Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mastaa Yanga wapewa tahadhari

Kalala Mayele Fiston Yanga wameanza Ligi kwa Ushindi kila mchezo katika mech zao tano walizocheza

Thu, 4 Nov 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mashabiki wa Yanga wamedhamiria kufanya kweli msimu huu, hivyo kutoa tahadhari kwenye kikosi chao kutobweteka na ushindi wanaoendelea kuupata.

Wapenzi wa Yanga kwa sasa wanaridhika kuingia viwanjani, kukaa mbele ya televisheni zao na kuitazama Yanga inapocheza mechi zake.

Hayo yamesemwa na wanachama wa tawi la Yanga Tamla lililopo eneo la Foma - Temeke ambao wanataka kuhakikisha msimu huu wanatwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara ambao wamekuwa wakiuota kwa miaka minne.

Katibu msaidizi wa tawi hilo, Said Nachenda amesema kuwa ushindi wanaopata unawapa matumaini makubwa ya kufanya vizuri msimu huu ingawa wachezaji wanapaswa kutambua kuwa bado safari ni ndefu.

“Ligi ni mbio ndefu tumeona kabisa safari hii tuna timu ya ushindani lakini tusilewe sifa mapema kwa sababu hata msimu uliopita tulianza hivi hivi, hivyo tuendelee kuwa makini,” amesema.

Kauli ya katibu huyo iliungwa mkono na mwenyekiti wa tawi, Abdallah Maulid ‘Skwashi’ aliyesema kuwa kitu ambacho timu yao inabidi kukifanyia kazi ni kufunga mabao mengi kwa kuwa wapo wachezaji wengi wenye uwezo mkubwa wa kufunga.

“Tunapata ushindi lakini bado naona hautoshi kwa sababu tunapopata timu ya kufunga mabao mengi tufanye hivyo kwa kuwa itafikia muda tunaweza tukalingana na wapinzani wetu alama alafu wakatuzidi mabao jambo ambalo hatutaki litokee,” alisema.

Naye mMtunza fedha wa tawi hilo, Omary Hamis Mtopa alisema kuwa licha ya kiwango kinachoendelea kuonyeshwa na wachezaji wao ila viongozi bado una deni la kutafuta mbadala wa Feisal Salum ‘Fei Toto’.

“Nafasi nyingi tuna wachezaji wengi wenye uwezo, lakini tatizo pekee ninaloliona ni endapo Fei Toto atapata majeraha hali ya kikosi chetu itakuwaje kwa sababu katika nafasi anayocheza sioni mwingine anayeweza kucheza kwa ufanisi mkubwa,” alisema.

Kwa upande wa Ahmed Ally ‘Chamangwana GSM’ ambaye ni mhamasishaji wa tawi hilo, alisema licha ya kazi nzuri inayofanywa na benchi la ufundi ila wasiridhike na upatikanaji wa bao moja.

“Wachezaji wetu wanapopata nafasi wazitumie ipasavyo ili kutuepushia sisi mashabiki presha kwa sababu msimu huu hatutaki masihara kabisa na suala la kukosa ubingwa,” amesema.

Tawi hili linaloitwa Yanga Tamla lilianzishwa mwaka 2020 lina wanachama 131 na safu ya viongozi inaongozwa na mwenyekiti Abdallah Maulid, msaidizi wake Juma Ismail, katibu mkuu ni Kondo Longino, msaidizi wake ni Said Nachenda, mtunza fedha Omary Hamisi Mtopa na mhamasishaji ni Ahmed Ally.

Yanga imeshacheza michezo mitano ya Ligi Kuu na kuibuka na ushindi katika michezo yote huku wakitakata kwa soka safi linalooneshwa na wachezaji wao.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live