Mastaa wa Liverpool wanamtaka Pep Lijnders kuchukua mikoba ya Jurgen Klopp mwishoni mwa msimu huu na kuendeleza falsafa za Mjerumani huyo huko Anfield, imeelezwa.
Kocha, Klopp ataachana na Liverpool mwishoni mwa msimu huu, huku akipambana kuhakikisha timu hiyo inabeba mataji ya kutosha katika msimu wake wa mwisho baada ya kunyakua Kombe la Ligi na bado ipo kwenye msako wa taji la Ligi Kuu England na Europa League.
Klopp amekuwa kwenye kikosi hicho cha Anfield kwa miaka tisa, lakini Mdachi Pep Lijnders amekuwa kweye timu hiyo kwa muda mrefu zaidi.
Kwa mujibu wa taarifa, wakali wawili Alan Brazil na Dean Saunders, wachezaji kuna mtu wanamtaka akabidhiwe mikoba baada ya Klopp kuondoka.
Brazil alisema: “Nimeambiwa wachezaji hawajali kama watanolewa na namba mbili, Pep achukue timu.” Saunders aliongeza: “Nilisikia hilo. Walau Lijnders anafahamu kinachoendelea kwenye timu. Ni uamuzi mgumu sana, nani unampa timu? Ile klabu ni kubwa.”
Lijnders alijiunga na Liverpool kwa mara ya kwanza mwaka 2014 na kufanya kazi na Kocha Brendan Rodgers kabla ya kuungana na Klopp na kuwa kwenye benchi lake la ufundi. Alibaki kwenye timu kwa miaka mitatu kabla ya kuondoka kwenda kuinoa NEC huko Uholanzi. Lakini, alirudi baada ya mwaka mmoja na kujiunga tena kwenye benchi la ufundi la Mjerumani Klopp.
Kocha wa Bayer Leverkusen, Xabi Alonso amekuwa akipewa nafasi kubwa ya kwenda kumrithi Klopp, huku makocha wengine wanaohusishwa na timu hiyo ni Roberto De Zerbi wa Brighton, Julian Nagelsmann wa Ujerumani na Ruben Amorim wa Sporting Lisbon.