Wawakilishi wa Tanzania kwenye Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika Simba na Yanga zinashuka dimbani wikiendi hii zikiwa ugenini nchini Morocco na DR Congo kwa ajili ya kuhitimisha hatua ya makundi baada ya kujihakikisha nafasi ya kufuzu robo fainali ya michuano hiyo.
Simba yenye pointi tisa katika kundi 'C' itacheza na vinara Raja Casablanca Aprili 1, huku Yanga ikihitaji pia kuweka tu heshima itakapocheza na TP Mazembe Aprili 2.
Wakati miamba hiyo ikiwa dimbani, tayari Shirikisho la Soka Afrika CAF limetangaza waamuzi watakaochezesha mechi hizo ambapo kwa Simba itachezeshwa na Ahmad Heeralall kutoka Mauritania huku kwa upande wa Yanga mwamuzi wa kati atakuwa ni Lahlou Benbraham wa Algeria.
Rekodi zinaonyesha katika michezo 13 ya Kimataifa aliyochezesha mwamuzi, Ahmad Heeralall ni mechi moja tu ambayo hajatoa kadi ya njano huku nyekundu ikiwa ni moja.
Katika michezo hiyo timu za nyumbani zimeshinda mechi nane, sare minne huku ya ugenini ikishinda mmoja tu ambao ulikuwa wa Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya makundi ambapo Yanga ilipoteza kwa mabao 3-2 dhidi ya Gor Mahia ya Kenya, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa Julai 29, 2018.
Kwa upande wa mwamuzi wa mechi ya Yanga, Lahlou amechezesha michezo 10 ambapo kati ya hiyo ametoa kadi za njano 31 na nyekundu moja tu. Kwenye michezo hiyo 10 aliyochezesha timu zilizocheza nyumbani zimeshinda mitano, sare miwili huku zile za ugenini zikishinda mechi tatu tu.
Ushindi mkubwa kwa timu iliyokuwa nyumbani ambayo mwamuzi huyo alichezesha ni ule wa Wydad Casablanca ya Morocco ilipoibuka na ushindi wa mabao 5-1 dhidi ya Petro de Luanda kutoka Angola kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika katika mechi iliyopigwa Aprili 3, mwaka jana.