Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mastaa Ligi Kuu wanaogopa kupanda ndege

Mhilu Yusuph KGR Yusuph Mhilu.

Mon, 26 Feb 2024 Chanzo: Mwananchi

Maisha ya wanasoka siyo ya kuishi sehemu moja, wanasafiri kwenda mikoani na nchi tofauti kwa ajili ya kutimiza majukumu yao.

Mara nyingi wachezaji wengi wamekuwa wakipanda ndege baada ya kujiunga na timu za ligi kuu kwa kuwa wengine wametoka vijijini kabisa.

Lakini kuna ambao wamezaliwa mjini na hawataki kusikia chochote kuhusu kupanda ndege kwa kuwa wana asili tu ya uongo.

 Wapo baadhi ambao usafiri wa ndege kwao ni changamoto, lakini wengine wanaufurahia sana.

Spoti Mikiki kupitia gazeti la Mwananchi, limefanya mahojiano na baadhi ya wachezaji, waliopo Ligi Kuu na wengine kwa sasa wapo huru, wamezungumzia jinsi ambavyo wanaogopa ndege, wengine wakisimulia matukio yaliowatisha zaidi.

Juma Makapu -Mashujaa Kiungo mkabaji wa Mashujaa FC, Juma Makapu anasema anaouogopa usafiri wa ndege na mara nyingi akipanda huwa anasumbuliwa na kichwa na anahitaji mtu wa kumsaidia, kinachomtisha zaidi ni mawingu na wakati inatua.

"Kwa mara ya kwanza kupanda ndege ni mwaka 2014, nilikuwa na Timu ya Taifa ya Maboresho, tulikuwa tunaenda Mbeya, kuna mchezaji alinisaidia sana, akawa ananipa maji na kunishika, wakati nilipokuwa naogopa ndege ikiwa kama inayumba,"anasema na kuongeza;

"Safari ya nje ya kwanza 2014/15, Yanga ilikwenda kuweka kambi Uturuki, nakumbuka nilitapika sana na aliyekuwa ananisaidia ni Pato Ngonyani, kunipa maji, kunishika pale nilipokuwa naona hapa ni mwisho wangu, hadi nafika kichwa kiliniuma sana."

Yusuph Mhilu -Geita  Straika wa zamani wa Yanga na Simba, Yusuph Mhilu ambaye kwa sasa anacheza Geita Gold anasema sababu inayofanya awe na hofu na usafiri wa ndege ni mahesabu anayopiga ya kutoka angani hadi chini ya ardhi.

"Nimesafiri kwa nyakati tofauti, nikiwa na Simba na Yanga, ila sikuwahi kuwa na amani, nilikuwa nawaza hivi likitokea jambo lolote hapa nitafanya nini, ukiacha ndege naogopa sana kupanda bodaboda labda itokee dharura  nakuwa sina cha kufanya,"anasema.

Jamal Mnyate - Huru Mchezaji wa zamani wa Simba na Stars, Jamal Mnyate, aliwahi kusema hapendi kabisa usafiri wa ndege, alijikuta analazimika kupanda akiwa na timu kwa kuwa hana jinsi, tukio lililomtisha  2011 wakati anacheza Azam FC aliitwa kikosi cha Stars U-23, ambapo kulitokea changamoto wakiwa angani.

"Nakumbuka kocha alikuwa Jamhuri Kihwelo 'Julio' tulikuwa tunakwenda Comoro, ndege ilipata shida tukiwa angani, niliwaza nitafia nchi za watu, tangu hapo niliingiwa na uoga sana,"anasema na kuongeza;

 "Nikiwa Simba, nilikuwa napenda kukaa karibu na Pascal Wawa, ndege ikianza kupaa ama kushuka nilikuwa namshikilia kwa nguvu, basi alikuwa anacheka sana na kuniambia 'What’s wrong with you' pamoja na hayo yote alikuwa ananisaidia sana, ila ndege sio usafiri ninaoweza kupanda kwa kupenda."

Hamis  Nyenye -Namungo  Kiungo wa Namungo FC, Hamis Nyenye anasema mwaka 2021 timu yao, ilipata nafasi ya kucheza Kombe la Shirikisho Afrika (Caf), wakati inakwenda Angola kucheza dhidi ya De Agosto ya Angola hakusafiri, kisa kuogopa ndege.

 "Niliwaomba viongozi na makocha, kwamba sitaweza kusafiri kwa sababu naogopa ndege, wakati timu imesafiri mimi nilibaki kambini, nikawasubiri hadi waliporejea Tanzania,"anasema.

Wilbol Maseke -KMC Kipa wa KMC, Wilbol Maseke anasimulia sababu ya kuogopa usafiri wa ndege akiwa Azam FC "Ilikuwa mwaka 2022 tulikuwa tunasafiri kwenda kucheza dhidi ya Kagera, nikiwa ndani ya ndege nilimsikia mhudumu akisema kuna tatizo, ingawa Kiingereza siyo mtalaamu sana ila nilielewa kuna hatari.

 "Wachezaji tunapenda kukaa siti za nyuma, nikasimama na kutoa begi langu, wenzangu wakaanza kunicheka na kuona nimechanganyikiwa, walipoona wazungu watano ambao walikuwemo ndani ya ndege hiyo, wakaanza kutoa mabegi yao, ndipo wakaniamini kama nilielewa tangazo la mhudumu, likatoka tangazo lingine kwamba tutabadilishiwa ndege.

 "Baada ya muda wakaja na tangazo wamerekebisha ndege ilikuwa na shida ya milango, tukatakiwa kupanda kuendelea na safari, nikagoma akaja kocha na meneja wa ndege nikakataa, nikageuka na mabegi yangu kurejea kambini, tangu hapo nikawa nasafiri na basi pekee yangu zaidi ya  10, nikifika jioni ama usiku miguu imevimba wenzangu walikuwa wananicheka."

Hussein  Kazi -Simba  Beki wa kati wa Simba, Hussein Kazi anasema analazimika kupanda ndege, kutokana na majukumu ya timu na kwa mara ya kwanza ilikuwa 2015 akiwa na Simba B, kikosi cha wakubwa kilihitaji huduma yake kwa muda, hivyo akatoka Dar es Salaam kwenda Zanzibar.

 "Niliwahi kucheza Simba B 2015, kabla ya kusajiliwa timu ya wakubwa msimu huu, kikosi cha wakubwa kilikuwa kimeweka kambi Zanzibar sasa kuna beki aliumia, ndipo nikapandishwa ndege kwenda kuziba pengo, kwa sasa napanda kwa sababu sina namna na naanza kuzoea," anasema.

Edward  Christopher -Huru Mshambuliaji wa zamani wa Simba, Edward Christopher, anasema "Naogopa usafiri wa ndege, mara nyingi nikiwa angani mawazo mengi potofu yanakuwa yananijia kwamba ikidondoka nitavunjika vipande vipande, ukiacha huo naogopa sana bodaboda, nimewahi kupata ajali mara mbili."

Chanzo: Mwananchi