Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mastaa Simba waitisha Yanga

Simba Hilal Bn Mastaa Simba waitisha Yanga

Mon, 6 Feb 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kikosi cha Simba jana jioni kilikuwa uwanjani kumalizana na Al Hilal ya Sudan kwa mechi ya kirafiki ya kimataifa, kabla ya kesho kusafiri hadi Guinea kwa mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika, huku mastaa wake wakiitisha Yanga sambamba na kutamba wameipania michuano ya CAF.

Simba inashika nafasi ya pili ya Ligi Kuu nyuma ya Yanga huku ikiwa imefuzu makundi ya Ligi ya Mabingwa ikipangwa Kundi C na AC Horoya ya Guinea, Raja Casablanca ya Morocco na Vipers ya Uganda na itaanzia ugenini nchini Guinea wikiendi ijayo.

Pamoja na akili za mastaa wa timu hiyo na makocha kuwa kwenye michuano hiyo, lakini hawajaiweka kando ligi ikisema wanataka kuuga ndege wawili kwa jiwe moja kwa kufanya kweli nyumbani kurejea taji linaloshikiliwa na Yanga kabla ya kugeukia mechi hizo za CAF kufika mbali.

Rekodi za Simba kwa misimu minne iliyopita inaelezwa zimemdatisha kocha Roberto Oliveira ‘Robertinho’ aliyeapa kuifikisha hadi fainali ya CAF ikiwezekana, lakini akapata mzuka zaidi baada ya mastaa kumuahidi kufanya balaa zaidi ndani na nje ili mambo yawe mswano.

Robertinho aliliambia Mwanaspoti, hakuna kinachoshindikana kwenye soka na kutambia rekodi ya kuifikisha Vipers ya Uganda kwa mara ya kwanza makundi Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.

“Najua malengo ya Simba ni kufika nusu fainali, ila mimi nina njaa zaidi nataka kufika fainali, nafikiria hilo na ninaona linawezekana kwa jinsi wachezaji walivyo na mzuka,” alisema Robertinho anayependelea soka la kasi na pasi.

Mastaa wa timu hiyo kwa nyakati tofauti walisema na kuahidi kuipigania timu wakianza kwenye ligi ili kuzima ubabe wa Yanga, kisha kugeukia kimataifa kuona wanafika mbali na mafanikio waliyokuwa nayo msimu minne iliyopita ya kufika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika.

Staa aliye moto kwenye Ligi Kuu akifunga mabao sita katika mechi tatu za kwanza akiwa na Simba akiasisti mara mbili, Saido Ntibazonkiza alisema anaweka akili mechi za Ligi Kuu ili kurejesha taji, lakini anaichukulia kwa ukubwa michuano ya CAF na yupo tayari kucheza kwa uwezo wake wote ili aache alama.

“Nimecheza michuano tofauti mikubwa duniani lakini hii ni mikubwa kwa Afrika ngazi ya klabu na sijawahi kuicheza kwa kiwango bora. Sasa nipo tayari kupambana na kuhakikisha naacha alama kwa kuifikisha Simba katika malengo kwa msimu huu,” alisema Saido aliyewahi kucheza Ufaransa.

Staa wa zamani wa Zanaco ya Zambia, Moses Phiri anayeongoza kwa mabao ndani ya Simba akifunga 10 alisema ni ndoto ya kila mchezaji kufanya vizuri kwenye michuano ya ndani na ile ya kimataifa naye yupo tayari kulinda heshima ya Simba.

“Simba ni miongoni mwa timu zenye historia ya kipekee miaka ya karibuni kwenye michuano ya CAF na kila mmoja anajua hilo. Tumesajiliwa ili kuhakikisha linaendelea na ikiwezekana tufike mbali zaidi hivyo binafsi nipo fiti kwa mapambano,” alisema.

Mshindi wa Bao Bora la Mwaka kwa michuano ya CAF msimu uliopita, Pape Ousmane Sakho alisema anahitaji kuendeleza alipoishia ili kuendelea kujitengeneza wasifu bora na kuisaidia timu.

“Baada ya kushinda tuzo msimu uliopita watu wengi walinifuatilia na kutaka kujua muendelezo wangu, hilo linanipa shauku kubwa ya kutaka kufanya vizuri msimu huu nikiendeleza nilipoishia,” alisema Sakho, huku kiungo mpya Ismail Sawadogo alisema michuano ya CAF ni sehemu ya kujitangaza zaidi na kuonyesha kila alichonacho.

“Licha ya ligi ya Tanzania kufuatiliwa, lakini michuano ya CAF nadhani inafuatiliwa zaidi, hivyo ukipata nafasi ya kucheza huko kama ilivyo kwetu haupaswi kuichezea zaidi ya kuonyesha kila kitu ulichonacho,” alisema Sawadogo.

Chanzo: Mwanaspoti