Marouf Tchakei ambaye ni miongoni mwa maingizo mapya kwenye kikosi cha Singida Fountain Gate ameanza kujizolea umaarufu kwa mashabiki na wapenzi wa soka nchini kutokana na kile ambacho amekuwa akikionyesha akiwa na timu hiyo.
Tchakei aliyezaliwa Desemba 15, 1995 huko Bassar, Togo, alijiunga na wawakilishi hao wa nchi katika Kombe la Shirikisho Afrika akitokea AS Vita ya DR Congo kwa mkataba wa miaka miwili.
Nyota huyo ameonekana kuingia moja kwa moja kwenye mfumo wa Hans van der Pluijm huku akicheza katika nafasi ambayo alizoeleka kuonekana akitumika Bruno Gomes. Ubora wa kiungo huyo mshambuliaji kutoka Togo ambaye alitupia mabao mawili kwenye mchezo wa raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya JKU wakati wakiibuka na ushindi wa mabao 4-1 ni wazi kuwa utanogesha safu hiyo.
UTAMU ULIPO
Licha ya ugeni wake, Tchakei ameonyesha kuwa ni mchezaji mwenye uwezo wa kuunganisha timu kama ilivyokuwa kwa Bruno na kuipa faida nyingine ya mabao lakini pia amekuwa akiisaidia kuzuia.
Pluijm amekuwa akipenda wachezaji ambao wamekuwa wakijitoa zaidi kwa ajili ya timu hivyo ni wazi kuwa tutaendelea kumuona akitumika kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo.
Pamoja na kwamba Singida FG haikufua dafu mbele Simba kwenye mchezo wa ngao ya jamii, Mtogo huyo alikuwa mwiba kwenye ukuta wa wekundu hao wa Msimbazi, alionyesha kuwa na anakitu hata dhidi ya Azam wakati akitafutwa mshindi wa tatu kiasi cha kutoonekana pengo la Bruno ambaye alichelewa kujiunga na wenzake kwa ruhusu maalum.
Kuonyesha kwamba Pluijm hakufanya makosa kumuamini kwenye kikosi chake cha kwanza alipachika mabao mawili dhidi ya JKU na kuifanya Singida FG kuwa na nguvu kwenye eneo la kiungo mshambuliaji wakati huu ambao Bruno anajitafuta taratibu baada ya urejeo wake.
BRUNO AJIPANGE
Pluijm itabidi kufanya mambo mawili kwenye kikosi chake kuwatumia wote wawili, Bruno na Tchakei huku akipunguza nguvu kwenye eneo la kiungo ambalo wamekuwa wakicheza Yusuph Kagoma na Morice Chukwu.
Au mmoja kati yao aanze huku mwingine akisubiri, awatumie kulingana na mipango ya michezo ambayo itakuwa mbele yao.
Hakuna shaka juu ya uwezo wa Bruno akiwa kwenye kiwango chake kile ambacho kilizifanya Simba na Yanga kummezea mate msimu uliopita lakini kwa hiki ambacho ameanza kukionyesha Tchakei ni wazi kuwa Pluijm atakuwa na faida kwenye kikosi chake.
Mara baada ya kurejea kikosini, Bruno alisema kutoanza maandalizi ya msimu na wenzake kumemfanya kuchelewa kuchanganya hivyo anaamini atakuwa sawa na kuendelea kuisaidia timu kwa kushirikiana na wachezaji wapya ambao wameingia dirisha hili.
HUKU FRESHI
Mbali na kuwa na uwezo mkubwa wa kucheza nyuma ya mshambuliaji au mshambuliaji wa uongo, Tchakei anaweza kushambulia akitokea pembeni hasa kulia upande ambao kwenye kikosi cha Singida FG anaonekana kufanya vizuri Duke Abuya huku kushoto akiwa Dickson Ambundo.
Eneo lingine ambalo anaweza kucheza ni kiungo mkabaji hapa unaweza usipate ubora wake kwani kucheza kwake chini kutamnyima uhuru wa kuwa karibu na eneo la hatari la wapinzani.
MSIKIE PLUIJM
Pluijm anafurahia kile ambacho anakionyesha Tchakei na anaamini kwa kushirikiana na wenzake wanaweza kuwa tishio kwenye ligi na hata kufikia lengo la kutinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho.
“Ni kijana mzuri na msikivu sana, nimekuwa nikiongea naye ili kuhakikisha anaendana na aina yetu ya uchezaji, kuna vingi ambavyo anaweza kuonyesha tumpe muda maana anaendelea kuzoeana na wachezaji wenzake,” anasema kocha huyo. Kuhusu nafasi ya Bruno kwenye kikosi chake, Pluijm anasema:
“Tunajua kazi kubwa aliyoifanya msimu uliopita, hakuwa na sisi katika maandalizi yetu hivyo taratibu atakuwa sawa na wenzake na kuendelea kuisaidia timu, naamini tunaweza kugombani mataji.”
Bruno alichelewa kujiunga na wenzake kwenye maandalizi ya msimu huu wa mashindano 2023/24 kutokana na kuwa kwao Brazil ambako alienda kufunga ndoa na mpenzi wake wa muda mrefu, Nathalia.
Timu hiyo ambayo inashiriki Ligi Kuu Bara msimu huu ukiwa ni pili, imeanza kuwa tishio kwa vigogo kutokana na usajili ilioufanya wa maingizo mengi kikosini yaliyoanza kuifanya ianze kutabiriwa mengi.