Swahiba wangu, Mmakonde mwenzangu, Ahmed Ally siku chache zilizopita nimemsikia akilalamika kuwa mashabiki wa Simba wameizomea timu hiyo wakati ilipokuwa safarini kutoka Mtwara kuja Dar es Salaam, Jumatatu iliyopita.
Mashabiki hao wa Simba wameonekana kutofurahishwa na kichapo cha mabao 2-1 ambacho timu yao ilikipata kutoka kwa Azam FC, Jumapili iliyopita katika mechi ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC), iliyochezwa kwenye Uwanja wa Nangwanda, Mtwara.
Ni matokeo ambayo yameifanya Simba itupwe nje katika mashindano hayo lakini pia kuifanya imalize bila kutwaa taji lolote msimu huu, jambo ambalo linatokea kwa mara ya pili mfululizo.
Baada ya kuzomewa huko, Ahmed Ally kawataka mashabiki wasifanye hivyo kwa vile yeye, viongozi, benchi la ufundi pamoja na wachezaji wanaumizwa na kitendo hicho.
Malalamiko ya Ahmed Ally ni jambo lililotushangaza kidogo hapa kijiweni na kiukweli sikutegemea kwa mtu kama yeye ambaye anaujua vyema mpira, ni kocha na mwandishi wa habari kitaaluma ayatoe.
Mashabiki wa Simba kwa kuizomea timu yao, wanahitaji pongezi na sio lawama kwa vile wametimiza moja kati ya wajibu wao wa msingi kwani mwingine ni kushangilia. Tayari wameshaishangilia timu msimu mzima na hadi kwenye nusu fainali kule Mtwara ikashindwa kuwapatia taji, kilichobakia kilikuwa ni hicho cha kuzomea ambacho wamekifanya japo naona haitoshi wangezomea zaidi.
Wanapozomea kuna jumbe wanazotaka kuzifikisha kwa wachezaji, viongozi na benchi la ufundi.
Kwa wachezaji wanataka kuwakumbusha kuwa wao mashabiki wanahitaji kuona wanavuja jasho kwa ajili ya timu ili ipate ushindi na sio kutolewa kiume.
Kwa benchi la ufundi, ujumbe ambao wanataka ulifikie ni kwamba mashabiki bado hawajaridhika na kiwango cha timu na cha mchezaji mmojammoja.
Viongozi wanafikishiwa ujumbe kuwa wanahitajika kuhakikisha timu inasajili kikosi imara na bora kitakachowapa uhakika wa kupata matokeo mazuri. Sio kuwasajilia mchezaji ambaye hajacheza mpira kwa miaka miwili mfululizo.
Hivyo naunga mkono mashabiki wa Simba walioizomea timu. Wametimiza wajibu wao na kama inawezekana namba ya wanaozomea iongezeke zaidi ili yasijirudie msimu ujao.