Dar es Salaam. Mpango wa usajili wa Simba na Yanga huenda ukageuka neema kwa klabu nyingine kama ilivyowahi kutokea nyakati za nyuma.
Licha ya idadi kubwa ya klabu kutokuwa na misuli ya kiuchumi kupambana katika usajili, huenda zikanufaika kupitia wachezaji wanaoweza kutemwa na Simba, Yanga ili kupisha usajili wa wachezaji wapya.
Klabu hizo zinaweza kuwapata kirahisi bila kutumia gharama kubwa wachezaji kadhaa ambao watapewa mkono wa kwaheri na vigogo hivyo vya soka nchini ama kwa uhamisho wa moja kwa moja au mkopo.
Kutokana na mazoea ya muda mrefu ambayo yamekuwepo ya Simba na Yanga kutochukuliana wachezaji ambao wametemwa, timu za madaraja ya kati na chini zinaweza kunufaika kupitia mpango huo.
Yanga ambayo imepania kufanya mabadiliko ya kikosi kipindi cha usajili wa kiangazi, inatajwa katika mpango wa kuachana na Paul Godfrey ‘Boxer’, Juma Mahadhi, Mrisho Ngassa, Kelvin Yondani, Adeyoum Ahmed, Ally Ally, Mwarami Issa ‘Marcelo’, Rafael Daud, Patrick Sibomana, Yikpe Gnamien, David Molinga na Andrew Vincent ‘Dante’.
Kwa Simba huenda isifanye usajili mkubwa lakini wachezaji ambao wamekuwa wakitajwa kuwa katika mpango wa kuachana nao ni Marcel Kaheza, Mohamed Rashid, Paul Bukaba, Mohamed Ibrahim, Haruna Shamte, Abdul Selemani, Said Mohammed ‘Nduda’ na Said Ndemla.
Pia Soma
- Simba, Yanga zaizidi kete TP Mazembe
- Chama? msikilize Eymael
- Bosi GSM : Pesa ya kushusha mashine kali Yanga ipo
Uthibitisho wa hilo ni namna Polisi Tanzania ilivyoneemeka msimu huu kutokana na uwepo wa wachezaji watatu iliowapata kutoka Yanga ambao ni Pius Buswita, Matheo Anthony na Pato Ngonyani.
Anthony ameshaifungia timu hiyo mabao manne katika Ligi Kuu wakati Ngonyani anayecheza nafasi ya kiungo mkabaji amekuwa tegemeo katika safu ya ulinzi ya Polisi iliyoruhusu nyavu kutikiswa mara 26 wakati Buswita amekuwa chachu ya kupika mabao akicheza nafasi ya winga.
Pia Polisi inanufaika na uwepo wa Kaheza ambaye anacheza kwa mkopo katika klabu hiyo akiifungia mabao matatu na kupiga pasi nne zilizozaa mabao katika Ligi Kuu hadi sasa.
Namungo ni miongoni mwa timu zilizoruhusu idadi ndogo ya mabao ikiwa imefungwa mabao 25 na hapana shaka mchango wa beki wa kati Paul Bukaba anayecheza kwa mkopo akitokea Simba umesaidia katika ulinzi.
Kinda Abdul Selemani ambaye yuko kwa mkopo Ndanda akitokea Simba amefunga mabao matatu.
Kocha wa Mtibwa Sugar, Zuberi Katwila alisema siri ya wachezaji wanaotoka Simba na Yanga kutamba katika timu za chini ni kutokuwa na presha kubwa na kupata maandalizi mazuri.
Kocha wa Namungo Hitimana Thiery alisema ni mapema kuthibitisha kama atasajili wachezaji watakaoachwa Simba na Yanga msimu ujao.
“Nadhani ligi itakapokwisha ndio nitakuwa na nafasi ya kutazama mahitaji niliyonayo kikosini na kufanya tathmini ya aina ya wachezaji ninaowahitaji ila kwa sasa suala la usajili bado kidogo,” alisema Hitimana.