Kamati ya Marekebisho ya Katiba ya Klabu ya Simba imefanya kikao chake cha kwanza Desemba 21, 2023 kupitia mapendekezo na maoni ya marekebisho ya katiba yao yaliyotolewa na wanachama wao.
Simba ilielekezwa na RITA pamoja na Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kufanya marekebisho ya Katiba baada ya kubainika kuwa na mapungufu ambayo yalipelekea kukwamisha mchakato wa mabadiliko ya uendeshaji wa klabu kukwama.
Marekebisho ya Katiba ya Simba ni moja ya ajenda ya mkutano wa mwaka unaotarajiwa kufanyika Januari na kwa mujibu wa taarifa ya klabu hiyo iliyotolewa leo Jumanne, Desemba 26, 2023, kamati inawashukuru wote ambao wametoa mapendekezo yao na inaahidi kuyafanyia kazi.
Taarifa imesema: "Kamati inawataarifu wanachama wote kuwa pamoja na maeneo mahususi ambayo Serikali ilielekeza kufanyiwa marekebisho kupitia RITA na BMT pia maoni ya wanachama na wapenzi wa klabu yatazingatiwa."
Mchakato huo umeanza wiki iliyopita, mwisho wa kutoa maoni hayo ni Desemba 31, 2023 saa 6:00 mchana na Desemba 30 kamati hiyo itakutana tena kabla ya kufunga zoezi hilo.
Kamati hiyo imeendelea kuwasisitiza wadau wake ambao ni wanachama kuwasilisha maoni yao kupitia njia walizoelekezwa kutuma ama kupelekea kwenye ofisi za Simba moja kwa moja.
Kamati hiyo maalumu inaongozwa na Mwenyekiti, Wakili Hussein Kitta akisaidiwa na Makamu wake, Wakili Aziza Omary Msangi huku wajumbe ni Ustaadh Masoud, Zulfika Chandoo, Wakili Moses Kaluwa, Hamis Mkomwa na Mohammed Soloka.
Simba ipo kwenye mchakato wa kurekebisha mfumo wa uendeshaji wa klabu hiyo ili uwe wa hisa ambapo wanachama watakuwa wanamiliki asilimia 51 wakati mwekezaji atakuwa na asilimia 49 ambaye kwa sasa anatambulika ni Mohammed ‘Mo’ Dewji.