Mabosi wa Young Africans wanataka kuona msimu huu wanavunja rekodi ya michuano ya kimataifa waliyoipata msimu uliopita, baada ya kukutana na wachezaji na kuwapa ahadi ya kuwaongezea bonasi.
Msimu uliopita, Young Africans iliweka rekodi ya kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya kwanza ambapo walipoteza na kumaliza washindi wa pili wa michuano hiyo.
Kwa msimu huu, timu hiyo ineanza vema Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya awali kwa kuwaondoa ASAS ya Djibouti, huku ikijiandaa kupambana na Al Merrikh katika mchezo wa Mkondo wa Kwanza, wa Mzunguuko wa Pili wa michuano hiyo kuwania kutinga hatua ya makundi.
Akizungumza kwa sharti la kutokutajwa jina lake hadharani, mmoja wa mabosi wa timu hiyo, amesema msimu huu malengo ya kwanza waliyoyaweka ni kucheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Bosi huyo amesema mara kwa mara wamefanya vikao na wachezaji, na kikubwa wamewasisitizia kufikia malengo hayo, huku wakiahidiwa bonasi kubwa zaidi ya msimu uliopita.
“Msimu huu tunataka kuiweka rekodi kubwa zaidi ya msimu uliopita ambayo tuliiweka katika Kombe la Shirikisho Afrika. Katika kuhakikisha tunafikia malengo hayo, tumewaandalia wachezaji wetu bonasi kubwa zaidi ya waliyokuwa wanaipata msimu uliopita kwa lengo la kuwaongezea molari.
“Kwa usajili huu ambao tumeufanya kwa kusajili wachezaji wengi wenye viwango bora na uzoefu wa michuano mikubwa, ninaamini tutafanikisha malengo yetu,” amesema mtoa taarifa huyo.
Rais wa Young Africans, Injinia Hersi Said, amezungumzia hilo kwa kusema: “Msimu huu tuna malengo makubwa ambayo tumejiwekea, kwanza kabisa ni kuhakikisha timu inafuzu hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika.”