Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mashujaa ni klabu ya mfano Ligi Kuu

Fd Mashujaa Mashujaa ni klabu ya mfano Ligi Kuu

Fri, 22 Mar 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Baada ya kupata ushindi katika mechi mbili kati ya tatu za mwanzo za Ligi Kuu msimu huu, Mashujaa ikapita katika kipindi kigumu mno ambacho kama ni mgonjwa unaweza kusema alikuwa chumba cha wagonjwa mahututi.

Ikacheza mechi 13 mfulizo bila kupata ushindi na ilitoka sare katika michezo minne huku ikipoteza mechi tisa na ikafunga mabao manane huku yenyewe ikiruhusu nyavu zake kutikiswa mara 22.

Kila mmoja akaanza kuipigia hesabu za kushuka daraja hadi kusababisha baadhi ya watu wa ndani wa timu kukata tamaa na kuanza kujiondoa mmojammoja.

Miongoni mwa waliokuwa katika hali ngumu ni kocha Abdallah Mohamed ‘Baresi’ ambaye ilifikia hatua yeye mwenyewe pasipo kushurutishwa na mtu yeyote, aliamua kujiweka kando na akaandika barua kwa uongozi wa Mashujaa kuomba kupisha ili mwingine aje kuchukua nafasi yake.

Hata hivyo, uongozi wa Mashujaa FC ukatumia akili ya hali ya juu kufanya tathmini ya timu na kugundua tatizo la kufanya vibaya kwa kiasi kikubwa halisababishwi na kocha hivyo ukamjibu fasta kuwa haukubali kujiuzulu kwake na unamtaka aendelee kuwa kocha wao mkuu.

Chini ya Mwenyekiti Meja Abdul Tika, uongozi wa Mashujaa ulibaini kinachowaangusha ni kuwa na wachezaji wengi ambao wana uwezo mdogo na hata uzoefu wao kwa ligi haukuwa mkubwa hivyo wakaamua kuongeza vifaa katika dirisha dogo la usajili.

Baada ya hapo mambo yakabadilika na Mashujaa ikawa haina unyonge tena kwa kucheza mechi nne mfululizo bila kupoteza, ikishinda tatu na kutoka sare katika mechi moja kabla ya kupoteza mechi ya tano dhidi ya Simba.

Nawapongeza viongozi wa Mashujaa kwa sababu timu nyingi hapa nchini hufikiria kila zinapofanya vibaya, basi anayesababisha hivyo ni kocha na hivyo kuamua kumtimua hata kama sio yeye muhusika halisi wa kinachozitokea.

Wakati mwingine makocha wanaweza kuwa wamefanya kazi yao vizuri tu ila wakaangushwa na sababu nyingine zilizo nje ya uwezo wao.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live