Ni rekodi ya kipekee kwa klabu za Tanzania mbili kuingia hatua ya robo fainali ya mashindano makubwa ya ngazi ya klabu chini ya mwavuli wa Shirikisho la Soka Afrika ‘CAF’.
Jasho liliwatoka, damu ilimwagika na nguvu ilitumika kwa wawakilishi wetu Yanga na Simba hadi kufanikiwa kufuzu hatua hiyo huku wakiwa bado na mchezo mmoja mkononi kwa kila mmoja.
Simba ambao wanashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika katika mechi zao tano walizocheza wamefanikiwa kushinda tatu na kupoteza mara mbili hivyo wamekusanya alama tisa wako nafasi ya pili kwenye kundi lao.
Yanga wakiwa wanashiriki Kombe la Shirikisho wao kwenye mechi tano walizocheza wameshinda tatu, sare moja na kupoteza mara moja hivyo wamelamba alama 10 na wako kileleni mwa kundi lao.
Hadi kufikia hapa sio mchezo kwa kuwa kila kundi lilikuwa na klabu ngumu ambazo zilipigana kufa na kupona kusonga mbele lakini Simba na Yanga wakawa kati ya wale waliotoboa.
Hapa Championi tunakuletea baadhi ya mastaa kutoka Yanga na Simba ambao walikiwasha balaa kwenye hatua hii;
MANULA/DIARRA Aishi Manula kipa namba moja wa Simba ni mechi tano hatua ya makundi amecheza na zote alicheza mwanzo mwisho hivyo jumla kayeyusha dakika 450.
Hajafungwa kwenye mechi tatu mfululizo ambazo ni dakika 270 ilikuwa Februari 25, 2022 Vipers 0-1 Simba kisha ule mchezo uliochezwa Uwanja wa Mkapa Machi 7, Simba 1-0 Vipers na Simba 7-0 Horoya.
Kitasa Joash Onyango amekuwa na kazi kubwa kuweka lango salama ambapo Simba ikiwa imetunguliwa mabao manne ni moja wametunguliwa kwa mkwaju wa penalti.
Ni kwenye harakati za kuokoa Onyango kasababisha penalti hizo ilikuwa dhidi ya Horoya ugenini hapa Manula aliokoa ila ile dhidi ya Raja Casbalanca ilizama mazima nyavuni.
Djigui Diarra kipa wa Yanga kwenye Kombe la Shirikisho amekaa langoni mechi tano akisepa na dakika 450, mabao manne kaokota nyavuni kwake ambapo mabao mawili alitunguliwa na US Monastir, bao moja dhidi ya TP Mazembe na moja dhidi ya Real Bamako ana clean sheets tatu.
HENOCK INONGA Beki wa kati anayeshikilia rekodi ya kuwa nyota wa kwanza kufunga katika hatua ya makundi ilikuwa dhidi ya Vipers ugenini.
Beki huyu wa Simba alipachika bao hilo dakika ya 19 ikiwa ni baada ya Simba kucheza mechi mbili mfululizo na wakatunguliwa.
Bakari Mwamnyeto yupo zake ndani ya Yanga akiwa kwenye ni chaguo la kwanza la Nabi katika eneo la ulinzi akiwa shuhuda wa mechi mbili ambazo hawajafungwa na ni nahodha aliyekiongoza kikosi kutinga robo fainali Kombe la Shirikisho.
MOSES PHIRI Kwenye mechi mbili mfululizo Phiri raia wa Zambia katengeneza pasi za mabao ilikuwa dhidi ya Vipers nje ndani ile ya ugenini alimpa Inonga na pale Uwanja wa Mkapa alimpa Clatous Chama.
Kennedy Musonda pia raia wa Zambia yupo ndani ya Yanga akiwa ametengeneza pasi tatu za mabao ilikuwa dhidi ya TP Mazembe, Real Bamako na dhidi ya US Monastir zote Uwanja wa Mkapa na katupia kambani mabao mawili.
CLATOUS CHAMA Kiungo Chama anafanya watu waamini kwamba mpira ni kitu rahisi kutokana na utulivu wake pamoja na aina ya mabao anayotupia. Anataka uteseke kwanza ndipo akufunge.
Kibindoni katupia mabao manne lile la kwanza aliwatungua Vipers dakika ya 45 huku matatu akiwatungua Horoya ilikuwa dakika ya 9,18 na 69 akasepa na mpira wake huku akitoa pasi moja ya bao.
Mechi zote tano Chama kasepa na dakika 90 na kumfanya awe ametumia dakika 450 kahusika kwenye mabao matano kati ya 9 ambayo yamefungwa na Simba hatua ya makundi.
SADIO KANOUTE Mkata umeme Kanoute mzee wa mikato ya kimyakimya ndani ya Simba ametupia kambani mabao mawili ilikuwa dhidi ya Horoya, Uwanja wa Mkapa.
Khalid Aucho yupo zake Yanga kwenye eneo la kiungo amekuwa mtuliza makeke ya wapinzani huku akitembeza mikato kimtindo.
Mzamiru Yassin kwa mastaa wazawa ndani ya kikosi cha Simba eneo la ukabaji hana jambo dogo anakiwasha huku akiwa kwenye orodha ya waliopata kadi mchezo dhidi ya Horoya.
Mudhathir Yahya anakipiga Yanga katika hatua ya Kombe la Shirikisho dhidi ya TP Mazembe alipachika bonge moja ya bao akiwa ni mzawa aliyefunga katika hatua ya makundi.
SHOMARI KAPOMBE Beki wa kulia Kapombe ana pasi moja ya bao kibindoni ilikuwa dhidi ya Horoya na alisababisha penalti moja kwenye mchezo huo. Ushirikiano wake na Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jr’ unaiweka ngome ya Simba salama.
Djuma Shaban kwa Yanga ni mkali wa kumwaga krosi akiwa na pasi moja ya bao alitoa kwenye mchezo dhidi ya TP Mazembe, Uwanja wa Mkapa.
JEAN BALEKE Mshambuliaji wa kwanza wa Simba kufunga hatua ya makundi ilikuwa dhidi ya Horoya alipotupia kambani mabao mawili dakika ya 32 na 65.
Mzee wa kutetema Fiston Mayele yupo zake ndani ya Yanga katika Kombe la Shirikisho Afrika akiwa ametupia kambani mabao matatu, Real Bamako kawatungua mabao mawili na bao moja kawatungua US Monastir.