Uongozi wa Polisi Tanzania umekaa kikao kujadili mambo mbalimbali na mojawapo ni kutoa motisha katika timu yao ili ifanye vizuri na kuepuka janga la kushuka daraja kutokana na kutokuwa kwenye mazingira salama.
Katika kikao hicho kilichofanyia makao makuu ya Polisi, Moshi moja ya ajenda kubwa ni kuongeza bonasi za wachezaji kwenye kila mchezo wakiamini kwa kufanya hivyo italeta morali na motisha ya wao kupambana zaidi.
Akizungumza na Mwanaspoti mmoja wa kiongozi wa klabu hiyo aliliambia Mwanaspoti, mastaa wao awali hawakuwa wanapata kiasi kikubwa cha fedha kutokana na mishahara wanayolipwa ingawa wameamua kuondoa utaratibu huo.
"Kila mchezo una kiwango chake lakini kwa mechi za kawaida kila mchezaji alikuwa anapata sh50, 000 na baada ya majadiliano ya kina tumeona ni vyema tukiongeza wakati tunaenda mwisho wa ligi tumeongeza hadi 70,000 kwa kila mechi ambayo watashinda," kilisema chanzo chetu.
Kwa upande wa Katibu Mkuu wa timu hiyo, ASP Michael Mtebene alisema michezo miwili ya ugenini imewapa mwanga mkubwa wa kuamini bado wana nafasi kubwa ya kubaki Ligi Kuu licha ya kukiri ushindani umeongezeka kwa timu za chini.
Kikosi hicho kinachonolewa na Mkongomani, Mwinyi Zahera kilitoka sare ya bao 1-1 juzi dhidi ya Geita Gold na kukifanya kuvuna pointi nne ugenini katika michezo miwili baada ya kuifunga Namungo FC mabao 2-0, Januari 14.