Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mastaa Yanga: Mnatuzingua

Mstaa Pic Data Mastaa Yanga: Mnatuzingua

Thu, 15 Apr 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

MASTAA wa zamani waliofanya vizuri na Yanga, wamedai kwamba wachezaji wa timu hiyo wanawazingua na viwango vya wengi wao ni duni wanashangaa hata walisajiliwaje Jangwani.

Wameenda mbali na kudai kwamba wamepata fedheha mitaani kutokana kiwango duni kinachoonyesha na Yanga kila kukicha ikiwemo mechi iliyopita dhidi ya KMC walipoambulia kwa taabu sare ya bao 1-1.

Nyota wa zamani, Zamoyoni Mogella, Ivo Mapunda na Sunday Manara wametamka bila kificho kwamba hali ni mbaya na inakoelekea Yanga ni pabaya.

Mogella ambaye aliichezea Yanga na Simba alisema, aina ya wachezaji wa timu hiyo hawastahili kuichezea klabu kubwa kama hiyo kwani hawajaimarika kama ilivyo watani zao Simba ambao wapo imara kila idara.

“Shida kubwa ya Yanga ni wachezaji yaani Yanga ni timu kubwa na kongwe kuna wachezaji wamesajiliwa bahati mbaya hadhi yao sio ya kucheza timu kubwa kama hiyo, yaani Yanga kubwa kuliko wao,”alisema.

Mogella alisema; “Viongozi waliangalie sana hili la kubadilisha benchi la ufundi ni shida, ukiangalia Juma Mwambusi ni kocha mzuri sana lakini kaikutaje timu, hapo ndipo wanapotakiwa kujiuliza na kufanyia kazi udhaifu huo bila ya hivyo wataumia sana.”

“Kuelekea msimu ujao wajitahidi kuwaondosha nyota ambao hawana hadhi na uwezo wa kucheza Yanga na pia waimarishe benchi la ufundi basi wataweza kushindana bila hivyo wakienda Kimataifa hatua ya kwanza nje,”alisema staa huyo kwa uchungu.

Kwa upande wa Manara alisema, wachezaji wa timu hiyo hawajiamini na hiyo inachangiwa na uwezo wao hivyo matokeo wanayapata kulingana na uwezo wao ni sawa.

Alisema timu ikiingia uwanjani haina ushindani kama ambavyo watani zao wanafanya kitendo kinachowafanya wanayanga wengi wazidi kuumizwa na matokeo hayo.

“Yanga inavyofanya vibaya wanayanga tunaumia sana, wachezaji hakuna muunganiko kabisa, hata mechi ya juzi kila mchezaji anajichezea tu ilimradi kacheza,uwezo wa wachezaji ni mdogo na hiyo inachangiwa na skauti inavyofanya uchaguzi wa wachezaji husika, sasa hivi Yanga ushindani na Simba ni kazi sana Simba iko vizuri mno,”alisisitiza Manara ambaye ana heshima kubwa Yanga.

Ivo Mapunda ambaye pia amekipiga Simba na Yanga, alisema usajili waliofanya ndio unaowagharimu kutokana na aina ya wachezaji waliopo.

“Tuwe wakweli kinachoigharimu Yanga ni ubora wa wachezaji waliopo tena wengine wanazidiwa na hizo timu ndogo ndio maana KMC walionekana kuwa bora kuliko wao.

“Ili Yanga ifanye vizuri isiogope kabisa kujifunza mazuri ya Simba wanayoyafanya ambapo inazidi kufanya vizuri ni stresi pia kwa Yanga hivyo asikubali kuacha kutumia mbinu alizotumia Simba mpaka sasa wanafanya vizuri.

“Yanga ukiingalia kila idara imepwaya haiwezi kulinganisha na watani zao huu ni wakati wao kuiga mazuri ya Simba na kuboresha kwao hakuna ubaya kuiga kitu kizuri kwa ajili ya maendeleo,” alisema kipa huyo wa zamani wa Gor Mahia ya Kenya.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz