Mashabiki wa Manchester United wamemwambia winga wa Kibrazili Antony amjibu Kocha Erik ten Hag kama alivyofanya Jadon Sancho baada ya Mdachi huyo kumshambulia hadharani.
Kocha wa Man United, Ten Hag aliulizwa kuhusu majukumu ya Antony kwenye kikosi kama atacheza mechi na jana Jumanne ilitarajia kukipiga na Barnsley na kabla ya mechi hiyo, alikuwa amecheza dakika moja tu msimu huu.
Ten Hag alisema Antony ana haki ya kucheza, lakini itapotea kama hafanyi vizuri mazoezini - kama vile alivyofanya kwa Sancho mwaka jana.
Ten Hag alisema: "Tunafanya mazoezi kila siku na mchezaji anapaswa kupambana kupata haki ya kucheza. Wachezaji wanapofanya vizuri mazoezini, ari zao zikiwa nzuri na kuonyesha viwango bora mazoezini, wanakuwa na haki ya kucheza."
Mashabiki sasa wamesema maneno hayo yanalingana kabisa na yale ambayo Ten Hag aliwahi kumsema Sancho hadharani msimu uliopita, alipokosoa upambanaji wa winga huyo mazoezini kuwa hafifu na ndiyo maana hakucheza mechi dhidi ya Arsenal.
Sancho alimjibu Kocha Ten Hag na kusema ni muongo, huku akidai alichokuwa akifanya ni kumtoa tu kafara. Ten Hag akaamua kumwadhibu Sancho kwa kumwondoa kwenye kikosi chake cha kwanza kabla ya kumpeleka kwa mkopo Borussia Dortmund.
Sasa jambo hilo linamtokea Antony, kitu kinachowafanya mashabiki kumtaka Mbrazili huyo amjibu Ten Hag bila ya kujali ni kitu gani kinaweza kumtokea winga huyo.
Shabiki wa kwanza alisema: "Kaka Antony. Binafsi nisingekubali, lazima ujitetea mwenyewe. Nakushauri ujibu kuonyesha vile unavyojifikiria."
Shabiki mwingine aliongeza: "Mimi ninafsi ningetoa taarifa ya kupinga hiyo kitu, lakini hiyo kama ningekuwa mimi."
Shabiki wa tatu aliandika: "Sancho angejibu haraka kwa maneno marefu hadi kufikia wakati huu."
Shabiki wa nne alisema: "Tunamsubiri Antony aposti kitu kwenye mtandao wa kijamii."
MASTAA WANAOLIPWA MISHAHARA MIKUBWA MAN UNITED NI HAWA
1.Casemiro, Pauni 375,000 kwa wiki
2.Bruno Fernandes, Pauni 325,000 kwa wiki
3.Marcus Rashford, Pauni 325,000 kwa wiki
4.Mason Mount, Pauni 250,000 kwa wiki
5.Antony, Pauni 200,000 kwa wiki