamoja na mechi mbili za Ligi Mabingwa Ulaya. Ilitarajiwa kiungo huyo atakuwa nje ya dimba kwa muda wa mwezi mmoja kutokana na matatizo ya goti. Hata hivyo, Eriksen anatarajia kurejea baada ya Sikukuu ya Krimasi.
Mason Mount
Moja ya usajili ghali kipindi cha kiangazi, Mount ameshindwa kufiti kwenye kikosi cha Ten Hag tangu alipotua. Kiungo huyo hajacheza mechi ya ligi tangu Man United iliposhinda 1-0 dhidi ya Luton City mwezi uliopita. Ni miongoni mwa wachezaji waliorejea mazoezi lakini haijafahamika kama atacheza dhidi ya Liverpool.
Marcus Rashford
Mfungaji bora wa Man United msimu uliopita, lakini msimu huu amekuwa na kiwango kibovu, amefunga mabao mawili tu. Aliwekwa benchi kwenye mechi ya kipigo cha mabao 3-0 kutoka kwa Bournemouth, alikosa mechi dhido ya Bayern kwa sababu kuumwa. Hata hivyo, haifahamiki kama tacheza dhidi ya Liverpool.
Anthony Martial
Mfaransa huyo aliachwa katika kikosi mechi kadhaa zilizopita kabla ya kurejea dhidi ya Bournemouth wikiendi iliyopita. Kama Rashford, aliumwa na alikosa mechi dhidi ya Bayern.
Bruno Fernandes
Kiungo huyo atakosa mechi dhidi ya Liverpool kutokana na kufikisha kadi tano za njano kwenye ligi. Nahodha huyo alilimwa kadi ya njao kdhidi ya Bournemouth wikiendi iliyopita na kuipa pigo timu yake kulekea mechi yao Anfield.