Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mashindano CAF ni fedha tu inaongea

Mashindano CAF Fedha Mashindano CAF ni fedha tu inaongea

Mon, 23 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (Caf) lilifanya uzinduzi rasmi wa mashindano ya African Football League (AFL), tukio ambalo lilifanyika katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kwa uwepo wa mechi baina ya Simba ya Tanzania na Al Ahly ya Misri.

Licha ya kwamba ndio yanafanyika kwa mara ya kwanza, mashindano hayo yameonekana kuteka hisia za wadau wengi wa mpira wa miguu barani Afrika hasa kutokana na zawadi za fedha ambazo zinatolewa kwa timu shiriki na zile zinazofanya vyema kwa kusogea hatua za juu za mashindano hayo.

Kwa mujibu wa Caf, bingwa wa mashindano hayo anapata kiasi cha Dola 4 milioni (Sh 10 bilioni) huku mshindi wa pili akipata kiasi cha Dola 3 milioni (Sh 7.5 bilioni), timu inayoishia hatua ya nusu fainali inapata kiasi cha Dola 1.7 milioni (Sh 4.2 bilioni) na timu ambayo inakomea robo fainali inapata kiasi cha Dola 1 milioni (Sh 2.5 bilioni).

Kiasi hicho cha fedha kinachotolewa kwa washindi wa AFL kinayafanya yawe mashindano ambayo yana fedha nyingi zaidi za zawadi kuliko mengine yaliyo chini ya Caf kwa ngazi ya klabu huku yakishika nafasi ya pili kwa kuwa na malipo makubwa ya fedha za zawadi kwa timu katika mashindano yote ya Caf yakiongozwa na Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon).

Mashindano ya AFL ni ishara tu ya namna ambavyo mashindano ya caf yalivyo na fedha kwa timu shiriki iwe yale ya ngazi ya taifa ya klabu na makala hii inaonyesha ni kwa namna gani timu za klabu au za taifa zinaweza kuvuna fedha kupitia baadhi ya mashindano ya Caf.

AFCON

Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) ndio mashindano yenye thamani kubwa zaidi katika soka hapa Afrika kulinganisha na mengine kutokana na kiasi kikubwa cha fedha ambacho kinalipwa kwa washindi.

Bingwa wa Afcon anavuna kiasi cha Dola 5 milioni (Sh 12.5 bilioni) huku mshindi wa pili akiondoka na kiasi cha Dola 2.75 milioni (Sh 6.9 bilioni) huku timu mbili zinazotinga hatua ya nusu fainali, kila moja ikipata kifuta jasho cha Dola 2.2 milioni (Sh 5.5 bilioni).

Lakini sio timu zilizofika hatua za juu tu za mashindano hayo ndio zinapata fedha bali hata zile zitakazoishia hatua ya makundi nazo zitapata kifuta jasho ambapo inaripotiwa kwamba kila moja inapata kiasi cha Dola 700,000 (Sh 1.8 bilioni).

CHAN

Ni mashindano ya mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani ambayo yalianzishwa rasmi mwaka 2009 ambapo bingwa wake anapata kitita cha Dola 2 milioni (Sh 5 bilioni) huku mshindi wa pili akiondoka na kitita cha Dola 1.25 milioni (Sh 3.1 bilioni).

Kwa timu ambayo inaishia hatua ya makundi, inapata kiasi cha Dola 200,000 (Sh 500 milioni).

WAFCON

Bingwa wa mashindano ya Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON) anapata zawadi ya fedha kiasi cha Dola 500,000 (Sh 1.3 bilioni) wakati mshindi wa pili anapata kiasi cha Dola 300,000 (Sh 750 milioni).

Mkaa bure sio sawa na mtembea bure kwani timu ambayo inashika mkia kwenye hatua ya mwanzoni ya mashindano hayo ambayo ni ya makundi inapata Dola 100,000 (Sh 250 milioni) na ile inayoshika nafasi ya tatu kwenye kundi inapata Dola 150,000 (Sh 375 milioni).

Ligi ya Mabingwa Afrika

Heshima na hadhi ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kiasi kikubwa inachangiwa na ukubwa wa zawadi ya fedha ambazo zimekuwa zikitolewa kuanzia hatua ya makundi hadi ile ya fainali.

Kitendo cha kutinga tu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kinaihakikishia timu kiasi cha Dola 700,000 (Sh 1.8 bilioni) na ile inayoingia hatua ya robo fainali inavuna Dola 900,000 (Sh 2.3 bilioni).

Bingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika anapata kiasi cha Dola 4 milioni (Sh 10 bilioni) na mshindi wa pili anapata kitita cha Dola 2 milioni (Sh 5 bilioni).

Kombe la Shirikisho Afrika

Msimu uliopita, Yanga iliitoa kimasomaso Tanzania kwa kutinga hatua ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika ambayo ilipoteza mbele ya USM Alger na kwa kufika hatua hiyo ikapata kiasi cha Dola 1 milioni (Sh 2.5 bilioni) wakati waliotwaa ubingwa walipata Dola 2 milioni (Sh 5 bilioni).

Timu inayoishia hatua ya makundi ya mashindano hayo inapata kifuta jasho cha Dola 400,000 (Sh 1 bilioni).

Taji la Super Cup

Super Cup ni shindano linaloshirikisha bingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika na bingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika na mshindi anapata kiasi cha Dola 500,000 (Sh 1.3 bilioni) na ile inayopoteza mechi inapata Dola 250,000 (Sh 625 milioni).

Klabu Bingwa Afrika Wanawake

Bingwa wa taji la Kombe la Klabu Bingwa Afrika kwa wanawake anapata kiasi cha Dola 400,000 (Sh 1 bilioni) na mshindi wa pili anapata Dola 250,000 (Sh 625 milioni).

Kwa timu ambayo inaishia hatua ya makundi ya mashindano hayo, inapata kiasi cha Dola 100,00 (Sh 250 milioni).

Chanzo: Mwanaspoti