'Kigoma ndipo soka lilipoanza.' Huu ni msemo maarufu kwa watu wanaotokea Mkoa wa Kigoma. Hii ni kutokana na mkoa huo kutoa wanasoka wengi. Ni mkoa uliotingisha nchini miaka ya nyuma kwa mastaa kibao kuibuka na kutamba katika timu mbalimbali za soka ndani na nje ya nchi.
Kigoma ilikuwa ikiutumia msemo huo kushindana na mikoa ya Mwanza, Morogoro na Tanga ambayo ilisifika pia ya nyuma kwa kutoa mastaa wakubwa wa soka nchini waliotamba ndani na nje ya mipaka ya Tanzania na bara zima la Afrika.
Asikuambie mtu, enzi hizo miaka ya 1970-2000, Kigoma ilikimbiza kwa mastaa kutoka mkoa huo kufunika kwelikweli, wakichuana na wale wa mikoa hiyo mingine ukiwamo wa Dar es Salaam.
Hizo Simba na Yanga na klabu nyingine zilikuwa zikibebwa na mastaa kutoka Kigoma na kikubwa walijaliwa kipaji, kujituma na kuzipambania sana timu.
Utabisha nini? Kuna watu kama Makumbi Juma 'Homa ya Jiji' a.k.a Bongabonga, Abeid Mziba 'Tekero', Mavumbi Omar, Edibily Lunyamila, Alphonce Modest, Said Sued 'Scud', Juma Kaseja, Salum Kanon, Amri Kiemba, Hussein Sued, Suleiman Kibuta na Lambele Jerome wanatokea hapo.
Pia kuna wakali kama Nteze John, Seleman Matola, Wilfred Kidao, Gerard Lukindo, Omar Issa, Kabali Faraji, Said Maulid na wengineo ambao walileta heshima ya soka nchini kutokea mkoa huo wa Kigoma kwani walijua kuwapa raha mashabiki wa soka wanapokuwa uwanjani wakisakata soka.
Hata hivyo, sijui ni upepo gani uliupitia mkoa huo na kujikuta wakiishia kwa karibu miaka 20 bila ya kuwa na klabu yoyote ya Ligi Kuu Bara, hata kama mastaa wanaotokea mkoa huo wakiendelea kuwasha moto katika klabui mbalimbali zikiwamo Simba na Yanga.
Mara ya mwisho kwa Kigoma kushuhudia mechi ya Ligi Kuu ilikuwa ni 2004, yaani tangu timu ya Reli Kigoma ambayo awali ilifahamika kama Congo FC kushuka daraja ikiwa ni msimu mmoja tu baada ya Mmbanga FC nayo kutangulia.
Kabla ya timu hizo Kigoma ilitamba na RTC Kigoma iliyowaibuka baadhi ya nyota waliolitumikia taifa kwa ufanisi mkubwa.
Baada ya kushuka kwa timu hizo, Kigoma iliishia kung'ara kwenye fani za muziki na michezo mingine, hawa kija Japhet Kaseba, Ali Kiba, Diamond, Linex, Chegge, Baba Levo, Peter Msechu, Banana Zorro na wengine waliubeba mkoa huo katika ramani ya burudani na michezo.
Katika Soka Chama cha mchezo huo mkoani humo, KRFA kilikuwa kikipambana kurejesha timu katika Ligi Kuu, lakini ilikuwa ikikwamia njiani kutokana na kilichoelezwa ujuaji mwingi uliokuwepo kwa baadhi ya wadau wa soka wa mkoa huo.
KRFA iliangushwa katika jitihada hizo kutokna na JKT Kanembwa kuishia kushushwa daraja kutoka Ligi Daraja la Kwanza (sasa Ligi ya Championship) kutokana na kashfa ya upangaji matokeo 2016, msala uliozikuta pia Polisi Tabora, Oljoro JKT na Geita Gold. Msala huo ulioibuka siku ya mechi za mwisho wa FDL, uliinufaisha Mbao FC iliyomaliza nafasi ya nne msimu huu kupandishwa daraja.
Hapo awali Kigoma ilikuwa ikiitegemea Mvuvumwa FC, iliyokuwa ikimilikiwa na mtu binafsi, lakini ikawekewa mizengwe hadi ikahama kutoka mkoani humo hadi Dar es Salaam kucheza mechi zao za Ligi Daraja la Kwanza (FDL) na kuzimika kimya kimya kabla ya kuibuka kwa Kanembwa.
MASHUJAA SASA
Hata hivyo baada ya msoto mkubwa wa miaka karibu 20 na Kigoma kupotea kwenye ramani ya soka, mambo yamebadilika baada ya timu ya Mashujaa FC juzi kupanda Ligi Kuu Bara kwa kuifunga Mbeya City kwa jumla ya mabao 4-1. Awali iliifumua kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma kwa mabao 3-1 na juzi Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya waliikandamiza tena kidude kimoja.
Kifupi ni kwamba msimu ujao, Kigoma itaziona Simba na Yanga kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika kwa raha zao wakiwa na washiriki wa ligi hiyo.
Mashabiki wa soka waliokuwa na kiu ya muda mrefu ya kushuhudia mechi za ligi zikipigwa hapo sasa wajipange tu kwani Mashujaa imewaheshimisha baada ya yenyewe kusota kwa muda mrefu kwenye Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kabla ya kubadilishwa na kuwa Ligi ya Championship ikipenya kupitia play off.
Wanajeshi wa Mpakani hao, walimaliza nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi hiyo, nyuma ya Pamba na kulazimika kuchujana wenyewe ili kupata timu ya kucheza na moja kati ya timu mbili za Ligi Kuu zilizomaliza kwenye nafasi ya 13 na 14. Mashujaa wakainyoa Pamba kwa jumla ya mabao 5-4 baada ya awali kushinda 4-0, kisha kufungwa na Pamba jijini Mwanza kwa mabao 4-0.
KMC na Mbeya City zikapepetana zenyewe na KMC ikasalimika kushuka kwa kuwafunga wapinzani wao kwa jumla ya mabao 3-2, ikilala ugenini 2-1 na kushinda nyumbani 2-0, hivyo City ikalazimika kukutana na Mashujaa ili kujiokoa isishuke.
Hata hivyo mambo yaliwaendea kombo na kushushwa daraja baada ya kudumu katika Ligi Kuu kwa miaka 10 tangu ilipopanda msimu wa 2013-2014 na kumaliza nafasi ya tatu na msimu uliofuata wa 2014-2015 kumaliza ndani ya Nne Bora. Mbeya City imezifuata Ruvu Shooting na Polisi Tanzania zilizoshuka daraja moja kwa moja kwa kushika nafasi mbili za kwisho za Ligi Kuu Bara.
Kwa upande wa Mashujaa kwa matokeo ya juzi imeungana na JKT Tanzania na Kitayosce zilizotangulia mapema kupanda kushiriki Ligi Kuu Bara msimu ujao na kuufanya mkoa wa Kigoma kwa sasa kutembea kifua mbele.
FURAHA KUBWA
Kupanda kwa Mashujaa iliyowahi kuitoa nishai Simba kwenye pambano la mechi za awali za Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) 2018, kumeresha furaha kwa mashabiki wa soka wa mkoa huo ambao mwaka juzi walionyeshwa ladha ya Simba na Yanga kwa kupelekewa fainali ya ASFC mjini humo.
Hii ni mara ya kwanza kwa Mashujaa kufika hatua mtoano kwenye Ligi ya Championship huku ikiwa inapewa sapoti kubwa na wadau wa soka mkoani Kigoma ambao walikuwa na hamu kubwa ya kushuhudia Ligi Kuu katika ardhi yao.
Mashujaa ilipata umaarufu mkubwa msimu wa mwaka 2018/19 ilipoichapa Simba na kuiondoa Kombe la Azam (ASFC) hatua ya 32 kwa mabao 3-2 na kutinga hatua ya 16 kwa mabao ya Shaabani Hamisi, Jeremiah Josephat na Rajab Athuman huku mabao ya Simba yakifungwa na Paul Bukaba dakika ya 19 na 78.
Kocha Mkuu wa Mashujaa, Abdul Mingange kabla mchezo wa juzi alisema morali kubwa ya vijana wake itasaidia kupata kitu katika mchezo huo na kuwawezesha kucheza Ligi Kuu msimu ujao na ndivyo ilivyokuwa.
Mingange anasema uongozi na wadau wa timu ndio silaha kubwa kwao kila wakati walikuwa wakiwasapoti wachezaji na kuwapa nguvu ya kupambana ili wafanikiwe.
HAPA PALINOGA
Mabosi wa mashujaa katika kuhamasisha michezo ya mwisho waliamua kuondoa viingilio ili kutoa hamasa zaidi ka wapenzi wa soka mkoani Kigoma kwa kushirikiana na Mkuu wa Mkoa, Thobias Andengenye.
Hatimaye Mashujaa ikamaliza msimu wa Ligi ya Championship ikiwa na alama 49 katika nafasi ya nne na kukutana na Pamba iliyokuwa nafasi ya tatu kwa alama 59.
Mashujaa ikashinda 4-0 nyumbani kisha ikapoteza 4-1 Uwanja wa Nyamagana, Mwanza lakini bao la ugenini likawabeba na kukutana na Mbeya City hatua ya mwisho ambapo nyumbani ikashinda 3-1 na ugenini ikashinda 1-0.
Ushindi huo ukampa nguvu Mkuu wao Mkoa ambaye alitangaza dau kwa kununua kila bao kwa Sh600,000 na kuongeza morali kwa wachezaji ambao sasa wanauhakika wa kubeba kitita hicho.
Mashujaa ilianza msimu ikiwa chini ya Kocha Jumanne Challe kisha timu ikakabidhiwa kwa Rashid Idd 'Chama' nyota wa zamani wa Yanga na Ndovu ya Arusha.
Ilipofika hatua ya mtoano mabosi wakaongeza nguvu kwenye benchi la ufundi kwa kumpa kazi maalumu kocha, Abdul Mingange kuwa kocha mkuu akisaidiana na Chama.
SHANGWE KAMA LOTE
Mwenyekiti wa Mashujaa, Abdul Tika anasema kilichotokea ni historia katika soka hasa kwa vijana hao kupambana na kurejesha heshima ya Mkoa wa Kigoma.
"Hii furaha sio ya wachezaji pekee bali kwa kila mmoja mpenda soka hasa mkoa wa Kigoma huko aliko atakuwa amejaa furaha ya aina yake kwa mafanikio haya.
"Ushirikiano tuliouonyesha unatakiwa uongezeke ili msimu ujao wa Ligi Kuu tuwe na kikosi bora zaidi na kufanya timu imara sio kupanda na kushuka," anasema Tika.
ZIJIPANGE
Hii ni mara ya pili kwa timu ya Ligi ya Championship kupanda Ligi Kuu kupitia hatua ya mtoano kwani timu ya kwanza kufanya hivyo ilikuwa Ihefu FC kwa kuiondoka Mbao FC msimu wa 2020/21.
Ihefu ilishinda nyumbani 2-0 kisha ikapoteza 4-2 ugenini lakini msimu uliofuata ikashuka daraja kabla ya kujipanga upya na kurejea tena msimu huu.
Mashujaa sasa inaungana na JKT Tanzania pamoja na Kitayosce ambazo ndio zilizotangulia kupanda Ligi Kuu baada ya kumaliza kwenye msimamo nafasi mbili za juu.
Kwa kuangalia misimu saba kuanzia mwaka 2015 timu nane zimepanda na kushuka daraja huku sababu zikionekana ni uwepo wa maandalizi mabovu kwa timu na kuwepo kwa viongozi wasiojua soka.
Msimu wa mwaka 2015/16 African Sports ilipanda na msimu uliofuata ikashuka, msimu wa mwaka 2017/18 Majimaji FC na Njombe Mji zikapanda na msimu uliofuata zikashuka, African Lyon ilipanda msimu wa mwaka 2018/19 na ikashuka msimu uliofuata.
Singida United iliyopanda Ligi Kuu msimu wa mwaka 2018/19 msimu uliofuata ikashuka daraja, Ihefu FC zilizopanda msimu wa mwaka 2020/21 msimu uliofuata zikashuka daraja na Mbeya Kwanza ilipanda msimu uliopita na msimu huu ipo Championship.