Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mastaa 10 wanaosota benchi Ligi Kuu Bara

97027 Benchi+pic Mastaa 10 wanaosota benchi Ligi Kuu Bara

Wed, 26 Feb 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Zimebaki raundi 15 kabla ya msimu wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2019/2020 kumalizika rasmi ingawa zipo timu ambazo zimebakiza idadi kubwa ya mechi baada ya kucheza michezo pungufu.

Wakati ligi ikiwa katika hatua ya lala salama, wapo wachezaji ambao wamekuwa muhimili wa timu zao kutokana na kucheza mara kwa mara ingawa wapo ambao wamekuwa wakisota benchi ingawa awali walikuwa tishio katika timu zao.

Kuna wachezaji ambao wanakaa benchi kutokana na viwango vyao kutoridhisha makocha wao lakini wapo ambao hawapati nafasi ya kucheza kutokana na ubora na uwezo wa wachezaji wanaocheza katika nafasi zinazofanana.

Spoti Mikiki inawamulika wachezaji kumi ambao wana kiwango kizuri ambacho pengine kingewafanya wawe mastaa kwingine lakini kutokana na ushindani na ubora wa wachezaji wanaowania namba katika timu zao, hivi sasa wanasota benchi.

Manyika Peter-Polisi Tanzania

Amejiunga na Polisi Tanzania katika dirisha dogo la usajili akitokea KCB inayoshiriki Ligi Kuu ya Kenya.

Pia Soma

Advertisement
Alitarajiwa kuwa kipa chaguo la kwanza katika kikosi cha Polisi kutokana na uwezo na uzoefu wake lakini amekuwa akisota benchi akishindwa kumpoka nafasi kipa Mohammed Yusuph ambaye amekuwa akionyesha kiwango bora.

Gadiel Michael-Simba

Alisajiliwa na Simba akiwa beki chaguo la kwanza upande wa kushoto katika timu ya taifa ‘Taifa Stars’ na Yanga.

Maisha yake Simba yamekuwa magumu kwani hana nafasi ya kudumu kutokana na uwepo wa beki Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ ambaye hata katika kikosi cha Taifa Stars wamekuwa wakiwania namba.

Feisal Salum ‘Fei Toto’-Yanga

Ni mchezaji mzuri katika nafasi ya kiungo na timu nyingi zinamtamani ili ajiunge nazo lakini ndani ya kikosi cha Yanga amekuwa na wakati mgumu msimu huu mbele ya Mapinduzi Balama na Haruna Niyonzima ambao wamekuwa wakipangwa nafasi yake.

Stahimil Mbonde-Mtibwa Sugar

Ameanza kupewa nafasi katika siku za hivi karibuni lakini amekuwa akisota benchi kwenye mechi nyingi za Mtibwa Sugar ambapo nafasi yake imekuwa ikichezwa na Riffat Hamisi.

Daniel Amoah-Azam FC

Ni beki ambaye idadi kubwa ya timu za Ligi Kuu zinavutiwa naye lakini uwepo wa Aggrey Morris na Yakub Mohammed umekuwa ukimnyima nafasi pindi wawili hao wakiwa fiti ingawa amekuwa akicheza wanapotumia mfumo wa kuchezesha mabeki watatu wa kati.

Mohammed Mkopi-Polisi

Tanzania

Ni mshambuliaji mwenye uwezo wa hali ya juu wa kufumania nyavu, kupiga pasi za mwisho na kuchezesha timu lakini uwepo wa Sixtus Sabilo na Matheo Anthony umemfanya awe anasugua benchi.

Awesu Awesu-Kagera Sugar

Fundi wa kumiliki mpira, kupiga pasi na kuvunja ukuta wa timu pinzani lakini amekuwa hapati nafasi katika kikosi cha kwanza cha Kagera Sugar mbele ya Abdallah Seseme.

Awesu alitabiriwa makubwa wakati ligi inaanza kutokana na uhodari wake akicheza na kinara mwingine wa mabao Yusuf Mhilu, lakini kwasasa amepotea.

Richard Djodi-Azam FC

Ni mshambuliaji mahiri ambaye amekuwa akifunga mabao kila anapopewa nafasi na hadi sasa ameweka wavuni matatu Azam katika Ligi Kuu lakini uwepo wa Obrey Chirwa ambaye ni chaguo la kwanza umekuwa ukimnyima nafasi.

Patrick Sibomana-Yanga

Alianza vizuri msimu huu akiifungia Yanga mabao manne katika Ligi Kuu lakini ghafla anasota benchi akishindwa kupata namba mbele ya winga raia wa Ghana, Bernard Morrison ambaye ndiye amekuwa akianza.

Yusuf Mlipili-Simba

Ni mmoja wa mabeki wazuri wa kati ndani ya kikosi cha Simba na alikuwa nyota muhimu misimu miwili iliyopita akipewa nafasi mara kwa mara ya kucheza.

Hata hivyo mambo yamekuwa magumu msimu huu ambapo ameshindwa kucheza hata mechi moja ya Ligi Kuu baada ya kushindwa kufua dafu mbele ya mabeki Kennedy Juma, Tairone Santos, Pascal Wawa na Erasto Nyoni.

Chanzo: mwananchi.co.tz