Mpira wa kisasa umebadilika vitu vingi. Zamani wachezaji walikuwa wanacheza kwa namba uwanjani. Siku hizi sio hivyo. Ni mwendo wa kupewa majukumu. Ndiyo maana unaweza kuona mabeki watatu wote wa kati wakianza katika mechi.
Ndiyo maana unaweza kuona kiungo mshambuliaji akiwa kama straika pale mbele. Ndiyo ilivyopia kwenye vikosi. Zamani timu ilikuwa inapambana kupata kikosi cha kwanza bora, lakini siku hizi zinapambana kupata kikosi kipana.
Sio kikosi cha kwanza ni kuwa na kikosi kipana. Unapataje kikosi kipana? Ni mambo mawili tu makubwa. Kwanza ni kusajili wachezaji walau wawili kila nafasi uwanjani na kuwatumia kwa uwiano unaokaribiana.
Ukishakuwa na walau wachezaji wawili kwenye kila nafasi ambao uwezo wao haupishani sana kinachofuata ni kutengeneza uwiano mzuri wa wote kucheza. Mmoja anaweza kupata dakika nyingi kuliko mwingine, lakini lazima wote wapate. Je, ni kweli mashabiki wa Yanga wanaijua timu kuliko Kocha Miguel Gamondi? Jibu litakuwa ni hapana.
Mchezo wa soka unachezwa hadharani. Kila mtu anaona. Halafu mashabiki wa siku hizi pia sio kama wale wa zamani. Wanapata nafasi ya kuiona timu yao kila siku. Wanapata pia nafasi ya kuona timu za watu wengine. Wanajifunza kila siku. Uelewa unaongezeka.
Ukiona wanapiga kelele Juu ya jambo fulani, wasikilizwe. Mashabiki wa Yanga wamekuwa wakipiga sana kelele juu ya kocha wao kutumia kikosi kidogo cha timu yake tu ya kwanza. Siku chache kabla ya mechi na Mtibwa Sugar kocha alilitolea ufafanuzi jambo hilo lakini hakukuwa na uhalisia.
Nadhani kocha alitafakari na kuamua kufuata maoni na mtazamo wa mashabiki mechi dhidi ya Mtibwa Sugar. Pamoja na maingizo mengi ya wachezaji Yanga ilikuwa bora sana uwanjani. Pamoja na kutoa burudani, Yanga walitoa pia kichapo kikubwa.
Je, ni kweli mashabiki wanaijuia sana timu yao kuliko Gamondi? Jibu ni hapana lakini kuna muda wana hoja. Wasikilizwe Wasipuuzwe. Gamondi ni kocha mzuri sana lakini amekuwa mzito wa kutumia wachezaji wengi kwenye mashindano tofauti.
Utakuta hata kwenye Kombe la Mapinduzi kikosi cha kwanza anataka kuanza na Maxi Nzengeli. Ukute hata mechi za awali za Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) anataka kuanza na Pacome Zouzou. Huyo ndiyo Gamondi. Ni kweli wachezaji hawawezi kucheza kwa dakika sawa lakini kuwapa walau wengine dakika chache kila mechi inasaidia.
Mchezaji anaongezeka kiwango cha kucheza. Kucheza kwa Sure Boy dhidi ya Mtibwa Sugar kunamjenga mchezaji. Hata siku ukipata majeraha kwa mchezaji wako wa kwanza akija chaguo la pili anakuwa na ubora unaokaribiana. Hivi ndivyo inavyopaswa kuwa. Angalia matumizi ya Kennedy Musonda na Clement Mzize.
Wote wanacheza. Wote wana furaha. Yeyote atakayeanza unajua kabisa baadaye lazima mwingine atakuja. Angalia matumizi ya Dickson Job, Ibrahim Bacca na Bakari Mwamnyeto, wote wanacheza. Hii ndiyo njia sahihi ya kuwafanya wachezaji wako kuwa fiti.
Nadhani mashabiki walikuwa sawa sana kumlalamilia kocha wao. Nadhani pia kocha amekuwa msikivu na kufanyia kazi maoni yao. Mashabiki hawawezi kuwa na uwezo wa kocha, lakini kuna muda wanatoa hoja zenye mashiko. Wasikilizwe. Wasipuuzwe. Bila kelele za mashabiki huenda hata mechi dhidi ya Mtibwa Sugar mziki ungekuwa uleule uliocheza na Al Ahly.
Baada ya muda mrefu hatimaye nikamuona Farid Mussa uwanjani. Farid ni miongoni mwa wachezaji wachache ambao kila siku nawaona kama hawajatumika. Ni mchezaji mpya kila siku.
Bado ana uwezo wa kucheza kikosi cha kwanza kwenye timu yoyote hapa nchini. Kupata mchezaji anayeweza kucheza nafasi zaidi ya nne na akakupa ubora uleule sio jambo dogo. Farid anaweza kazi hiyo. Kama kocha taratibu ataanza kumpa nafasi kuna siku jina lake litaimbwa tena.
Yule Sure Boy sio wa mchezaji wa kukaa benchi kila siku. Anahitaji walau dakika 30 tu kila mechi. Ni moja kati ya viungo wachache nchini wenye uwezo wa kukaa na mpira. Miguu yake ni kama ina gundi. Mpira unamtii. Nimependa sana namna kocha alivyofanya mechi dhidi ya Mtibwa Sugar.
Ni Mwendo wa kutengeneza kikosi kipana sio kikosi cha kwanza. Kuna siku timu itamkosa Khalid Aucho watu wataanza kutafutana. Mfano nimeona mechi zote za kimataifa msimu huu Nzengeli hajawa kwenye moto mkubwa kama alivyo kwenye mechi za ndani. Lakini bado ameendelea kucheza kwa dakika zote 90.
Ni mchezaji mzuri na mkubwa lakini kuna siku mechi inakataa. Hata kina Cristiano Ronaldo na Lionel Messi kuna siku gemu inawakataa wanatolewa. Mabadiliko aliyofanya Gamondi dhidi ya Mtibwa Sugar yana afya sana kwa timu.
Yanga wameshinda mabao matano karibu mechi tatu kwenye mashindano yote msimu huu, lakini manne dhidi ya Mtibwa ilikuwa ni habari nyingine. Mabao yanayovutia kutoka kwa wachezaji tofauti. Hivi ndivyo timu kubwa inapaswa kuwa. Kocha anajua zaidi kuliko mtu yeyote lakini kusikiliza maoni ya mashabiki nalo ni jambo jema.
Umemuona Stephen Aziz KI? Nadhani amezaliwa upya. Huu ndiyo msimu anaoonyesha sababu halisi za msimu jana kutambulishwa saa tisa slfajiri. Ni mchezaji anayeonyesha rangi zake halisi msimu huu.
Ndiye kinara wa mabao Tanzania. Ndiye mchezaji mwenye furaha zaidi pengine pale Jangwani. Hata afunge bao mchezaji yeyote, utamuona anakuwa wa kwanza kwenda kushangilia naye. Kama atakuwa fiti msimu mzima tunaweza kuona mabao mengi sana kutoka kwake.
Hawa ndiyo aina ya wachezaji wa kigeni tunaowahitaji nchini. Wachezaji wa Kigeni wanahitaji kuleta kitu cha tofauti nchini. Tunahitaji wachezaji wa kigeni wanaoleta utofauti na kuongeza thamani ya ligi yetu. Nadhani huu ni msimu wake.
Ni muda wake wa kutengeneza heshima. Msimu uliopita Aziz KI alipigiwa kelele sana na mashabiki na kuna wakati alilazimika kuanzia benchi lakini sio msimu huu. Mabao tisa ya Ligi Kuu, mchango mkubwa kimataifa sioni wa kumzuia. Aziz KI anaonyesha thamani halisi ya pesa. Mashabiki sio makocha lakini wanaweza kuona tatizo.
Wanaweza kuelezea tatizo. Wasipuuzwe. Wasikilizwe. Leo ni siku ya mechi kubwa kwa Yanga. Safari ya kuelekea robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika inaanza na ushindi wa mechi dhidi ya Medeama. Bila shaka yoyote kocha Gamondi atafanya tena mabadiliko ya kikosi cha kwanza kidogo ili kwenda kuzisaka alama tatu kwa Mkapa. Kila la heri Wananchi.