Mashabiki wa Chelsea wamemwomba Mauricio Pochettino aende kumaliza manyanyaso wanayokutana nayo baada ya bao la kujifunga la staa wao kuweka kwenye wakati mgumu kwenye mechi ya Ligi Kuu England dhidi ya Brentford usiku wa juzi Jumatano.
Chelsea ilikuwa nyuma kwenye dakika 37 tu baada ya mpira wa kona ya Brentford kumbabatiza mchezaji Cesar Azpilicueta na kutinga nyavuni. Chelsea ilikumbana na kipigo cha tano mfululizo tangu timu hiyo ilikabidhiwa kwa kocha wa muga gwiji wa klabu, Frank Lampard.
Na mashabiki waliamua kutumia kurasa zao za Twitter kuelezea namna wanavyoumizwa, huku wengine wakitania kwamba wanaweza kushuka daraja kama Pochettino hatakuwa haraka Stamford Bridge kuokoa jahazi.
Shabiki wa kwanza alisema: "Mpendwa @todd_boehly, mlete Pochettino sasa hivi, sio baadaye. Tunataabika sana, huu sio utani tena, ni ukatili mkubwa. Hatuwezi kuendelea zaidi ya hapa, inaumiza. Wako, mashabiki wote wa Chelsea."
Shabiki mwingine alisema: "Washambuliaji sita kwenye benchi, mmoja uwanjani. Ukweli, aje tu Poch sasa hivi. Ukweli ni upuuzi mkubwa ukitazama kikosi kinachoanza na waliopo benchi. Kwenye benchi kumejaa wachezaji wengi wa kuuzwa. Hii hapana kwakweli."
Mwingine alisema: "Hivi tunaweza kushuka daraja ee?" Akajibiwa na mwingine: "Tunashuka daraja." Mambo yalikuwa mabaya zaidi kwa Chelsea baada ya Bryan Mbeumo kuifungia Brentford bao la pili kwenye dakika ya 78 na kumfanya Lampard kupoteza mechi zote tano mfululizo alizoiongoza timu hiyo aliporejeshwa kwenye benchi la ufundi kama kocha wa muda.
Chelsea kwa sasa inashika nafasi ya 11 kwenye msimamo wa ligi baada ya kucheza mechi 32, ikishinda 10, sare tisa na vichapo 13, huku ikiwa imefunga mabao 30 na kufungwa 35 na kukusanya pointi 39.