Kali Ongala, Kocha Mkuu wa Azam FC, amewaonya mastaa wa timu hiyo huku akiwaambia kwamba ni lazima wajitafakari kutokana na matokeo wanayopata.
Timu hiyo mchezo uliopita wa Ligi Kuu Bara, ilishuhudia ubao wa Uwanja wa Highland ukisoma Ihefu 1-0 Azam FC, jambo lililowafanya waache pointi tatu mazima ugenini.
Kipigo hicho kimeifanya Azam kutolewa rasmi kwenye mbio za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu kutokana na mechi zake tano zilizobaki kuwapa pointi ambazo hazitawafikia vinara Yanga wenye pointi 65. Azam wana pointi 47, wakishinda zote tano watafikisha 62.
Ongala amesema: “Kilichotokea kwenye mchezo wetu uliopita tulikaa na wachezaji na kuzungumza nao na kuwaambia kwamba wanapaswa wajitafakari kutokana na kile ambacho kinatokea.
“Lakini muhimu zaidi ni kuwa na mwendo mzuri na kufanya yote kwa vitendo kwani tunaweza kuzungumza siku nzima na tusimaliz.”
Timu hiyo ilikuwa imealikwa kucheza na Gor Mahia ya Kenya Jumapili katika mchezo wa kirafiki, safari hiyo imesitishwa kutokana na sababu za kiusalama.