Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mashabiki Yanga waachwa ‘solemba’

Fd4d126b6f7612cea5360c0e92b0940a Mashabiki Yanga waachwa ‘solemba’

Fri, 28 Aug 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MAMIA ya mashabiki wa soka wa Yanga wamejikuta katika wakati mgumu, baada ya kutowasili kwa mchezaji waliokwenda kumpokea kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam jana.

Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela, juzi aliwataka mashabiki wa timu hiyo jana kujitokeza kwa wingi kwenye uwanja huo kumpokea mchezaji wa Burkina Faso, Sogne Yacouba, anayekuja kujiunga na klabu hiyo lakini hakutokea.

Mashabiki waliitikia wito huo wa Mwakalebela kama walivyofanya kwa wachezaji wengine wa kigeni wa timu hiyo walipowasili uwanjani hapo na kukutana na mashabiki lukiki ambao waliondoka kwa maandamano hadi makao makuu ya klabu hiyo yaliyopo mitaa ya Twiga na Jangwani.

Wakiwa katika makundi makundi nje ya kiwanja hicho jana, mashabiki hao walionekana kulalamika, huku wakiwataka viongozi wa klabu hiyo kijitokeza na kuwatangazia kilichokuwa kikiendelea.

Hata hivyo, hakukuwa na kiongozi yeyote wa Yanga na kuwafanya mashabiki hao kuzidi kuwa wakali na wengine wakifoka kuwa wamepoteza muda wao na viongozi hawawajali.

Mbali na Mwakalebela kuwataka mashabiki kujitokeza kwa wingi kumlaki mchezaji huyo, Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli, naye alisisitiza kuwa mchezaji huyo alitarajiwa kuja nchini jana mchana na kuwataka mashabiki kuendeleza utamaduni wao wa kujitokeza kwa wingi kumpokea.

“Kesho (jana) mchezaji wetu tuliyemsajili kutoka Burkina Faso, Yacouba atawasili kwenye uwanja wa ndege, mashabiki wetu kama ilivyokuwa kawaida wajitokeze kwa wingi majira ya mchana tutakuwa na jambo letu,” alisema Mwakalebela.

Mashabiki hao walionekana kutomuamini mtu aliyejitokeza kiwanjani hapo kutoa taarifa kuwa mchezaji huyo hatawasili tena na hakusema atakuja lini.

Mashabiki hao walionekana kuwa na msimamo wakiamini taarifa ya kutokuja kwa mchezaji huyo inapikwa na watu wasioitakia mema Yanga na kutaka taarifa zitolewe na viongozi kama mchezaji huyo hatafika kama ilivyoelezwa.

Mkurugenzi wa Uwekezaji wa Kampuni ya GSM, Injinia Hersi Said, anayesimamia usajili wa wachezaji katika klabu hiyo alipoulizwa jana kuhusu ujio wa mchezaji huyo, alisema kama atakuja watatoa taarifa.

“Hakuna taarifa za kuja mchezaji mpya, kwanza nashangaa nani amewaambia, ratiba ya kuja mchezaji mpya tuliyemsajili itatangazwa na mashabiki watatangaziwa na watajitokeza kama ilivyofanya kwa nyota wengine tuliokwisha wasajili,” alisema Said.

Yanga ambayo hadi sasa imesajili nyota wa nne wa kimataifa akiwemo Tuisila Kisinda, Tunombe Mukoko kutoka DR Congo, Michael Sarpong wa Ghana na Carlos Fernandes 'Carlinhos’ kutoka Angola, ambao wote walipata mapokezi makubwa kutoka kwa mashabiki hao.

Chanzo: habarileo.co.tz