Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mastaa Ligi Kuu waibeba Pamba Jiji ikigawa dozi Nyamagana

Pamba Jiji FC Mastaa Ligi Kuu waibeba Pamba Jiji ikigawa dozi Nyamagana

Tue, 12 Sep 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Pamba Jiji FC imeanza kwa kishindo Ligi ya Championship ikipata ushindi mnono wa mabao 4-0 dhidi ya Cosmopolitan ya jijini Dar es Salaam huku mastaa wao ambao wamesajiliwa kutoka timu za Ligi Kuu waking'ara.

Pamba Jiji FC ambayo kwa sasa inamilikiwa na Halmashauri ya Jiji la Mwanza imepata ushindi huo mnono leo Septemba 11, 2023 katika uwanja wa Nyamagana kwenye mchezo huo wa mzunguko wa kwanza ambao umechezwa kuanzia saa 10:00 jioni.

Katika mchezo huo ambao umekuwa na mvuto ukihudhuriwa na mashabiki wengi, mabao matatu ya Pamba yamefungwa na wachezaji ambao wametua dirisha kubwa kutoka timu za Ligi Kuu Bara.

Nyota, Haruna Chanongo amefungua ukurasa wa mabao akifunga kwa mkwaju wa penalti katika dakika ya 17 baada ya mabeki wa Cosmopolitan kumuangusha katika eneo la hatari mshamhuliaji, Jamal Mtegeta.

Pamba imepata bao la pili dakika ya 27 kupitia kwa winga wake, Jamal Mtegeta aliyesajiliwa kutoka Dodoma Jiji, ambaye amefunga kwa kichwa akiunganisha vyema krosi iliyochongwa na beki wa kulia, Frank Mwinga.

Mshambuliaji wa zamani wa Coastal Union na Tanzania Prisons, Mudathir Said ameifungia Pamba bao la tatu mnamo dakika ya 45 na kuipeleka timu yake kifua mbele ikienda mapumziko kwa uongozi wa mabao 3-0.

Kipindi cha pili, Cosmopolitan ya jijini Dar es Salaam ambayo imepanda daraja msimu huu baada ya kuwa bingwa wa First League msimu uliopita, imeingia ikiwa imara na kufuta makosa hivyo kuimudu Pamba ambayo imeshindwa kufurukuta kwa takribani dakika 40.

Hata hivyo, dakika ya 80, kiungo, Lazaro Mlingwa akaiandikia Pamba bao la nne na la ushindi kwa shuti kali baada ya kutokea heka heka katika lango la Cosmopolitan, dakika 90 za mchezo huo zimemalizika Pamba ikiibuka na ushindi wa mabao 4-0.

Baada ya ushindi huo Pamba inaungana na timu nyingine za Fountain Gate Talents, Mbeya City na Pan African zilizoshinda mechi zao za kwanza huku ushindi huo ukiipeleka kileleni mwa msimamo wa Ligi ya Championship.

Pamba itarudi dimbani Septemba 15, mwaka huu katika Uwanja wa Nyamagana, Mwanza kumenyana na Pan African, huku Cosmopolitan ikivaana na Copco Veteran FC katika Uwanja wa CCM Kirumba Septemba 16, mwaka huu.

Akizungumzia kichapo hicho, Kocha wa Cosmopolitan, Abbasi Marijani amesema mchezo huo umekuwa mzuri na wameingia na mpango mzuri lakini kwa namna fulani maamuzi ya marefarii likiwamo tukio la penalti yamewatoa mchezo vijana wake huku akiwapongeza kwa kupambana katika mchezo wao wa kwanza wa ligi.

Chanzo: Mwanaspoti