Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Masenga: Freddy anajua sema basi tu!

Cvx Masenga: Freddy anajua sema basi tu!

Sun, 17 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Unapoizungumzia Tanzania Prisons (Wajelajela) huwezi kuacha kumtaja Jamal Masenga kwa kuwa ni mmoja kati ya wachezaji nguzo kwenye nafasi ya ulinzi ya timu hiyo.

Jamaa alizaliwa Novemba 20, 2001 na ni mtoto aliyekulia kwenye familia ya soka ambapo elimu ya msingi aliipata katika shule ya Msamvu B, mjini Morogoro huku ile ya sekondari akiipata Kawenzi.

Leo ni miongoni mwa wachezaji tegemezo kutoka Tanzania Prisons kwa kuwa timu hiyo kwa sasa ni miongoni mwa zinazoogopwa kwenye ligi kutokana na staili ya uchezaji wake.

Mchezaji huyo amefanya mazungumzo maalumu na gazeti hili ambapo amezungumza mengi kuhusiana na historia yake kwenye soka.

KUANZA SOKA

Jamal anasimulia kwamba, alianza kucheza soka kwenye kituo cha Moro Kids wakati anasoma kuanzia ngazi ya shule ya msingi akifanikiwa kucheza mashindano ya Umitashumta na Umisseta, ambapo baada ya kufanya vizuri alichaguliwa kujiunga na timu ya taifa U-15, U-17 na baada ya hapo alichaguliwa kujiunga na Mtibwa Sugar alikocheza misimu mitatu timu kubwa, lakini baadaye alipata majeraha ambayo yalisababisha apate wakati mgumu.

AONDOKA MTIBWA

Anasema majeraha ndiyo yalimuondoka Mtibwa.

“Kutokana na majeraha niliyokuwa nayo kwa muda mrefu, uongozi wa Mtibwa Sugar wakati huo walihisi sitapona kutokana na majibu waliyokuwa wanapewa na madaktari. Nilijaribu kumsihi kocha wetu wa wakati huo anibakizie nafasi kwenye usajili akakataa, badala yake akasema wanipeleke kwa mkopo timu yoyote,” anasema.

ATUA PRISONS, APATA ZALI LA JESHI

Jamali anasema mguu aliotua nao Prisons ulikuwa na bahati kwani alionyesha kipaji chake.

“Baada ya kucheza play off (mchujo) kati ya Mtibwa Sugar na Prisons, Oktoba 8, 2023 - Prisons wakanitafuta. Kwa kuwa bado nilikuwa nina mkataba na Mtibwa, uongozi wa Prisons nikawaambia wawafuate viongozi wa Mtibwa. Nikafanikiwa kutolewa kwa mkopo kwenda Prisons mwaka huohuo nikapata nafasi ya kujiunga na Jeshi la Magereza nikajiriwa mpaka leo,” ALISEMA.

FAMILIA YA SOKA

Mchezaji huyo anasema anatoka katika famili ya soka na hapa anasema, “familia yangu ni watu wa soka kwa kuwa baba mzazi mzee Idd Masanga alikuwa mcheza soka, tena nafasi ya kipa. Nakumbuka aliwahi kucheza Ushirika Moshi. Baba yangu mkubwa Hamad Masenga alicheza Reli Morogoro, Coastal Union pamoja na Mtibwa Sugar.”

ANAIONAJE LIGI

Kuhusu Ligi Kuu, beki huyo anasema: “Ligi ya Tanzania kwa sasa ni ngumu na imekuwa na ushindani mkubwa. Naweza kusema tangu nianze kucheza soka huu ndio msimu ambao nimeona ligi ikiwa na timu imara. Hakuna timu ndogo kama zamani, kiufupi ligi imepiga hatua.”

MECHI NA SIMBA

Hivi majuzi Prisons waliichapa Simba mabao 2-0 katika Ligi Kuu mjini Morogoro, lakini Jamal anasema walijipanga kwelikweli kumkabili Mnyama. “Ni kweli Simba tuliwafunga, na ilikuwa mechi nzuri lakini tulifanya maandalizi mazuri. Kocha na wachezaji binafsi walijiandaa vilivyo, na kile tulichojipanga nacho tukafanikiwa. Sio kwamba tulijituma sana kupita mechi zingine ila sisi tulifanya tulichotumwa na kocha, lakini ilikuwa mechi ngumu licha ya kwamba tulishinda.”

UGUMU KUMKABA FREDDY

Pamoja na mambo mengi, mchezaji huyo anamzungumzia straika mpya wa Simba, Freddy Michael kwamba ni mtu kwelikweli uwanjani na kumkaba lazima ujipange.

“Kwanza ni mshambuliaji mzuri, kwani ana nguvu na uwezo mkubwa na ni ngumu kumkaba. Changamoto niliyoipata wakati wa kumkaba ni kuwa na nguvu na huwa hahami maeneo na ukifanya kosa anaweza kukuadhibu maana huwa hazunguki anakuwa mbele ya lango muda wote.”

“Utofauti upo maana Freddy ni mtu wa kukaa mbele ya goli na mguso wake wa mpira ni tofauti na washambuliaji wengine kwa kuwa anakaa eneo moja la goli. Washambuliaji wengine wanakuwa wanakimbia muda wote kitu ambacho Freddy hafanyi.”

MALENGO YA SOKA

Kila mtu ana malengo katika masiha, na Jamal anasema: “Malengo yangu ni kupata nafasi ya kuchezea timu ya taifa ‘Taifa Stars’ maana tangu nimechezea timu za vijana sijabahatika kuitwa tena’ hivyo nikipata nafasi hiyo nitafurahi. Malengo mengine natamani kucheza soka la kulipwa nje ya nchi na naendelea kupambana. Naamini itawezekana”

UBINGWA MSIMU HUU

Akizungumzia ubingwa wa ligi anasema hakuna timu ambayo imejihakikishia na yoyote miongoni mwa zile timu tatu za juu inaweza kutwaa ndoo.

“Ligi ni mbichi na atakayejipanga kucheza mechi zake ndiye atatwaa ubingwa.”

Pia alizungumzia ujio wa kocha mpya kikosini kwao baada ya kuondoka kwa Fred Mizniro akisema: “Kiukweli Hamad Ally kikosini ameongeza hamasa kubwa na ana mchango mkubwa katika mabadiliko ya namna timu inavyocheza kwa sasa maana anao uwezo mkubwa na muda wote tumehamasika kiukweli.”

MBANGULA KIKOSINI

Wakati timu zingine zinapowakosa washambuliaji wao hatari, Jamal anasema wao pia hutokea kwa Samson Mbangula, lakini kwa sasa timu inaundwa kupitia kwa wachezaji wote. “Timu yetu kwa sasa haipo katika mfumo wa kumtegemea mchezaji mmoja, lakini kiukweli anapokosekana mshambuliaji Mbangula tunakuwa na wakati mgumu maana tunakuwa na matarajio ya mwendelezo wa kufunga mabao hivyo ikitokea hayupo inatupa wasiwasi lakini huwa tunaamini kwenye maagizo ya kocha wetu.”

MTIBWA NA PRISONS

Akizungumzia tofauti iliyopo kati ya Mtibwa na Prisons anasema hazitofautiani sana katika suala la uchezaji, ila nje na hapo kuna tofauti flani.

“Kwenye Ligi Kuu nimecheza timu mbili tu, Mtibwa Sugar na Prisons na utofauti haupo sana... utofauti mkubwa uliopo ni kwamba viongozi wengi wa Prisons wamecheza soka na wanafuatililia mpira inavyopaswa, ila kwa kipindi nilichokuwepo Mtibwa viongozi wake walikuwa si watu wa mpira, yaani unakuta mtu kasomea kilimo ndiye anakuja kuwa kiongozi wa timu.”

MECHI MCHANA NA USHIRIKINA

Timu nyingi zinacheza mechi za jioni na usiku kwa sasa, lakini kuna nyakati ambapo hulazimika kukipiga saa 8:00 mchana, na hilo Jamal anasema kuna mahali lina shinda na sehemu zingine fresh tu. “Nimewahi kucheza mechi nyingi saa nane mchana. Kwa hapa Mbeya hali ya hewa haisumbui, lakini ukienda mikoa yenye joto zinakuwa ngumu mno, hivyo naiomba Bodi ya Ligi iangalie namna ya kuondoa ratiba ya mchana.”

Kuhusu imani za kishirikina katika soka, anasema: “Kiukweli naamini ushirikina upo, lakini kwa upande wangu situmii kwa kuwa siamini kama unaweza kunisaidia kwa chochote, hivyo huwa upo lakini mimi si miongoni mwa wanaoamini kutumia.”

Chanzo: Mwanaspoti