Wachezaji na benchi la ufundi la timu ya taifa ya Angola wamepewa zawadi ya pesa pamoja na simu, iPhone 15 baada ya kutinga robo fainali ya michuano ya Afcon 2023 inayoendelea huko Ivory Coast, imeripotiwa.
Kikosi hicho cha Angola maarufu kama Palancras Negras kiliichapa Namibia mabao 3-0 katika mchezo wa mtoano wa raundi ya 16 bora Jumamosi iliyopita na kutinga robo fainali ambapo watakuwa na kasheshe la kuwakabili Nigeria, ambayo iliwatupa nje Cameroon kwa ushindi wa mabao 2-0.
Mchezo huo wa Angola na Nigeria wa kusaka tiketi ya kutinga nusu fainali, utapigwa uwanjani Felix Houphouet-Boigny, Abidjan, Ijumaa wiki hii.
Kwa mujibu wa taarifa za kutoka Angola, Banco Angolano de Investimento, benki ya Luanda, Angola, ilitangaza kwamba kila mchezaji na benchi la ufundi watapokea Kwanza 5 milioni (Sh15.2 milioni)
Aguinaldo Jaime, rais wa Bodi ya Wakurugenzi ya UNITEL, kampuni binafsi ya simu za mkononi huko Angola, nayo imetoa zawadi ya simu aina iPhone 15 pamoja na muda wa maongezi, SMS na intaneti bure kwa kila mtu aliyekuwapo katika kikosi cha Angola kilichopo kwenye fainali hizo huko Ivory Coast.
Kampuni nyingine ya Sodiam EP imetangaza itatoa zawadi ya Dola 250,000 (Sh634.5 milioni kwa wachezaji na benchi la ufundi kama timu ya Angola itafika fainali za Afcon 2023.
Angola na Nigeria zitakutana huku kila timu ikiwa haijapoteza mchezo wowote kwenye fainali hizo. Super Eagles imecheza mechi nne bila ya kupoteza baada ya ushindi wao mbele ya Cameroon, Guinea-Bissau, Ivory Coast na kutoka sare na Equatorial Guinea na watapambana kutinga nusu fainali kwa mara ya 16 kwenye historia yao, huku Palancas Negras wao watasaka nusu fainali yao ya kwanza kwenye AFCON.