Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mashabiki Arsenal, Man United wote wamkataa refa wa mchezo wao Jumapili

Anthony Taylor Denied Mwamuzi Anthony Taylor

Thu, 19 Jan 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Mwamba huyu hapa. Anthony Taylor amethibitishwa kuwa ndiye atakayeshika filimbi kuchezesha kipute chenye hadhi ya ubingwa wakati Manchester United itakapowafuata Arsenal uwanjani Emirates, Jumapili hii.

Wakati mwamuzi huyo mahiri akipewa mechi hiyo kubwa, jambo limeibuka kwa mashabiki wa timu hiyo kila upande ukidhani kwamba atatibua mipango yao kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu.

Na baadhi ya mashabiki wa Man United walitumia kurasa zao wa mitandao ya kijamii kuzungumzia suala la mwamuzi huyo kupewa majukumu ya kuchezesha mechi yao dhidi ya Arsenal ugenini kwenye Uwanja wa Emirates.

Taylor, 44, anahesabika kama mmoja wa waamuzi wa hadhi kubwa kabisa kwenye Ligi Kuu England na alichaguliwa kuchezesha mechi kwenye fainali za Kombe la Dunia 2022 zilizofanyika Qatar.

Man United imekuwa kwenye kiwango bora kwa siku za karibuni, wakipanda hadi kwenye Top Four na hivyo kujiweka pazuri kwenye mbio za ubingwa.

Ushindi kwenye mchezo huo wa Jumapili dhidi ya Arsenal, unaweza kuwafanya Man United kupunguza pengo la pointi na kufikia tatu kama watakuwa wamewachapa Crystal Palace katika mchezo wa jana Jumatano usiku.

Lakini, baadhi ya mashabiki wa Man United wanadhani Taylor atatibua mipango yao ya kupata ushindi kwenye mchezo huo wa Arsenal.

Shabiki mmoja aliandika: "UshindI ni mzuri sasa, lakini umefika mwisho."

Shabiki wa pili aliandika kwa hasira: "Kutakuwa na wachezaji 12 uwanjani."

Wakati shabiki wa tatu aliandika: "Penalti kwa Arsenal."

Na shabiki mwingine wanne aliandika: "Ah mwendo wetu wa kugawa vichapo unafika mwisho."

Kwa msimu huu, Taylor amechezesha mechi mbili za Man United, ile ya kichapo cha mabao 3-1 kutoka kwa Aston Villa na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Nottingham Forest. Na kile kichapo cha Aston Villa ndicho kinachowafanya mashabiki wa Man United wamtazame Taylor kama kikwazo kwao.

Aston Villa ilikuwa mbele kwa mabao 2-0 kupitia mkwaju wa faulo wa Lucas Digne. Katika mchezo huo, mwamuzi Taylor alirudisha nyuma sana ukuta wa wachezaji wa Man United waliokuwa wanazuia wakati wa upigaji wa friikiki hiyo, ambapo ilionekana refa amekosea baada ya kuamrisha ukuta ujipande umbali unaozidi yadi 10 kutoka mpira ulipo.

Kampuni inayosimamia waamuzi wa Ligi Kuu England, PGMOL baadaye ilitoa taarifa ya kukiri Taylor alifanya makosa katika mechi hiyo kwa namna alivyopanga ukuta wa Man United, kwamba ulikuwa mbali zaidi ya yadi 10.

Mechi hiyo iliyopigwa Novemba 6 mwaka jana, ndiyo kipigo ilichokuwa imepata Man United kwenye ligi kwa siku za karibuni, kabla ya mchezo wa jana usiku.

Ukiweka kando wasiwasi wa mashabiki wa Man United juu ya mwamuzi Taylor, upande wa Arsenal, mashabiki nao wametia shaka juu ya refa huyo.

Shabiki mmija aliandika: "Huyu refa anazipendelea Man United na Man City."

Shabiki wa pili aliongeza: "Ukweli, hakuna refa atachaguliwa na kutupa sisi unafuu. Wote ni majanga tu."

Shabiki wa tatu alikwenda kinyume cha kauli za wengine, aliposema: "Tbh amekuwa mzuri kwenye mechi zetu za msimu huu."

Kwenye Ligi Kuu England, Arsenal na Man United zimekutana mara 61, mechi 18 zilimalizika kwa sare, wakati 17 zilikuwa za ushindi wa Arsenal na 26 ilishinda Man United. Katika mechi 17 ilizoshinda Arsenal, 13 kwenye uwanja wake wa nyumbani na mara nne tu ugenini, wakati Man United imeshinda nyumbani mara 18 na ugenini mara tisa.

Kwa takwimu hizo, hiyo inamaana, Arsenal wanarekodi nzuri nyumbani, wakishinda 13, lakini Man United nao wapo vizuri wanapokwenda kuwakabili Arsenal kwao, wamepata ushindi mara nane.

Waamuzi wa mechi tano zilizopita

Arsenal vs Man United kwenye ligi kuu England

-Man United 3-1 Arsenal - Refa Paul Tierney

-Arsenal 3-1 Man United - Refa Craig Pawson

-Man United 3-2 Arsenal - Refa Martin Atkinson

-Arsenal 0-0 Man United - Refa Michael Oliver

-Man United 0-1 Arsenal - Refa Mike Dean

Chanzo: Mwanaspoti