Ligi Kuu ya England imeziambia klabu zake 20 kurejea katika kanuni za kujikinga na kuzingatia sheria mpya za Corona.
Sheria hizo ni pamoja na umbali wa kijamii, zilizoletwa mwanzoni mwa msimu.
Klabu zilizo na viwango vya juu vya chanjo zilikuwa zimelegeza baadhi ya hatua lakini lazima sasa zirudi tena katika vizuizi ili kusaidia kupunguza kuenea kwa kirusi kipya cha Omicron.
Mechi ya Ligi Kuu ya Tottenham dhidi ya Brighton iliyokuwa ichezwe kesho imeahirishwa kufuatia wachezaji wa Spurs kukutwa na Corona.
Wachezaji kadhaa wa Leicester hawakusafiri kwenda Italia kwa ajili ya mechi yao ya makundi ya ligi ya Europa dhidi ya Napoli Alhamisi iliyopita kwa sababu ya kukutwa na Corona.
Ligi Kuu haijasema ni klabu ngapi zimeweza kulegeza hatua hizo.
Itifaki pia ni pamoja na kuvaa barakoa katika maeneo ya ndani, tiba haichukui zaidi ya dakika 15 na wafanyakazi wa matibabu
wanaohitajika kuvaa vikinga mwili wote wakati wa kuwahudumia wachezaji.
Mechi ya Ligi ya Europa kati ya Spurs dhidi ya Rennes Alhamisi pia iliahirishwa baada ya wachezaji wanane na wafanyakazi watano kupimwa na kukutwa na Corona katika klabu hiyo ya London.
Spurs walilazimika kufunga kituo chao cha timu ya kwanza cha mazoezi Jumatano.
Waziri Mkuu Boris Johnson alitangaza serikali inaanzisha ‘mpango B’ wa kupambana na kuenea kwa Omicron Jumatano.