Wachezaji wa Young Africans wamesema kwa sasa nguvu na akili zao wamezielekeza katika mchezo wa hatua wa awali wa Ligi ya Mabingwa Afrika, huku kikubwa wanataka kuona wanaandika rekodi ya kuifikisha timu hiyo hatua ya makundi.
Hiyo ikiwa ni siku chache tangu Young Africans itoke kufungwa dhidi ya Simba SC katika mchezo wa Fainali ya Ngao ya Jamii uliochezwa Agosti 13, 2023 kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Mwishoni mwa juma lililopita, Young Africans inatarajiwa kucheza mchezo huo wa hatua ya awali dhidi ya ASAS kutoka Djibout kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamanzi, Dar.
Akizungumza jijini Dar es salaam, kiungo wa Young Africans raia wa Uganda, Khalid Aucho, amesema wamesahau matokeo ya Ngao ya Jamii na sasa nguvu zao wanazielekeza katika mchezo wa kimataifa dhidi ya ASAS.
Aucho amesema katika mchezo huo, wataingia uwanjani kucheza kwa lengo moja pekee ambalo ni kupata ushindi utakaowarejeshea matumaini mashabiki ya kufanya vizuri kimataifa baada ya kuipoteza Ngao ya Jamii.
“Tunafahamu mashabiki wamechukizwa na matokeo mabaya tuliyoyapata katika mchezo wa Ngao ya Jamii, hivyo basi wanatakiwa kusahau na badala yake kuhamishia nguvu katika mashindano mengine msimu huu kwa kuanza dhidi ya ASAS katika mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika.
“Kama wachezaji tumejiandaa na tunaendelea kujiandaa kambini na kocha wetu Gamondi (Miguel) kwa kuboresha sehemu zenye upungufu ili tupate ushindi katika mchezo huo,” amesema Aucho.
Nahodha wa timu hiyo, Bakari Mwamnyeto, alisema: “Lengo kuu la Young Africans msimu huu ni kufuzu hatua ya Makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kila mchezaji analifahamu hilo, hivyo ni lazima tulifanikishe.
“Katika michuano hii, Young Africans tumekuwa na rekodi mbaya kwani hatujafanikiwa kutinga hatua hiyo kwa kwa muda wa miaka 20 iliyopita, hilo si jambo zuri, hivyo tunatarajia kuanzia msimu huu tufanye vizuri.”
Naye mshambuliaji wa timu hiyo, Mzambia, Kennedy Musonda, alisema: “Tunafahamu kipi ambacho wanakitaka viongozi na mashabiki wetu msimu katika mashindano ya kimataifa, hivyo tutahakikisha tunapambana kufanikisha malengo yetu ya kufika hatua ya makundi. Uzuri ni kwamba wachezaji wote tupo katika morali kubwa ya kupata ushindi.”