Aaada ya kucheza mechi tano sawa na dakika 450, bila ushindi hali hiyo imemshtua kocha mkuu wa Mtibwa Sugar, Habibu Kondo akikiri vijana wake kutofanya vizuri huku akiahidi kutumia siku 14 kusuka upya timu.
Mtibwa Sugar haijawa na matokeo mazuri kufuatia mechi tano ilizocheza Ligi Kuu bila kuonja ushindi wowote na kuwa nafasi mbili za mkiani na kuweka presha kubwa katika vita ya kukwepa kushuka daraja.
Pia timu hiyo imeonekana kutokuwa imara kwenye sehemu ya beki kutokana na kila mchezo kuruhusu bao na kufanya wavu wake kufungwa mabao tisa hadi sasa na kufunga manne tu.
Akizungumza jijini Mbeya, Kondo alikiri ligi ni ngumu, lakini nyota wake pia wamekuwa wakifanya makosa mengi akisema kuwa kwa kipindi cha wiki mbili Ligi Kuu ikisimama kwa muda atasahihisha upungufu ulioonekana.
Alisema anaenda kuisuka timu nzima kuanzia eneo la kipa hadi ushambuliaji kutokana na makosa kuonekana maeneo yote na kuipa matokeo yasiyoridhisha timu yake huku akiwatuliza mashabiki kuwa Mtibwa itasimama imara.
“Inatusikitisha sana, kila siku tunasahihisha makosa, lakini yanajirudia yaleyale, timu nzima inaonekana kuwa na tatizo, tunaenda kujisahihisha tena ili kurudi katika muonekano mwingine,” alisema.