Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mashujaa yatanguliza mguu Ligi Kuu, dakika 90 kuamua Mbeya

Mashujaa FC VS Mbeya City Mashujaa yatanguliza mguu Ligi Kuu, dakika 90 kuamua Mbeya

Mon, 19 Jun 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Mashujaa FC imeanza vizuri kampeni yake ya kucheza Ligi Kuu msimu ujao baada ya leo kupata ushindi kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza wa mtoano dhidi ya Mbeya City.

Timu hiyo yenye maskani yake mkoani Kigoma, imepata ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Mbeya City kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika na kutanguliza mguu mmoja Ligi Kuu huku ikisubiri kujihakikishia nafasi hiyo katika mchezo wa marudiano utakaopigwa Juni 22, mwaka huu jijini Mbeya.

Mchezo huo umepigwa kuanzia saa 10 jioni ukichezeshwa na mwamuzi, Tatu Malongo kutoka Tanga huku uwanja ukiwa umefurika nyomi la mashabiki, ambapo Mashujaa imetangulia kupata bao dakika ya 23 likifungwa na Abiud Mtambuku ambaye amemalizia mpira ulioshindwa kuondolewa na mabeki wa Mbeya City.

Bao hilo limedumu kwa dakika 45 za kwanza Mashujaa ikienda mapumziko kifua mbele kwa bao 1-0. Kipindi cha pili kimeanza kwa Mbeya City kufanya mabadiliko ya wachezaji dakika ya 46, akitoka Shaban Dulaz na kuingia Frank Ikobela.

Mabadiliko hayo yameipa uhai timu hiyo na kupata bao la kusawazisha dakika ya 63 likifungwa na Gasper Mwaipasi hata hivyo furaha yao haikudumu kwani dakika ya 69, Mashujaa imepata bao la pili likifungwa na Asanga Stalon.

Mashujaa inayonolewa na Meja mstaafu Abdul Mingange na Rashid Chama, imepata bao la tatu kwa mkwaju wa penalti dakika ya 78 likifungwa na Shadrack Ntabindi baada ya mshambuliaji, Abiud Mtambuku kuangushwa ndani ya eneo la 18 na beki wa Mbeya City, Kenneth Kunambi.

Wachezaji, David Mwasa na Kenneth Kunambi wa Mbeya City wameonyeshwa kadi ya njano mnamo dakika ya 21 na 75 wote wakimfanyia madhambi, mshambuliaji wa Mashujaa, Abiud Mtambuku ambaye pia ameonyeshwa kadi ya njano dakika ya 23 baada ya kushangilia kwa kuvua jezi.

Mashujaa imevaana leo na Mbeya City baada ya kuibuka na ushindi wa jumla wa mabao 5-4 dhidi ya Pamba katika mchezo wa playoff, huku Mbeya City ikichapwa na KMC kwa jumla ya mabao 3-2.

Mashujaa ilipanda daraja kucheza Championship msimu wa mwaka 2020/2021 sambamba na timu za DTB (sasa Singida Fountain Gate FC), Pan African na Green Warriors.

Mbeya City ilipanda daraja kucheza Ligi Kuu msimu wa mwaka 2012/2013 ikidumu kwa misimu 11 ambapo inapambana isishuke daraja.

Mashujaa ilimaliza katika nafasi ya nne kwenye Ligi ya Championship ikivuna pointi 49 katika michezo 28, huku Mbeya City ikimaliza ya 14 kwenye Ligi Kuu ikivuna pointi 31 katika mechi 30.

Chanzo: Mwanaspoti