Safari ni ndefu sana kwa Mashujaa FC na dereva ndio kwanza ameanza kutoa basi katika kituo cha mabasi kuelekea katika nchi ya ahadi.
Ndugu zangu Mashujaa FC wamesimama imara kwenye basi tayari kwa safari na ndoto zao ni kusafiri umbali mrefu hadi pale watakapofika mwishoni mwa safari.
Mwisho wa safari ni wapi? Ni pale msimu utakapomalizika na kufika nchi ya ahadi ni ama kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu ya NBC au kumaliza katika nafasi nne za juu katika msimu wao wa kwanza.
Inahitaji uvumilivu, subira, kuaminiana, juhudi, upendo na ushirikiano kwa pamoja ili kushikilia bomba hadi mwisho wa safari na kupata kile wanachokitegemea jambo ambalo sio rahisi na ili litimie wanatakiwa kuvuja jasho hasa.
Wakifanikiwa kuwa na vitu nilivyovitaja hapo juu, hapana shaka Mashujaa watakuwa na muendelezo mzuri wa kile walichokianza katika michezo miwili ya mwanzo ya Ligi Kuu dhidi ya Kagera Sugar waliyoshinda kwa mabao 2-0 na ule dhidi ya Geita Gold ambao walitoka sare tasa.
Msimu hautakuwa mzuri kwa kucheza Ligi Kuu tu kwa mara ya kwanza bali pia wanaweza hata kumaliza katika nafasi za juu kwenye msimamo ambazo ni ndoto ya timu nyingi zinazoshiriki ligi hiyo.
Hapo watafuata nyayo za Mbeya City, Namungo FC, KMC na Singida Big Stars ambazo katika misimu yao ya kwanza tu ziliweza kutikisa nchi na kumaliza katika nafasi nne za juu katika msimamo.
Lakini ikiwa kinyume, hizi shangwe na mbwembwe ambazo tunaziona sasa hivi zitapotea na itabakia kuwa historia kwa upande wao.