Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mastaa Ligi Kuu na ulimwengu wa mapenzi

Mastaa Ndoa Mastaa Ligi Kuu na ulimwengu wa mapenzi

Mon, 29 Jan 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Ukiachana na ufundi ambao wachezaji wanaonyesha uwanjani na kuwapa burudani mashabiki wao, wana ulimwengu mwingine wa kimapenzi unaowafanya wawe wabunifu kwa wenza wao.

Awamu hii, Spoti Mikiki inakufichulia habari za baadhi ya wachezaji wakizungumzia upande wa mapenzi upoje, swali likiwa kwa mara ya kwanza kuwakaribisha wapenzi wao waliwawekea nyimbo zipi na walijiandaaje?

Ingawa kwa asilimia kubwa wengi wao siku ya kwanza walionekana kuigiza maisha - kwa kufanya usafi wa nyumba tofauti na uhalisia wa kila siku, lengo kubwa ilikuwa ni kuwaonyesha wenza wao kwamba ni watu wastaarabu na wenye malengo.

Baadhi yao wamefanikiwa kuwaoa wanawake hao huku wengine imekuwa zilipendwa kwani wameendelea na maisha mengine mapya baada ya kukumbana na changamoto za hapa na pale.

JACOB MASAWE-NAMUNGO

Kiraka wa Namungo FC, Jacob Masawe anasema alisoma na mkewe Beatrice, wakati wapo kidato cha pili alivutiwa na nidhamu na Uchamungu wake akaamua kumfuata na kumueleza anampenda na atamuoa.

"Nakumbuka siku ya kwanza kumualika nyumbani kwangu nilimuwekea wimbo wa 'Huyu ni chaguo lako ulioimbwa na Manesa Sanga ukatupa nguvu ya kuweka malengo ya kuoana," anasema.

"Katika msimu wa 2010/11 nilipata tuzo niliyopewa Sh 2,650,000 nikaenda moja kwa moja kutoa mahari na tangu tufunge ndoa tuna miaka 12 na tumefanikiwa kupata watoto wawili."

BENJAMIN ASUKILE-PRISONS

Nahodha wa Tanzania Prisons, Benjamin Asukile anasema alikutana na mkewe mwaka 2013 kipindi hicho walikuwa wapenzi

"Kwa mara ya kwanza nilikutana naye njiani mkoani Tabora, wakati huo nilikuwa nacheza Kagera Sugar, hivyo tulikuwa tunakwenda kucheza na Rhino Rangers, nilivaa kitanashati sana, kunukia vizuri, kwani nilijua anaweza akanikumbatia.

"Alikuwa anasoma Chuo cha Utumishi wa Umma kilichopo Tabora. Hosteli aliyokuwa anakaa alikuwa chumba kimoja na mdogo wangu. Nilikuwa nikimpigia mdogo wangu alikuwa ananiambia nina rafiki yangu msalimie baadaye akachukua namba ya simu akawa ananipigia. Hapo ndipo yalipoanzia mahusiano.

"Siku ya kwanza niliyomkaribisha nyumbani, nilitandika mashuka mapya, nikanunua pafyumu za ndani, nikapulizia hivyo chumba kikawa kinanukia vizuri, nyimbo nilizokuwa nazipiga siku hiyo zilikuwa za mwanamuziki kutoka Congo, Jean Baron nikaona kazielewa na akaingia laini na sasa ni mke na mume na tuna watoto," anasema Asukile.

DEOGRATIUS MUNISHI-NAMUNGO

Kipa wa Namungo FC, Deogratius Munishi 'Dida', anasema alikutana na mpenzi na sasa mkewe, mkoani Songea wakati anacheza Manyema ya Daraja la Kwanza.

"Alikuja uwanjani nilivyomuona kwa mara ya kwanza nikampenda. Wakati nakwenda kupeleka ombi la kumpenda nikajiweka kitanashati bahati nzuri na yeye alikuwa ananipenda," anasema.

"Nilichokifanya wakati nimeondoka Songea nikamtumia nauli na kumuelekeza kwangu na sasa tuna miaka 15 kwenye ndoa yetu, tuna watoto wawili Born na Luise, hivyo ingekuwa ngumu kumuwekea mziki kwani sikuwepo nyumbani."

JUMA MAKAPU-MASHUJAA

Beki wa zamani wa Yanga na sasa Mashujaa FC, Juma Makapu anasema siku ya kwanza kumkaribisha mpenzi wake nyumbani kwake alimuwekea wimbo wa Mr Blue wa Pesa na alifanya usafi wa kutosha, ili aonekane mwanaume mtanashati na mwenye malengo makubwa.

Pamoja na hayo yote kila mmoja ameendelea na maisha yake.

ADAM ADAM-MASHUJAA

Mshambuliaji wa Mashujaa FC , Adam Adam aliyefunga mabao matano kwenye Ligi Kuu, anasema alifunga ndoa 2014 akiwa Azam B.

"Nilifungia mkoani Moshi nikiwa kazini, kipindi hicho nilikuwa naishi kwa wazazi wangu Kawe, sasa baada ya kurejea Dar es Salaam nikamtumia nauli aje, wakati naenda kumpokea Kimara, niliacha nimefanya usafi wa kutosha chumbani kwangu, kwani nyumba ilikuwa kubwa, kisha nikapiga pamba za maana," anasema Adam

Anaongeza: "Tumefanikiwa kupata watoto wawili wa kwanza anaitwa Amina (9) na Omary (2), watoto wote nimempeleka hospital mwenyewe, baada ya kumuacha huko nikarudi nyumbani kufanya usafi wa maana, tuna miaka 10 kwenye ndoa."

ABDALLH SHAIBU -LUBUMBASHI

Beki wa zamani wa Yanga, Abdallah Shaibu ‘Ninja’ kwa sasa anaichezea FC Lubumbashi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), anasema kwa mara ya kwanza kumkaribisha mchumba wake kwake na sasa ni mkewe, alianza kufanya usafi wa maana, kutandika mashuka mapya, kamuandalia zawadi za hapa na pale, kisha akawa anapiga miziki tofauti ya kizungu.

YOHANA NKOMOLA-TABORA

Mshambuliaji wa Tabora United, Yohana Nkomola anasema siku ya kwanza kumkaribisha mpenzi nyumbani kwake alimuwekea nyimbo za msanii wa Bongo Fleva, Diamond Platnumz na alifanya usafi wa kutosha nyumbani kwake.

"Ukiwa msela hasa sisi wachezaji unaamka asubuhi kwenda mazoezini unasema nitatandika kitanda nikirudi. Baada ya mazoezi unakuwa umechoka, hivyo inakuwa ngumu kufanya usafi kihivyo," anasema Nkomola.

CHARLES ILANFYA-MTIBWA

Mshambuliaji wa Mtibwa Sugar, Charles Ilanfya anasema: "Sikuwa na mambo mengi ya kuweka muziki, ila nilifanya usafi wa kutosha, nakumbuka niliwasha tv kuangalia vipindi mbalimbali, huku nikimpigisha stori za hapa na pale."

Chanzo: Mwanaspoti