Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Maradhi chanzo cha kuachana na Soka kwa nyota hawa

Maradhi Pic Data Kuna nyota kadhaa ambao maradhi ya moyo ndio chanzo cha kustaafu Soka

Wed, 17 Nov 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Habari ya kushtua kutoka Hispania zimeripoti nyota wa Barcelona, Sergio Aguero huenda akastaafu kucheza soka kutokana na matatizo ya moyo anayokabiliana nayo kwa sasa.

Straika huyo wa zamani Manchester City alishindwa kuendelea na mechi ya La Liga, Barcelona ilipomenyana na Alaves, iliyopigwa mwezi uliopita kwenye Uwanja wa Camp Nou baada ya kushindwa kupumua vyema.

Aguero mkali wa mabao wa muda wote Man City alipelekwa hospitali kufanyia vipimo vya moyo, huku taarifa zikiripoti kwamba atakaa nje ya uwanja kwa muda wa miezi mitatu baada ya uchunguzi.

Baada ya vipimo vya Aguero kutolewa, imebainika majibu ya vipimo hivyo si mazuri kama ilivyodhaniwa, huenda akastaafu kucheza soka kutokana na matatizo ya moyo yanayomkabili.

Aguero amekuwa na wakati mgumu tangu alipotua Camp Nou akikabiliwa na maumivu ya kifundo cha mguu yaliomweka nje ya uwanja kwa muda wa mwezi mmoja.

Wakati anakipiga Etihad nyota huyo wa Kimataifa wa Argentina amecheza jumla ya mechi 275 na kufunga mabao 184 akifanya hivyo kuanzia msimu wa 2011 hadi 2021.

Wafuatao ni baadhi ya mastaa wa zamani waliostaafu kucheza soka kutokana matatizo ya moyo.

Ruben de la Red

Mwanzoni alikuwa mchezaji mwenye kipaji wakati huo anakipiga Real Madrid.

Mbali na Madrid staa huyo alikiwasha kila alipoitwa timu ya taifa ya Hispania kucheza michuano mbalimbali.

Lakini matatizo ya moyo aliyokuwa akikabiliana nayo yalimlazimisha mwanandinga huyo kustaafu kucheza mwaka 2010 akiwa na umri wa miaka 25. Ruben alijipa matumaini kwamba angerejea uwanjani lakini mambo hayakuwa hivyo, timu nyingine aliowahi kucheza ni Getafe.

Fabrice Muamba

Muamba alianza kucheza soka akiwa Arsenal kabla ya kujiunga na Birmigham City baadaye akahamia Bolton Wonderers.

Mwaka 2012 wakati wa mechi ya robo fainali ya Kombe la FA dhidi ya Tottenham, Muamba alidondoka uwanjani kutokana mshtuko wa moyo kwa muda wa dakika 78.

Baada ya tukio hilo Muamba aliwahishwa hospitalini kufanyiwa vipimo lakini alistaafu kucheza soka baadaye akiwa na umri wa miaka 24.

Stiliyan Petrov

Petrov alikuwa mchezaji muhimu wa Aston Villa tangu alipojiunga nayo mwaka 2006 akitokea Celtic.

Nyota huyo hakuendelea kucheza soka baada ya kuugua ghafla wakati huo akiwa na umri wa miaka 32 mwaka 2012.

Alifunga mabao 62 yakijiumuishwa na yale aliyotupia wakati anaichezea Celtic kabla ya kuhamia Aston Villa.

Baada ya kugundulika ana saratani ya damu Patrov alianza matibabu haraka iwezekanavyo.

Baada ya miezi kadhaa Petrov alirejea kambini kujiandaa na msimu mpya (Pre-season), lakini hakudumu sana alistaafu kucheza soka akiwa na umri wa miaka 32.

Chris Naumoff

Nyota huyu hakuwa na jina kubwa wakati anacheza soka kipindi hicho.

Naumoff alijulikana sana kipindi anacheza Ligi Kuu Australia inayofahamika kwa jina la A-League.

Nyota huyo alitabiriwa makubwa lakini ndoto zake zikayeyuka ghafla, licha ya kushinda tuzo ya mchezaji bora wa msimu mwaka 2014 wa ligi hiyo.

Ndoto za kinda huyo ziliishia ukingoni baada ya kugundulika ana matatizo ya moyo, yaliyosababisha dili lake la kujiunga na moja ya timu kutoka Hispania kugonga mwamba kustaafu akiwa na umri wa miaka 21.

Abdelhak Nouri

Nouri alipata mshuko wa moyo wakati wa mechi ya kirafiki ya kujiandaa na msimu mpya mwaka 2017 akiwa na timu ya Ajax.

Mbali na mshtuko wa moyo Nouri alipoteza fahamu kutokana na hitilafu ya ubongo iliyosababisha fahamu zake kupotea kwa muda miaka miwili.

Ajax ilihudumia matibabu ya Nouri hadi alipopata fahamu mwaka jana, lakini ilivunja mkataba wake ambao alisaini nao wakati anichezea timu hiyo.

Nouri amesataafu kucheza soka lake la kulipwa akiwa na umri wa miaka 24 kwa sasa huku hali yake ikiendelea kuonyesha matumaini baada ya kuamka kwa mujibu wa ripoti.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz