Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ Hanour Janza, amehimiza umoja na Mshikamano kwa Mashabiki wa soka la Bongo ili kuiwezesha timu hiyo kuwa na morari kuelekea mchezo dhidi ya Uganda.
Taifa Stars itacheza mchezo wa Mkondo wa pili wa kuwania kufuzu Fainali za Mataifa Bingwa Barani Afrika ‘CHAN’ jijini Kampala keshokutwa Jumamosi (Septemba 03), baada ya kupoteza nyumbani kwa kufungwa 1-0.
Kocha Janza amesema licha ya kuumizwa na matokeo yaliyopita, Watanzania wanapaswa kuwa kitu kimoja na kuipa ushirikiano timu yao ya Taifa, ambayo ina jukumu zito ugenini.
Amesema wachezaji waliopo kikosini wana sifa zote za kupata matokeo baada ya kufanya nao mazoezi kwa siku kadhaa tangu alipotangazwa kuwa Kocha Mkuu, hivyo anaamini bado mchezo dhidi ya Uganda upo wazi, na yoyote anaweza kupata tiketi ya kufuzu CHAN.
“Tuna wachezaji ambao wanaweza kutupa matokeo, tukianza kupata bao moja litabadilisha hali ya mchezo mzima, hivyo ni lazima tucheze kwa kujiamini ila lengo kubwa ni kushambulia na kutengeneza nafasi nyingi.”
“Matokeo ya mchezo wa kwanza yalimuumiza kila sahabiki, lakini hayo yamepita na sasa tunaangalia mbele, kikubwa ni kwa kila mtanzania kuendelea kutupa ushirikiano, kwani kufanya hivyo itawaongezea nguvu wachezaji ambao wana kazi ya kwenda kupambana ugenini,” amesema Janza
Taifa Stars itatakiwa kusaka ushindi wa zaidi ya bao moja dhidi ya Uganda, ili kukata tiketi ya kushiriki Fainali za Mataifa Bingwa Barani Afrika ‘CHAN’ zitakazounguruma nchini Algeria mwaka 2023.