Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mastaa Yanga: Hersi tuletee huyu mwamba

Sowah.jpeg Sowah.

Mon, 11 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Yanga SC imerejea nchini jana ikitokea Ghana kucheza mchezo wa tatu wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Medeama, lakini kuna mastaa wawili wameona kitu kwa mshambuliaji Jonathan Sowah na kushindwa kujizuia kwa kuutaka uongozi wa Yanga kufanya kila linalowezekana kumshusha nyota huyo.

Mastaa hao ni washambuliaji wawili wa zamani wa Yanga, Abeid Mziba ‘Tekero’ na Sekilojo Chambua waliowahi kufanya vizuri na timu hiyo ambao wote kwa pamoja wamepaza sauti wakimtaka Rais wa klabu hiyo Injinia Hersi Said kufanya kila linalowezekana kumsajili haraka mshambuliaji huyo ili kuwapunguzia stresi.

Sowah alicheza katika mechi hiyo ya Kundi D iliyopigwa mjini Kumasi na kufunga bao la penalti liliitia Yanga presha, ila ikapambana na kulirejesha kupitia Pacome Zouzoua, lakini nyota huyo aliisumbua sana ngome ya vijana wa Miguel Gamondi iliyokuwa chini na nahodha Bakar Mwamnyeto, Ibrahim Bacca na Dickson Job.

Wakizungumza na Mwanaspoti kwa nyakati tofauti wakongwe hao walisema Sowah anastahili kutua Jangwani ili kuziba nafasi ya Mayele kwa asilimia zote kwani ni mtu sana.

Mziba, aliyesifika kwa mipira ya vichwa alisema Sowah, licha ya kumuona kwa dakika 90 tu, lakini kwake zinatosha kumuomba Injinia Hersi anayedili na usajili wa Yanga kwa kipindi chote tangu atue klabuni hapo apambane ikiwezekana arudi naye kuja kuongeza kitu kikubwa kwenye kikosi hicho.

Mziba alisema Sowah ni mchezaji mwenye ubora mkubwa wa kujua kuwasumbua mabeki, pia akiwa na ubora mkubwa wa umiliki wa mpira ambapo kama atakuja Yanga kuungana na viungo waliopo sasa atafunga zaidi.

“Mimi nimejiuliza sana baada ya mechi ya jana (majuzi), hivi wakati tunamchukua huyu Hafiz (Konkoni) hatukupata taarifa za huyu Sowah? Yule kama Rais wangu Hersi atamleta pale kwetu haalafu akapewa baraka na wenye klabu pale jangwani basi kutakucha,” alisema Mziba na kuongeza;

“Ubora wa umiliki wake wa mpira alafu akaungana na Yanga yenye viungo bora kama hawa tulionao msimu huu kutakuwa na nguvu kubwa sana tumeiongeza pale mbele atakuwa ni mtu wa maana sana kwa namna alivyo na kasi.”

Kwa upande wa Sekilojo Chambua, kiungo wa zamani wa kimataifa wa timu hiyo na Taifa Stars alisema wakati Yanga ikisaka mshambuliaji basi Sowah ni mtu sahihi kuja kuziba nafasi ya Mkongomani Fiston Mayele pale mbele kwenye safu yao ya ushambuliaji.

Chambua alisema mshambuliaji huyo licha ya Yanga kupanga ukuta wake mgumu lakini bado alikuwa na dakika 90 bora akionyesha uwezo mkubwa wa kupanguia mabeki ambapo endapo atakuja kwenye timu yao utakuwa usajili bora.

“Sisi (Yanga) tunatafuta mshambuliaji yule Sowah ingawa nimemuona kwa dakika tisini tu lakini zinatosha kugundua kuwa ana kitu mguuni kwa namna alivyowapa wakati mgumu mabeki wetu,” alisema Chambua na kuongeza;

“Yanga tunahitaji mtu wa namna ile ilikuwa kuna wakati kama namuona Mayele hivi kwa jinsi alivyokuwa anawatoka mabeki sijali sana bao lake alilofunga kwa njia ya penalti lakini nimeshawishika na ubora wake miguuni na akili.

Tayari mabosi wa Yanga jana walikaririwa wamepanga kuongeza idadi ya wachezaji inayotaka kuwasajili wakiwamo washambuliaji wawili,kiungo na winga teleza mmoja kupitia dirisha dogo na kulazimika kuwataka wachezaji wanne wa kimataifa ili kuimarisha kikosi hicho.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live