Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mashine mpya zaanza na mabao Azam FC

Nyota Mpaya Azam Mashine mpya zaanza na mabao Azam FC

Sun, 16 Jul 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Beki Cheikh Sidibe na mshambuliaji Alassane Diao wameanza na mguu mzuri katika kikosi cha Azam FC baada ya kila mmoja kufunga bao katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Al Hilal ya Sudan uliochezwa juzi, katika Uwanja wa Rades, Tunis huko Tunisia walioibuka na ushindi wa mabao 3-0.

Huo ulikuwa ni mchezo wa kwanza kwa wawili hao tangu wajiunge na Aza FC wakitokea timu za Teungueth na US Goree za Senegal huku bao lingine likipachikwa na Prince Dube.

Sidibe anayecheza nafasi ya beki wa kushoto, alitangulia kuifungia Azam FC bao la kwanza katika kipindi cha kwanza akiunganisha kwa kichwa krosi ya Feisal Salum na baadaye kwenye kipindi cha Pili, Dube alipachjika bao la pili kabla ya Diao kumalizia la tatu.

Kuanza vyema kwa nyota hao pamoja na kiwango bora ambacho timu yake imekionyesha, kimefanya kocha wa Azam FC, Youssouph Dabo kuwa na matumaini ya kufanya vizuri msimu ujao.

"Kama nilivyosema mwanzoni tuna wachezaji wazuri sana wanaocheza kiufundi lakini changamoto kwao ni kwenye suala nzima la mbinu hivyo michezo hii tunayoendelea nayo na timu kubwa tunazocheza nazo inatupa nafasi ya kufanyia kazi," alisema Dabo aliyetua pia kutoka Senegal.

Kocha huyo aliongeza amefurahishwa na kiwango cha uchezaji cha mastaa wapya walioingia kikosini humo katika dirisha hili la usajili huku akiwataka kutobweteka kwani safari bado ni ndefu kwao na watambue wamebeba dhamana kubwa kwa mashabiki.

Katika dirisha la usajili linaloendelea, Azam FC tayari imeshafanya usajili wa wachezaji wanne wapya ambao ni Sidibe, Feisal, Diao pamoja na Djibril Silla.

Kikosi hicho kinaendelea na kambi ya wiki tatu kisha kitarejea nchini na mchezo wake wa kwanza utakuwa ni nusu fainali ya Ngao ya Jamii dhidi ya mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara Yanga utakaopigwa Agosti 9, kwenye Uwanja wa Mkwakwani.

Azam itaingia katika mchezo huo ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza dhidi ya Yanga kwani mara ya mwisho ilipoteza bao 1-0 kwenye fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) iliyopigwa Juni 12, kwenye Uwanja huo huo wa Mkwakwani mjini Tanga.

Mbali na mashindano hayo, Azam FC pia inajiandaa na mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao am,bayo itashiriki ikiwa pamoja na Singida Fountain Gate.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live