Kutokana na mashabiki kukosa taarifa za kutosha katika kile kinachojadiliwa kati ya mwamuzi wa kati na maofisa wa video saidizi kwa waamuzi, Bodi ya Kimataifa ya Chama cha Soka (IFAB) inayohusika na sheria za kandanda imependekeza utaratibu wa kuwepo kwa mawasiliano kwenye viwanja ili mashabiki wajue kinachojadiliwa kabla ya maamuzi.
Kumekuwa na sintofahamu kwa mashabiki kila ambapo tukio linatokea kisha mwamuzi pekee ndiye anakuwa na uwezo wa kusikia, sasa kama mapendekezo haya yataungwa mkono yataanza kutumika.
Mashindano ambayo IFAB wanakusudia yafanyike majaribio ya kutoa nafasi kwa watazamaji viwanjani kusikia kinachozungumzwa ni michuano ya Kombe la Dunia ngazi ya klabu Morocco kuanzia Februari 1-11.
Endapo kutakuwa na mafanikio kwenye majaribio ya awali, mawasiliano viwanjani yataanza kufanyika hata kwenye viwanja vingine.
Lugha ambayo itakuwa inazungumzwa Morocco bado haijaamuliwa lakini kiingereza, kifaransa na kiarabu huenda mojawapo itatumika.
“Tunadhani mashabiki zetu hawapati taarifa za kutosha juu ya sababu fulani inayochukuliwa na refarii kutokana na maelekezo ya maofisa wa VAR”, alisema Mark Bullingham, mtendaji mkuu wa FA.